• HABARI MPYA

    Wednesday, May 09, 2012

    OWEN ATUA YANGA KULIPIA KISASI CHA OKWI MSIMU UJAO


    Owen Kasule

    KIUNGO wa timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’, Owen Kasule ametua Dar es Salaam kufanya mazungumzo ya usajili na uongozi wa timu ya Yanga ya Dar es Salaam.
    Gazeti la Habari Leo, limeandika kwamba Kasule alifika Dar es Salaam juzi, ambapo jana alifanya mazungumzo ya muda mrefu na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga inayoongozwa na Salum Rupia kuhusiana na
    kusajiliwa na timu hiyo kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
    Habari zilizopatikana ndani ya Yanga jana na kuthibitishwa na Rupia pamoja na Kasule zilieleza kuwa mazungumzo hayo yalikuwa mazuri, lakini kuna mambo ya kimsingi ambayo yaliwakwamisha kufikia mwafaka.
    Rupia alikiri kuzungumza na Kasule jana, lakini alisema hawakusaini naye mkataba kwani amewaambia anaenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika timu ya Al Ahly ya Misri na kwamba kama atakwama huko atakuja kusaini Yanga.
    Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Usajili alisema, Kasule amewaeleza kuwa ni rafiki wa karibu wa mshambuliaji Hamisi Kiiza wa Yanga na Emmanuel Okwi wa Simba ambao amesoma nao shule Uganda, hivyo wanapomjulisha habari za soka la Tanzania anatamani sana kuja kucheza.
    “Ametwambia ana mapenzi sana na Yanga, hivyo naamini atakuja,” alisema Rupia. Okwi na Kiiza ni miongoni mwa wachezaji wa nje waliong’ara kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara iliyomalizika Jumapili.
    Kwa upande wake Kasule akizungumza jana akiwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kabla ya kurejea kwao, alikiri kuzungumza na Yanga, lakini akisema kuna mambo hawajafikia mwafaka.
    “Mazungumzo yetu hayajaisha, nitakujulisha kwa kirefu zaidi, lakini kwa sasa hapana, elewa kwamba tumezungumza na Yanga,” alisema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: OWEN ATUA YANGA KULIPIA KISASI CHA OKWI MSIMU UJAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top