Na Ezekiel Kamwaga, Khartoum
WAPINZANI wa
Simba katika michuano ya Kombe la Shirikisho (CAF), Al Ahly Shendi ya Sudan,
tayari wameanza visa. Leo hii, wachezaji na viongozi wa Simba wametelekezwa kwa
takribani masaa matano hotelini na wenyeji hao ambao walikuwa wameahidi
kuipeleka Simba katika mji wa Shendi. Wenyeji wa Simba nchini hapa ambao ni
Shendi na Chama cha Mpira wa Miguu Sudan (SFA), walikuwa wameahidi jana kwamba
Wekundu wa Msimbazi wataanza safari ya kwenda Shendi mara baada ya kupata
kifungua kinywa saa tatu asubuhi. Hata hivyo, hadi kufikia saa nane mchana,
hakukuwapo na basi lolote au mwakilishi yeyote wa kutoka Shendi au SFA
aliyekwenda kwenye Hoteli ya Safiga ilikofikia Simba na kwa mujibu wa
mawasiliano, walidai kwamba wamekwama kwenye foleni. Hali hiyo ilisababisha
wachezaji na viongozi wa Simba kushinda nje ya hoteli hiyo wakiwa wamekaa nje
kwenye viti vichache, huku wengine wakiwa wamesimama tu kwa muda wa zaidi ya
masaa mawili hadi matatu kwa vile muda wa kutoka hotelini ulikuwa umepita. Kwa
mujibu wa kanuni ya 14 (b) ya mashindano yanayosimamiwa na CAF, timu yeyote
inatarajiwa kusafirishwa kutoka eneo moja kwenda jingine katika muda ambao
unakubalika, labda kama imechelewa yenyewe. Kuna umbali wa kilomita 150 kutoka
mji mkuu wa Sudan, Khartoum iliko Simba hadi mji wa Shendi na kama Simba
itachelewa kuondoka jijini hapa, maana yake ni kwamba itashindwa kufanya
mazoezi leo jioni na hivyo Shendi na SFA wamekiuka kanuni hiyo. Akizungumzia
hali hiyo, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alieleza kuchukizwa kwake na
tukio hilo akisema linaonyesha namna Shendi na SFA walivyojipanga kutumia mbinu
za nje ya uwanja kushinda pambano hilo la marudiano. Katika pambano la kwanza
lililofanyika jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita, Simba iliibuka na
ushindi wa mabao 3-0. “Sisi tulitaraji kukumbana na yote haya ambayo tunayaona
sasa. Wanajua kwamba hawataweza kuishinda Simba ndani ya uwanja na hivyo
wameamua kutumia mbinu chafu. “Bahati nzuri, wachezaji wetu, benchi la ufundi
na sisi viongozi tumejiandaa kikamilifu kwa mambo kama haya. Hata hivyo,
tutapeleka mashitaka yetu kwa kamisaa wa mechi yetu kwa vile wao Shendi
walipokuja Dar tuliwahudumia vizuri kwa kila kitu,” alisema. Kutokana na
kuchelewa huko kuondoka, hoteli ya Safiga haikuwa imeandaa chakula cha mchana
kwa wachezaji na ilibidi Rage na daktari wa timu, Dk. Cosmas Kapinga, waende
kutafuta “vipoza njaa” kwa wachezaji wa Wekundu wa Msimbazi. Kwa upande wake,
Dk. Kapinga alisema inachofanyiwa Simba ni kitu ambacho kwa kitaalamu kinaitwa
uchoshwaji wa kisaikolojia, lengo lake likiwa kuiathiri timu kiakili. “Katika
mazingira kama haya, wachezaji na viongozi wanashindwa kufikiria kuhusu mechi
na badala yake wanafikiria kuhusu adha wanazozipata. Kama watakuwa
hawajaandaliwa vizuri kisaikolojia, hii inaweza kuwa mbaya. Kwa bahati nzuri,
wachezaji wa Simba wameandaliwa vizuri kwenye eneo hilo,” alisema Kapinga
SOURCE: DINA ISMAIL
(mamapipiro.blogspot.com)


.png)
0 comments:
Post a Comment