![]() |
Kikosi cha Simba |
BAADA ya kumaliza Ligi Kuu bara kwa
kishindo, Simba sasa inajipanga kwa safari ya kwenda Sudan kwa ajili ya mechi
ya michuano ya kimataifa, na imepanga kuondoka kesho kwa ndege ya kukodi.
Gazeti la Habari leo, limeandika kwamba Simba
iliifunga Yanga mabao 5-0 juzi katika mechi ya mwisho ya Ligi hiyo na hivyo
kunogesha furaha za kutwaa ubingwa ilioutwaa tangu Ijumaa iliyopita.
Akizungumza Dar es Salaam jana, makamu
mwenyekiti wa Simba Godfrey Nyange ‘Kaburu’ alisema kuwa timu yao itaondoka
kesho kwa ndege ya kukodi kuelekea Sudan kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa
Kombe la shirikisho dhidi ya Al Ahly Shandy ya huko.
Katika mechi ya kwanza ya raundi ya tatu ya
michuano hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa takriban wiki moja iliyopita, Simba
ilishinda kwa mabao 3-0 na hivyo kuhitaji sare ama ushindi wa aina yoyote
kwenye mechi hiyo ili kufuzu kwa hatua inayofuata.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Simba,
Ismail Aden Rage amesema kuwa mafanikio ya timu yao msimu huu yanatokana na
ushirikiano mzuri kati ya uongozi wa sasa, uongozi uliopita na marafiki wa
klabu hiyo ‘Friends of Simba’.
Rage akizungumza baada ya ushindi wa juzi
dhidi ya Yanga, alisema kuwa mshikamano uliokuwepo ndani ya klabu hiyo kwa sasa
ndio siri ya mafanikio ya timu yao.
Alisema kuwa siku zote panapokosekana
mshikamano madhubuti miongoni mwa wanachama wa klabu hiyo lazima timu yao
inakuwa haifanyi vizuri, lakini kwa sasa kwa kuwa wako pamoja ndio maana
mafanikio yanaonekana.
Alisema ana furaha kuhitimisha furaha yao
ya kutwaa ubingwa kwa kuifunga Yanga kwani ubingwa wao usingenoga kama
wasingeibuka na ushindi dhidi ya timu hiyo yenye upinzani wa kihistoria na
vijana hao wa Msimbazi.
Aliongeza kuwa alijua fika kuwa
wangeifungaYanga kwa idadi hiyo ya mabao kwani hata wakati anazungumza na kituo
kimoja cha redio kabla ya mechi hiyo aliwaeleza wazi kuwa wataifunga
Yanga kwa mabao matano.
Aidha, alisema kuwa timu yao sasa imeiva
kimazoezi na kwamba inaweza kuhimili dakika 90 za mchezo bila kuchoka tofauti
na zamani ambapo baada ya kuingia kipindi cha pili vijana wao walikuwa wakionekana kuchoka haraka.
0 comments:
Post a Comment