SHIRIKISHO la Soka la Tanzania (TFF),
limempa kocha wa timu za vijana za Tanzania, Kim Poulsen, jukumu jipya la
kuinoa timu ya wakubwa, Taifa Stars na kumpiga chini kocha wa sasa, Jan
Poulsen.
Gazeti la Mwanaspoti leo, limeandika kwamba Kim, ambaye yupo na Ngorongoro nchini Sudan
atarudi Jumatatu na kutangaza kikosi cha Taifa Stars kujiandaa kwa mchezo dhidi
ya Ivory Coast, Juni Mosi.
Jan amekamilisha mkataba wake mwisho wa
mwezi uliopita na mpaka sasa hakuna mazungumzo yoyote ya kuongeza muda
yaliyofanyika.
Duru za ndani ya TFF zimethibitisha kwamba
hatakiwi tena na Kim amepewa jukumu hilo la kuongoza Taifa Stars.
Hiyo inamaanisha kwamba Kim aliyeletwa
nchini kwa mapendekezo ya Jan, sasa yupo na Ngorongoro Heroes nchini Sudan
lakini Juni Mosi ataiongoza Stars nchini Ivory Coast kwenye mechi ya kufuzu
Kombe la Dunia na baadaye dhidi ya Gambia Juni 6.
Baada ya hapo ataiongoza Stars pia kwenye
mechi dhidi ya Msumbiji ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika
zitakazochezwa mwakani.
Kim ameshaambiwa suala hilo na tayari
ameanza kufuatilia mechi mbalimbali za Ligi Kuu mikoani Dar es Salaam
kutengeneza kikosi chake kipya ambacho watu wake wa karibu wanadai kitakuwa na
vijana wengi tofauti na Stars ya sasa.
Jan amekuwa kwenye wakati mgumu katika siku
za karibuni kutokana na kuyumba kwa timu hiyo kwenye michuano mikubwa huku
akiwaacha mastraika, Danny Mrwanda wa klabu ya DT Long ya Vietnam na Mbwana
Samatta wa TP Mazembe kwa madai kuwa hawajitumi.
Kuwaondoa wachezaji hao kikosini kumemweka
kwenye wakati mgumu kwa vile walioziba nafasi zao wameshindwa kuonyesha jipya
walilonalo.
TFF ilimtaka Jan kutangaza kikosi cha Taifa
Stars jana Ijumaa, lakini aligoma kwa madai kuwa yeye si kocha wa timu hiyo na
kesho Jumapili anakwenda Nigeria katika kazi zake za ukufunzi.



.png)
0 comments:
Post a Comment