TIMU ya taifa ya soka ya wanawake ya
Zimbabwe imefurahia kucheza mechi ya kirafiki na Tanzania (Twiga Stars)
itakayofanyika Jumamosi (Mei 12 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini
Dar es Salaam leo, Kocha Mkuu wa Zimbabwe, Rosemary Mugadza amesema wamefurahi
kupata mechi hiyo kwa vile wanaamini Twiga Stars ni kipimo kizuri kwao kabla ya
kucheza mechi yao ya mashindano ya Afrika dhidi ya Nigeria.
Amesema anaijua vizuri Twiga Stars, kwani
mwaka jana alicheza nayo mara mbili. Mara ya kwanza ilikuwa kwenye nusu fainali
ya Kombe la COSAFA ambapo katika mechi hiyo iliyochezwa Julai 5 jijini Harare,
Zimbabwe ilishinda kwa penalti 4-2.
Mechi ya pili ilikuwa kwenye michezo ya All
Africa Games (AAG) iliyofanyika Maputo, Msumbiji ambapo katika mechi yao
iliyochezwa Septemba 11 timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2. Mabao ya Twiga
Stars yalifungwa na Asha Rashid na Mwanahamisi Shuruwa.
Mugadza amesema sababu nyingine
iliyowafanya watake kucheza na Twiga Stars ni kwa vile ilishacheza na Nigeria
kwenye fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) zilizofanyika Afrika Kusini mwaka
2010. Twiga Stars ilifungwa na Nigeria mabao 2-1.
Kocha huyo amesema hiyo itakuwa mechi ya
pili kujipima nguvu kabla ya kuivaa Nigeria. Mwishoni mwa wili iliyopita
Zimbabwe ilicheza mechi ya kirafiki jijini Harare dhidi ya Zambia na kushinda
mabao 2-1.
Zimbabwe ambayo iliwasili jana (Mei 9 mwaka
huu) saa 1.30 usiku kwa ndege ya South African Airways (SAA) ina msafara wa
watu 28 ambapo kati ya hao 20 ni wachezaji wakati waliobaki ni benchi la ufundi
na viongozi wa timu hiyo.
Viingilio katika mechi hiyo kati ya Twiga
Stars na Zimbabwe itakayochezwa kuanzia saa 10.30 jioni ni sh. 1,000 tu kwa
sehemu zote isipokuwa VIP A ambayo ni sh. 10,000 na VIP B ambayo kiingilio
chake ni sh. 5,000.
Twiga Stars ilikuwa katika ziara ya mechi
za kirafiki katika mikoa ya Dodoma na Mwanza na inatarajia kurejea kesho (Mei
11 mwaka huu) tayari kwa mechi hiyo itakayochezwa na mwamuzi wa kimataifa
Judith Gamba.



.png)
0 comments:
Post a Comment