![]() |
Waziri Mkuu wa zamani, Mh Frederick Sumaye akihutubia jana katika tuzo za washindi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, hoteli ya Double Tree, Masaki, Dar es Salaam. |
Na Prince Akbar
WAZIRI Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye amesema kwamba soka
ya Tanzania kwa sasa imepoteza umaarufu wake, tofauti na ilivyokuwa awali
kuanzia miaka ya 1970.
Akizungumza jana katika halfa ya kukabidhi tuzo za washindi mbalimbali
wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, iliyofanyika katika hoteli ya Double Tree
By Hilton, Masaki, Dar es Salaam, Sumaye alisema kwamba sababu ya kuporomoka
kwa soka yetu ni mtazamo wa hapa hapa wa klabu zetu.
Sumaye alitolea mfano vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga
na kusema kwamba timu moja ikimfunga mwenzake inaona imemaliza na haifanyi
jitihada za ziada za kufika mbali zaidi.
“Umefika wakati timu zetu zijifunze kwa timu za nje, hata
timu nyingine hizi zinazosifiwa kuibuka kuja kuvipiku vigogo vya soka (Simba na
Yanga), nazo zikifunga Simba au Yanga, zinaona zimemaliza, lazima tubadilike
tufikirie kufika mbali zaidi,”alisema Sumaye.
Waziri Mkuu huyo, ambaye kuna tetesi ataomba ridhaa ya
kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM katika
uchaguzi Mkuu ujao, mwaka 2015, alisema kwamba Watanzania kwa sasa wanaangalia
zaidi soka ya nje kuliko ya nyumbani kutokana na kushuka kwa mchezo huo hapa
nchini.
“Ili turudishe heshima, lazima tupambane kurudisha kiwango,
tufikirie kuwa kama timu nyingine za Afrika zinazofanya vizuri, sio kuishia
kuangaliana hapa hapa wenyewe kwa wenyewe,” alisema.
Aidha, Sumaye alisema anasikitishwa na desturi ya Simba na
Yanga kuzomeana zinapocheza na timu za nje na akashauri wakati umefika sasa
kuachana na desturi hiyo yenye kutia aibu.
“Tuvuke huko, tuwe tunazomeana nyumbani tu, wewe
unashangilia timu ya Burundi, una uhusiano nao gani? Tuwe na uzalendo na
tutafika mbali,”alisema Sumaye, ambaye ni kipenzi cha Watanzania wengi,
kutokana na kumbukumbu ya uongozi bora akiwa Waziri Mkuu wa Rais Benjamin Mkapa
katika awamu ya tatu.
Aidha, Sumaye pia alielezea kukerwa na migogoro katika soka
ya Tanzania pamoja na viongozi wa klabu kutojali maslahi ya wachezaji na akaasa
hayo yaepekwe ili kukuza soka yetu.
“Mimi nachukizwa sana naposikia migogoro, tunagombea nini? Kama
mimi nitaomba nafasi kwa maslahi ya jamii, siwezi kupambana kwa kufa na kupona,
lakini kama nitaomba uongozi kwa maslahi binafsi, nitapambana kufa na kupona.
Naomba viongozi wa sasa, amueni kutumikia klabu na kujali maslahi
ya wachezaji. Wachezaji wetu wanaingia uwanjani tayari miguu haina nguvu, kwa
sababu sisi viongozi tunawanyonya,” alisema Sumaye, ambaye ni mpenzi wa Simba
SC.
Pamoja na ukweli huo kwamba yeye ni ‘Simba damu’, ila Sumaye
alisema anapenda timu ambayo inafanya vizuri uwanjani.
Serikali ya awamu ya tatu, ambayo Waziri Mkuu wake alikuwa
Sumaye, ilifanya mambo mengi katika sekta ya michezo ikiwemo kujenga Uwanja wa
kisasa wa michezo, Uwanja wa Taifa
Katika sherehe hizo za utoaji tuzo kwa wanamichezo bora jana
usiku, hoteli ya
Double Tree By Hilton, Masaki, Dar es Salaam, beki Aggrey Morris anayechezea Azam
aliibuka mchezaji bora wa ligi hiyo wakati Juma Kaseja anayedakia Simba alikuwa kipa
bora.
Kila mmoja alizawadiwa sh. 3,312,500 katika hafla hiyo
ambayo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye. Kaseja
aliwashinda makipa Mwadili Ally (Azam) na Deogratias Munishi (Mtibwa Sugar)
wakati Morris aliwashinda Haruna Niyonzima (Yanga) na Haruna Moshi (Simba).
John Bocco wa Azam aliyefunga mabao 19 ndiye mfungaji bora,
refa bora ni Martin Saanya kutoka Morogoro ambaye aliwashinda Oden Mbaga (Dar
es Salaam) na Amon Paul (Mara) wakati kocha bora ni Stewart Hall wa Azam
aliyewashinda Charles Kilinda (JKT Ruvu) na Charles Mkwasa (Ruvu Shooting).
Kila mshindi mepata sh. 3,875,000.
Timu yenye nidhamu bora ni Azam iliyopata sh. 7,750,000,
mshindi wa tatu Yanga sh. 15,500,000, makamu bingwa Azam sh. 22,000,000 na
bingwa Simba sh. 50,000,000.
Pia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
limewazawadia sh. 1,000,000 kila mmoja kwa wachezaji watatu vijana wenye umri
chini ya miaka 20 waliofanya vizuri kwenye ligi hiyo.
Wachezaji hao ambao walikuwa kwenye vikosi vya kwanza vya
timu zao ni Frank Domayo (JKT Ruvu), Rashid Mandawa (Coastal Union) na Hassan
Dilunga (Ruvu Shooting).
0 comments:
Post a Comment