• HABARI MPYA

    Monday, August 13, 2012

    MATOLA: AZAM HAWATISHI, SIHITAJI 'MAFAZA' KUWANG'OA SUPER 8


    Kocha Matola
    Na Prince Akbar, Mwanza
    KOCHA Mkuu wa Simba B, Suleiman Abdallah Matola amesema kwamba haihofii hata chembe Azam FC, kuelekea Nusu Fainali ya michuano ya BankABC Sup8r keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY mjini hapa, Nahodha huyo wa Simba SC alisema kwamba anawaamini sana vijana wake kwamba wanaweza kuitoa Azam inayotumia nyota wake wa Ligi Kuu wenye uzoefu.
    “Yaani katika mashindano haya siihofii timu yoyote. Na sihitaji mchezaji hata mmoja wa timu ya kwanza ili kuitoa Azam, hawa vijana nilionao nawaahidi wapenzi wa Simba kwamba watachukua Kombe hili,”alisema Matola.
    Matola amewataka wapenzi wa Simba SC kumiminika kwa wingi Uwanja wa Taifa, Jumatano katika Nusu Fainali hiyo, itayochezwa Saa 10:00 jioni baada ya Nusu Fainali ya Kwanza, kati ya Mtibwa Sugar na Jamhuri ya Pemba.
    Simba B ilitinga Nusu Fainali ya michuano ya BankABC Sup8r kwa kishindo jana, baada ya kuifunga Zimamoto ya Zanzibar mabao 2-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, mabao yake yote yakifungwa na kiungo chipukizi anayeinukia vema katika soka ya Tanzania, Christopher Edward kipindi cha pili.
    Christopher ambaye hukomazwa pia kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na kikosi cha kwanza cha Simba, alifunga bao la kwanza penalti dakika ya 50, baada ya beki Miraj Adam kuangushwa kwenye eneo la hatari.
    Edward ambaye ni kipenzi cha kocha Mserbia wa Simba, Profesa Milovan Cirkovick, alifunga bao la pili dakika ya 55 baada ya kuwapiga chenga mabeki watatu wa Zimamoto kabla ya kumchambua kipa wa timu hiyo ya Zanzibar.
    Pamoja na Simba SC kuwania ubingwa wa michuano hiyo, lakini sasa Christopher ameingia kwenye mbio za kiatu cha dhahabu cha michuano hiyo, kwa kufikisha mabao manne, akiwa anaongoza.
    Katika michezo mingine ya kuhitimisha hatua ya makundi ya michuano hiyo jana Uwanja wa Chamazi, Jamhuri FC iliichapa 4-0 Mtende, zote za Zanzibar mabao ya washindi yakifungwa na Sadik Rajab dakika ya 20, 44, Issa Achimwene aliyejifunga dakika ya 82 na Suleiman Khatib dakika ya 88.
    Kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, Azam FC ilitoka nyuma kwa bao 1-0 na kuifunga Polisi Moro FC mabao 2-1, mabao yake yakitiwa kimiani na beki Said Mourad dakika ya 20 na Abdi Kassim ‘Babbi’ dakika ya 70, wakati la Maafande wa Morogoro lilitiwa kimiani na Mokili Rambo dakika ya kwanza. Polisi ilimpoteza mchezaji wake, Abdallah Rajab dakika ya 88 aliyetolewa nje kwa kadi nyekundu.
    Uwanja wa Amaan, Zanzibar, Mtibwa Sugar iliichapa 5-0 Super Falcon FC katika mchezo wa mwisho wa makundi. Mabao yake yakitiwa kimiani na Shaaban Kisiga ‘Malone’ mawili, Dickson Daud, Mohd Mpoki na Ally Mohd ‘Gaucho’.
    Katika Kundi A, Simba SC imeongoza kwa pointi zake nne, baada ya kutoa sare moja na kushinda moja, ikifuatiwa na Zimamoto na Mtende zinazofungana kwa pointi tatu kila moja, wakati Jamhuri inashika mkia kwa pointi yake moja.
    Kundi B, Mtibwa inaongoza kwa pointi zake tisa ikifuatiwa na Azam FC na Polisi Moro, zenye pointi tatu kila moja, wakati Falcon inashika mkia, ikiwa haina pointi hata moja.
    Wakati hatua ya makundi inamalizika leo, mechi za Nusu fainali na fainali zote zitachezwa Dar es Salaam. Mdhamini wa michuano hiyo, Banc ABC anagharamia usafiri wa ndege kwa timu zote kutoka kituo kimoja hadi kingine, malazi na jezi.
    Kanuni za mashindano haya ni kushirikisha timu zilizoshika nafasi tatu za juu katika Ligi Kuu za Bara na visiwani na mbili zilioongoza katika kupanda Ligi Kuu zote mbili, lakini kwa Bara, Yanga waliokuwa washindi wa tatu msimu uliopita, walijitokea na nafasi yao ikachukuliwa na Mtibwa Sugar ambayo ilishika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu.
    Bingwa wa michuano hiyo mipya itakayokuwa ikifanyika kila mwaka, ataondoka na Sh. Milioni 40, mshindi wa pili Sh. Milioni 20, wa tatu Sh. Milioni 15 sawa na wa nne, wakati washiriki wengine wataondoka na Sh. Milioni 5 kila moja.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MATOLA: AZAM HAWATISHI, SIHITAJI 'MAFAZA' KUWANG'OA SUPER 8 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top