Na
Princess Asia, Zanzibar
SHAABAN Kisiga ‘Malone’
aliyekuwa anacheza soka ya kulipwa Uarabuni, amerejea nyumbani kwa kishindo,
safari kama mfungaji hodari wa mabao na si mpishi tena kama alivyozoeleka.
Kiungo huyo wa zamani
wa Bandari ya Mtwara, SC Villa ya Uganda, Simba SC na Azam FC za Dar es Salaam
jana alifunga mabao mawili wakati timu yake mpya, Mtibwa Sugar inaifunga 5-0 Super
Falcon katika michuano ya BankABC Sup8r kwenye Uwanja wa Amaan,m Zanzibar.
Kisiga ambaye aliporejea
nchini kwanza alienda kuomba kusajiliwa Simba SC wakampotezea, sasa amefikisha
mabao matatu na anachuana na chipukizi wa Simba SC, Christopher Edward kuwania
kiatu ncha dhahabu cha michuano hiyo.
Katika mechi hiyo ya
jana, mabao mengine ya Mtibwa yalifungwa na Ally Mohamed ‘Gaucho’, Mohamed Mpoki
na Dickson Daudi.
Mtibwa sasa imeungana
na Azam iliyoshika nafasi ya pili Kundi B, Simba na Jamhuri kutoka Kundi A
kutinga Nusu Fainali ya michuano hiyo.
Simba ilitinga Nusu Fainali ya michuano ya
BankABC Sup8r kwa kishindo jana, baada ya kuifunga Zimamoto ya Zanzibar mabao
2-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, mabao yake yote yakifungwa na
kiungo chipukizi anayeinukia vema katika soka ya Tanzania, Christopher Edward
kipindi cha pili.
Christopher ambaye hukomazwa pia kwenye kikosi cha timu ya
taifa ya Tanzania, Taifa Stars na kikosi cha kwanza cha Simba, alifunga bao la
kwanza penalti dakika ya 50, baada ya beki Miraj Adam kuangushwa kwenye eneo la
hatari.
Edward ambaye ni kipenzi cha kocha Mserbia wa Simba,
Profesa Milovan Cirkovick, alifunga bao la pili dakika ya 55 baada ya kuwapiga
chenga mabeki watatu wa Zimamoto kabla ya kumchambua kipa wa timu hiyo ya
Zanzibar.
Pamoja na Simba SC kuwania ubingwa wa michuano hiyo, lakini
sasa Christopher ameingia kwenye mbio za kiatu cha dhahabu cha michuano hiyo,
kwa kufikisha mabao manne, akiwa anaongoza akifuatiwa na Kisiga.
Katika michezo mingine ya kuhitimisha hatua ya makundi ya
michuano hiyo jana Uwanja wa Chamazi, Jamhuri FC iliichapa 4-0 Mtende, zote za
Zanzibar mabao ya washindi yakifungwa na Sadik Rajab dakika ya 20, 44, Issa
Achimwene aliyejifunga dakika ya 82 na Suleiman Khatib dakika ya 88.
Kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, Azam FC ilitoka nyuma
kwa bao 1-0 na kuifunga Polisi Moro FC mabao 2-1, mabao yake yakitiwa kimiani
na beki Said Mourad dakika ya 20 na Abdi Kassim ‘Babbi’ dakika ya 70, wakati la
Maafande wa Morogoro lilitiwa kimiani na Mokili Rambo dakika ya kwanza. Polisi
ilimpoteza mchezaji wake, Abdallah Rajab dakika ya 88 aliyetolewa nje kwa kadi
nyekundu.
Katika Kundi A, Simba SC imeongoza kwa pointi zake nne,
baada ya kutoa sare moja na kushinda moja, ikifuatiwa na Zimamoto na Mtende
zinazofungana kwa pointi tatu kila moja, wakati Jamhuri inashika mkia kwa
pointi yake moja.
Kundi B, Mtibwa inaongoza kwa pointi zake tisa ikifuatiwa na
Azam FC na Polisi Moro, zenye pointi tatu kila moja, wakati Falcon inashika
mkia, ikiwa haina pointi hata moja.
Wakati hatua ya makundi inamalizika leo, mechi za Nusu
fainali na fainali zote zitachezwa Dar es Salaam. Mdhamini wa michuano hiyo,
Banc ABC anagharamia usafiri wa ndege kwa timu zote kutoka kituo kimoja hadi
kingine, malazi na jezi.
Kanuni za mashindano haya ni kushirikisha timu zilizoshika
nafasi tatu za juu katika Ligi Kuu za Bara na visiwani na mbili zilioongoza
katika kupanda Ligi Kuu zote mbili, lakini kwa Bara, Yanga waliokuwa washindi
wa tatu msimu uliopita, walijitokea na nafasi yao ikachukuliwa na Mtibwa Sugar
ambayo ilishika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu.
Bingwa wa michuano hiyo mipya itakayokuwa ikifanyika kila
mwaka, ataondoka na Sh. Milioni 40, mshindi wa pili Sh. Milioni 20, wa tatu Sh.
Milioni 15 sawa na wa nne, wakati washiriki wengine wataondoka na Sh. Milioni 5
kila moja.
NUSU FAINALI
Agosti 15, 2012
Mtibwa Sugar Vs Jamhuri (Saa 8:00 mchana)
Simba SC Vs Azam FC (Saa 10:00 jioni)
(Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam)
KUNDI A
P W D L GD P
Simba B 3 2 1 - 3 7
Jamhuri FC 3 1 1 1 2 4
Zimamoto 3 1 - 2 -1 3
Mtende FC 3 1 - 2 -5 3
MATOKEO/RATIBA
Agosti 5, 2012
Simba SC 1-1 Jamhuri FC
Zimamoto FC 2-3 Mtende FC
Agosti 9, 2012
Jamhuri FC 0-2 Zimamoto FC
Mtende FC 0-2 Simba SC
Agosti 12, 2012
Simba SC 2-0 Zimamoto FC
Jamhuri FC 4-0 Mtende FC
KUNDI B
P W D L GD P
Mtibwa 3 3 - - 8 9
Azam FC 3 2 - 1 3 6
Polisi Moro 3 1 - 2 -1 3
S. Falcon 3 - - 3 -9 0
MATOKEO/RATIBA
Agosti 5, 2012
Super Falcon FC 0-2 Azam FC
Agosti 6, 2012
Mtibwa Sugar FC 2-1 Polisi Moro FC
Agosti 9, 2012
Azam FC 0-2 Mtibwa Sugar FC
Polisi Moro FC 2-0 Super Falcon FC
Agosti 12, 2012
Azam FC 2-1 Polisi Moro FC
Super Falcon FC 0-5 Mtibwa Sigar FC


.png)
0 comments:
Post a Comment