![]() |
| KINARA WA MABAO; Christopher Edward |
Na
Prince Akbar, Mwanza
SIMBA SC imetinga Nusu Fainali ya michuano ya BankABC Sup8r kwa
kishindo, baada ya kuifunga Zimamoto ya Zanzibar mabao 2-0 kwenye Uwanja wa CCM
Kirumba mjini Mwanza.
Simba walioingiza kikosi chao cha pili kwenye michuano hiyo,
kinachonolewa na Kocha Suleiman Abdallah Matola, ilipata mabao yote yote
kupitia kwa kiungo chipukizi anayeinukia vema katika soka ya Tanzania,
Christopher Edward kipindi cha pili.
Christopher ambaye hukomazwa pia kwenye kikosi cha timu ya
taifa ya Tanzania, Taifa Stars na kikosi cha kwanza cha Simba, alifunga bao la
kwanza penalti dakika ya 50, baada ya beki Miraj Adam kuangushwa kwenye eneo la
hatari.
Edward ambaye ni kipenzi cha kocha Mserbia wa Simba,
Profesa Milovan Cirkovick, alifunga bao la pili dakika ya 55 baada ya kuwapiga
chenga mabeki watatu wa Zimamoto kabla ya kumchambua kipa wa timu hiyo ya Zanzibar.
Pamoja na Simba SC kuwania ubingwa wa michuano hiyo, lakini
sasa Christopher ameingia kwenye mbio za kiatu cha dhahabu cha michuano hiyo,
kwa kufikisha mabao manne, akiwa anaongoza.
Katika michezo mingine ya kuhitimisha hatua ya makundi ya
michuano hiyo, Uwanja wa Chamazi, Jamhuri FC iliichapa 4-0 Mtende, zote za
Zanzibar mabao ya washindi yakifungwa na Sadik Rajab dakika ya 20, 44, Issa
Achimwene aliyejifunga dakika ya 82 na Suleiman Khatib dakika ya 88.
Kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, Azam FC ilitoka nyuma
kwa bao 1-0 na kuifunga Polisi Moro FC mabao 2-1, mabao yake yakitiwa kimiani
na beki Said Mourad dakika ya 20 na Abdi Kassim ‘Babbi’ dakika ya 70, wakati la
Maafande wa Morogoro lilitiwa kimiani na Mokili Rambo dakika ya kwanza. Polisi ilimpoteza
mchezaji wake, Abdallah Rajab dakika ya 88 aliyetolewa nje kwa kadi nyekundu.
Uwanja wa Amaan, Zanzibar, Kocha Mecky Mexime ataiongoza
Mtibwa Sugar katika mchezo wa mwisho wa makundi dhidi ya wenyeji Super Falcon
FC.
Katika Kundi A, Simba SC inaongoza kwa pointi zake nne,
baada ya kutoa sare moja na kushinda moja, ikifuatiwa na Zimamoto na Mtende
zinazofungana kwa pointi tatu kila moja, wakati Jamhuri inashika mkia kwa pointi
yake moja.
Kundi B, Mtibwa inaongoza kwa pointi zake sita ikifuatiwa na
Azam FC na Polisi Moro, zenye pointi tatu kila moja, wakati Falcon inashika
mkia, ikiwa haina pointi hata moja.
Wakati hatua ya makundi inamalizika leo, mechi za Nusu
fainali na fainali zote zitachezwa Dar es Salaam. Mdhamini wa michuano hiyo,
Banc ABC anagharamia usafiri wa ndege kwa timu zote kutoka kituo kimoja hadi
kingine, malazi na jezi.
Kanuni za mashindano haya ni kushirikisha timu zilizoshika
nafasi tatu za juu katika Ligi Kuu za Bara na visiwani na mbili zilioongoza
katika kupanda Ligi Kuu zote mbili, lakini kwa Bara, Yanga waliokuwa washindi
wa tatu msimu uliopita, walijitokea na nafasi yao ikachukuliwa na Mtibwa Sugar
ambayo ilishika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu.
Bingwa wa michuano hiyo mipya itakayokuwa ikifanyika kila
mwaka, ataondoka na Sh. Milioni 40, mshindi wa pili Sh. Milioni 20, wa tatu Sh.
Milioni 15 sawa na wa nne, wakati washiriki wengine wataondoka na Sh. Milioni 5
kila moja.
NUSU FAINALI
Agosti 15, 2012
Mtibwa Sugar Vs Jamhuri (Saa 8:00 mchana)
Simba SC Vs Azam FC (Saa 10:00 jioni)
(Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam)
KUNDI A
P W D L GD P
Simba B 3 2 1 - 3 7
Jamhuri FC 3 1 1 1 2 4
Zimamoto 3 1 - 2 -1 3
Mtende FC 3 1 - 2 -5 3
MATOKEO/RATIBA
Agosti 5, 2012
Simba SC 1-1 Jamhuri FC
Zimamoto FC 2-3 Mtende FC
Agosti 9, 2012
Jamhuri FC 0-2 Zimamoto FC
Mtende FC 0-2 Simba SC
Agosti 12, 2012
Simba SC 2-0 Zimamoto FC
Jamhuri FC 4-0 Mtende FC
KUNDI B
P W D L GD P
Mtibwa 2 2 - - 3 6
Azam FC 3 2 - 1 3 6
Polisi Moro 3 1 - 2 -1 3
S. Falcon 2 - - 2 -4 0
MATOKEO/RATIBA
Agosti 5, 2012
Super Falcon FC 0-2 Azam FC
Agosti 6, 2012
Mtibwa Sugar FC 2-1 Polisi Moro FC
Agosti 9, 2012
Azam FC 0-2 Mtibwa Sugar FC
Polisi Moro FC 2-0 Super Falcon FC
Agosti 12, 2012
Azam FC 2-1 Polisi Moro FC
Super Falcon FC vs Mtibwa Sigar FC (Saa 2:00 usiku, Z’bar)



.png)
0 comments:
Post a Comment