![]() |
Makamu Mwenyekiti wa Simba Sc, Geoffrey Nyange 'Kaburu' akimkabidhi jezi Ngassa kulia. Kumbe kabla ya kusaini Simba, dogo alisaini Yanga! |
Na Mahmoud Zubeiry
YANGA ya Dar es Salaam imesema kwamba,
iwapo Simba wataendelea kumuwekea pingamizi beki Kevin Yondan, na wao wataibua
mkataba ambao, Mrisho Ngassa alisaini na klabu yao.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga
aliiambia BIN ZUBEIRY jana usiku kwamba, Ngassa alisaini mkataba na
Yanga, lakini walipogundua amesaini na Simba wakaamua kuachana naye na
hawakudai chochote.
Sanga alisema wanashangazwa na hatua ya
Simba kuendelea kumng’ang’ania Yondan ambaye amekwishaonyesha mapenzi na Yanga
na amejiunga nayo, wakati wao waliamua kuachana na Ngassa mara moja
walipogundua amejiunga na Simba.
Ngassa alijiunga na Simba akitokea Azam
FC, ambayo ilimtoa kwa mkopo lakini Wekundu hao wa Msimbazi wakasaini naye
mkataba wa mwaka mmoja zaidi, kutoka ule wa mkopo wa mwaka mmoja waliopewa na
Azam.
Hatua hiyo ya Yanga inafuatia kikao cha
jana baina ya klabu hizo mbele ya Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za
Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake, Alex
Mgongolwa, kushindwa kufikia makubaliano.
Katika kikao hicho kilichoanza majira ya
saa 7:00 mchana, hoja ya kwanza kuwasilishwa mezani ilikuwa ni suala la beki
Twite na upande wa Yanga uliwakilishwa na Sanga na Katibu, Celestine Mwesigwa
wakati kwa Simba walikuwepo Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ), Zacharia Hans Poppe.
Ikumbukwe, Simba iliwasilisha malalamiko
ya kufanyiwa mchezo usio wa kiungwana na Yanga kwa Twite. Ilidai Twite alisaini
mkataba na klabu yao Agosti 1, mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la
Soka Rwanda (FERWAFA) na APR na kulipwa dola za Kimarekani 30,000 na nyingine
2,000 za nauli ya kuja Dar es Salaam kujiunga na klabu hiyo. Hata hivyo,
mchezaji huyo akahamia Yanga.
Katika mjadala huo, Simba ilikubali
kurudishiwa fedha zao, lakini viongozi wa Yanga wakasema hawawezi kutoa hadi
waombwe radhi na Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage, ambaye alisema
viongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake makutano ya mitaa ya Twiga na
Jangwani wana ‘fedha chafu za EPA’.
Simba wakasema kauli yake ya Rage
ilikuwa sehemu ya utani wa jadi, kama ambavyo Yanga walimvalisha jezi Twite
yenye jina la Rage.
Kufikia hapo, Simba wakasema hawawezi
hata kujadili suala la Kevin Yondan na Kamati ya Mgongolwa ikasema itapitia
maelezo ya pande zote, watatoa majibu kwa mujibu wa kanuni na sheria Septemba
10, mwaka huu.
Katika kesi ya Yondan, walalamikaji ni
Simba, ambao wanadai beki huyo alisaini Yanga akiwa bado ana mkataba na klabu
yao.
Sanga alisema mbali na suala la Twite,
katika kikao cha jana waligundua mapungufu kwenye mkataba wa Yondan
uliowasilishwa mezani na Simba na kwa sababu hiyo, nao wanaridhia suala hilo
liamuliwe na Kamati ya Mgongolwa.
Awali, Kamati ya Mgongolwa ilikutana
Jumapili asubuhi hadi usiku, bila kupata suluhisho la pingamizi hizo na kuamua
kutumia busara ya kuzikutanisha pande zinazopingana kujaribu kupata suluhu leo.
Pingamizi nyingine zilikuwa ni, Azam inayopinga
usajili wa Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba
naye unaomalizika Juni 11 mwakani na inaelezwa tayari klabu hizo
zimekwishamalizana juu ya kiungo huyo.
Yanga inapinga Simba kuwaacha wachezaji
Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo kwa maelezo
walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania walizozitumia kwenye
mashindano ya Kombe la Kagame. Pia inapinga Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga
Simba kwa vile ana leseni ya kuchezea Azam kwa msimu wa 2012/2013.
Pingamizi lingine la Yanga kwa Simba ni
kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa kwa maelezo
inao wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano. Imewataja wachezaji hao kuwa ni
Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal Ochieng,
Komalmbil Keita na Daniel Akuffor.
Pingamizi nyingine ambazo jumla zinahusu
wachezaji 17 walioombewa usajili katika timu za Ligi Kuu ni Toto Africans ya
Mwanza imewawekea pingamizi wachezaji Enyinna Darlington aliyeombewa usajili
Kagera Sugar, na Mohamed Soud anayekwenda Coastal Union kwa maelezo kuwa bado
ina mikataba na wachezaji hao.
Pia Flamingo ya Arusha inapinga usajili
wa wachezaji wake Kelvin Friday Iddy katika timu za Azam na Salim Walii (Polisi
Mara) kwa vile taratibu za kuwahamisha bado hazijafanywa. Nayo Kagera Sugar
inapinga usajili wa beki David Charles Luhende kwenda Yanga kwa vile ada ya
uhamisho haijalipwa.
Super Falcon ya Chanjamjawiri,
Chakechake, Pemba inapinga wachezaji wake wanne; Edward Christopher Shija,
Samir Said Luhava (Simba), Robert Joseph Mkhotya (African Lyon) na Sultan Juma
Shija (Coastal Union) kusajiliwa katika timu hizo kwa maelezo taratibu halali
za uhamisho hazikufuatwa.
Mchezaji Othman Hassan aliyeombewa
usajili Coastal Union anapingwa na Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na timu
hiyo unaomalizika Mei 24, 2013. Nayo Rollingstone Multipurpose Ateclass
Foundation ya Arusha inapinga usajili wa Kigi Makassy kutoka Yanga kwenda Simba
hadi itakapolipwa fidia ya kumlea mchezaji huyo kwa vile bado hajafikisha umri
wa miaka 23.
0 comments:
Post a Comment