![]() |
Na Mahmoud Zubeiry |
SIMBA SC itaiwakilisha Tanzania katika Ligi ya Mabingwa
Afrika mwakani na kwa sasa inakabiliwa na jukumu kubwa la kutengeneza timu yake
hadi kufika Januari wawe wamekamilika.
Pilika za kutosha na vurugu ndani yake zinafanyika kwa sasa
Simba katika kile unachoweza kukiita kujenga timu- wachezaji wanasajiliwa kwa
mamilioni baada ya wiki mbili wanafukuzwa, baada ya kucheza mechi moja au
mbili.
Lino Masombo, Patrick Kanu Mbivayanga, Mussa Mudde na Danny
Mrwanda ni baadhi ya wachezaji waliosajiliwa kwa fedha nyingi, lakini wakatemwa
hata kabla ya msimu kuanza.
Usajili wa wachezaji wote hawa wanne unakadiriwa si chini ya
Sh. Milioni 100, lakini fedha hizo ‘zimetupwa jalalani’ na sasa unaweza kuhisi
hali fulani kutokea tena ndani ya Simba SC.
Kelele zimekwishaanza juu ya wachezaji waliosajiliwa baada ya
kutupiwa virago akina Mudde, Mbivayanga na Masombo, ambao ni Komabil Keita,
Paschal Ochieng na Daniel Akuffo kwamba nao ni magalasa.
Angalau Akuffo hazungumziwi sana kwa sababu katika mechi nne
za kirafiki alizoichezea Simba amefunga mabao matatu, lakini mabeki Keita na
Ochieng kwa sababu timu hiyo inaruhusu sana mabao kipindi hiki, wao wameingia
kwenye ‘zengwe’.
Nimesoma gazeti la Mwanaspoti jana, Kocha wa zamani wa Yanga,
Kenny Mwaisabula anahoji Keita na Ochieng wamefuata nini Simba na kwa kuwa huyu
kwa sasa ni Mwandishi wa habari za michezo na mchambuzi na kwa jinsi ambayo
viongozi wa sasa wa Simba wanapenda kufanya kazi kupitia vyombo vya habari,
nina shaka na mustakabali wa wachezaji hao katika klabu hiyo.
Magazeti yanaandika Simba ilifungwa na Sofapaka ya Kenya
mabao 3-0 Alhamisi katika mchezo wa kirafiki kwa sababu ya kupwaya kwa Keita na
Ochieng wanaocheza pamoja katika beki ya kati.
Tayari huo unachukuliwa kama mwendelezo wa makosa ya Simba
katika usajili wa wachezaji wa kigeni, baada ya akina Lino Masombo, Mbiyavanga
na Mudde.
Mara nyingi nawaambia watu, kusajili wachezaji wazuri ni
jambo moja na kuwa na timu nzuri ni jambo lingine- timu nzuri ni ile inayotayarishwa
taratibu baada ya usajili.
Mfano mmoja ni jinsi ile timu B ya Simba iliyochukua Kombe la
BankABC mbele ya vikosi vya Ligi Kuu vya timu za Azam FC na Mtibwa Sugar- kwa
sababu imekaa pamoja muda mrefu na wachezaji wamezoeana.
Sasa leo Simba inasajili wachezaji wawili kutoka timu na nchi
tofauti, inataka ndani ya wiki moja tu wacheze pamoja kwa maelewano, jamani
hicho kitu hakiwezekani.
Miezi miwili iliyopita wakati wa michuano ya Klabu Bingwa
Afrka Mashariki na Kati, Kombe la Kagame watu walianza kumkosoa Felix Sunzu-
bahati kwake hayupo kwa sasa, lakini kama angekuwepo na matokeo haya, zengwe
lingeendelea na upande wake pia.
Sijui hata hao wanaojiita wachambuzi huwa wanachambua nini-
maana tatizo la Simba hivi sasa linaonekana wazi na litahitaji muda kidogo.
Kifo cha Patrick Mutesa Mafisango ndio kinaitesa Simba kwa
sasa- hajapatikana kiungo mbadala wake wa kuiongoza timu. Jamaa alikuwa ana
mchango mkubwa sana kwenye timu enzi za uhai wake na kwa kiasi kikubwa ubingwa
wa Ligi Kuu ulitokana na yeye.
Tulikuwa tunaishuhudia Simba inacheza ovyo, inapoteana kabisa
msimu uliopita ilipocheza bila Mafisango. Wakati Simba ikiwa inajiandaa na
mchezo wa marudiano na ES Setif ya Algeria ilimsimaisha Mafisango kwa utovu wa
nidhamu na ilipocheza mechi ya Ligi Kuu na African Lyon bila kiungo huyo,
iligundua haiwezi kwenda bila mtaalamu huyo (R.I.P.).
Ilicheza ovyo na kushinda ‘kizali zali’ 2-0 na baada ya hapo
ikamrejesha kundini Mafisango akasafiri na timu Algeria. Huyu ndiye alikuwa
mfungaji bora wa timu msimu uliopita kwa mabao yake 10.
Alikuwa anajua kuichezesha timu- sasa hayupo na bahati mbaya
zaidi klabu haijampata kiungo mpya mkabaji, hivyo safu ya ulinzi inakuwa na mzigo
mkubwa.
Katika soka, kitaalamu mabeki wakiwa wanamrudishia mipira
mingi kipa basi kuna tatizo kwenye kiungo pale chini katika kuiunganisha timu na
hilo ndilo linalojitokeza kwa sasa katika Simba.
Simba inacheza vizuri ikiwa na mpira, kwa sababu ina viungo
wengi wachezeshaji, lakini tatizo linakuja mpira unapohamia kwa wapinzani-
wanapita kiulaini na safu ya ulinzi ya klabu hiyo inafikiwa mno, tena kwa
urahisi.
Mipira inapenyezwa mno kwenye eneo la hatari la Simba- sasa
wazi hapa kabla ya kuanza kuwatazama mabeki, Simba waimulike safu yao ya
kiungo.
Pamoja na hilo, kubwa ni kwamba bado timu haijazoeana na hilo
limetokana na ile wachezaji wanasajiliwa, wanafukuzwa- maana yake kila siku
timu inaanza upya na sasa tushukuru pazia la usajili limefungwa hadi Januari,
timu haitabomolewa tena.
Amri Kiemba na Jonas Mkude ndio viungo pekee wakabaji katika
Simba kwa sasa ambao siku za karibuni hawapangwi- mi nitabaki kuwa mwandishi na
mchambuzi, lakini Profesa Milovan Cirkovick ni kocha na mtaalamu, hivyo anajua
anachokifanya.
IIa nachoweza kumshauri tu, babu huyo wa Kiserbia apunguze
kujiamini kwa sababu, maamuzi mengi ya viongozi wa Simba hutokana na presha ya
mashabiki au vyombo vya habari.
Mwandishi mnazi kwa hasira zake, timu yake imefungwa anaweza
kuandika kwa jazba bila kuzingatia vigezo wala utaalamu akaponda timu na
wachezaji na kiongozi asiye mweledi kesho akafukuza mchezaji. Hiyo ndio soka ya bongo.
Sasa kama hawa wanaowaponda Ochieng na Keita mapema yote hii,
ni kwa sababu ya zile bao tatu za Sofapaka- ila kama Wakenya hao wangepoteza
nafasi zote hizo na Simba wakatumia japo nafasi moja kati ya tatu walizopata,
mabeki hao leo wasingekandiwa.
Ufike wakati sasa Simba wakajifunza kuwa na subira.
Wakajifunza kutokana na makosa, kwani msimu uliopita walimfukuza Derrick
Walullya wakiamini ni galasa, ila alikuja na URA kwenye Kombe la Kagame Julai
mwaka huu akacheza soka baab kubwa, udenda ukawatoka.
Jumanne Simba wanacheza na Azam katika Ngao ya Jamii,
wanacheza na timu ambayo kwa kiasi kikubwa ni ile ile iliyokaa pamoja muda
mrefu na kuzoeana, itakuwa mechi ngumu kwao.
Wanacheza dhidi ya mshambuliaji ambaye anajiamini anapokutana
nao, John Bocco ‘Adebayor’- ambaye mara ya mwisho Simba ilipokutana na Azam
alifunga mabao yote, katika ushindi wa 3-0, itakuwa mechi ngumu kwao na hasa
kulingana na hali halisi ya Simba hivi sasa.
Kabla ya mechi hiyo, nawaambia kabisa Simba wanapaswa kutulia
na kuangalia mbele katika kutengeneza timu yao kuelekea Ligi ya Mabingwa mwakani,
kwa matokeo yoyote yale Jumanne wazingatie hilo.
0 comments:
Post a Comment