• HABARI MPYA

    Sunday, September 09, 2012

    MAFUNZO YAANZA VEMA LIGI ZANZIBAR, FALCON YAENDELEA KUANGUSHA MOJA MOJA

    Mafunzo SC

    Na Ally Mohamed, Zanzibar
    PAZIA la Ligi Kuu Zanzibar, limefunguliwa jana kwa mechi mbili kuchezwa katika viwanja viwili tofauti, kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja, Mabaharia wa KMKM walikutana na Mafunzo, ambapo mechi hiyo imemalizika kwa Mafunzo kuchomoza na ushindi wa bao 1-0, bao hilo pekee likipatikana katika dakika ya tano, mfungaji Mohammed Abdulrahman.
    Huko kisiwani Pemba nako ilipigwa mechi moja ikiwakutanisha mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Super Falcon na Chipukizi ambapo kwa mara nyengine tena Super Falcon ambao ni wawakilishi wa Zanzibar katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani, wamefungwa 2-0.
    Hii ni mechi ya sita mfululizo Super Falcon wanapokea kipigo, wakianzia katika michuano ya BancABC Super 8, ambapo walipoteza mechi zao zote 3 za hatua ya makundi, kabla ya kukubali kipigo cha 3-1 kutoka kwa Jamhuri katika mechi ya Ngao ya Jamii iliyochezwa Septemba 1, mwaka huu Uwanja wa Amaan na juzi wakicheza na Coastal Union ya jijini Tanga katika mechi ya kirafiki, mchezo uliochezwa Uwanja wa Ngome, Fuoni, Wilaya ya Magharibi, Unguja walifungwa 2-0.
    Ligi hiyo inatarajia kuendelea tena leo kwa mechi mbili, katika Uwanja wa Amaan kisiwani unguja, Klabu ya Malindi ambao wamenunua daraja kutoka kwa Miembeni SC watacheza na timu iliyopanda daraja msimu huu, Bandari na katika Uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba washindi wa pili wa ligi iliyopita, Jamhuri wakicheza na Duma, mechi zota zinatarajiwa kuanza saa 10:30 jioni.
    Ligi kuu ya Zanzibar, ambayo msimu huu inafahamika kwa jina la Zanzibar Grand Malt Premier League kutokana na mdhamini kinywaji cha Grand Malt, inashirikisha timu 12, huku timu 8 zikitoka kisiwani Unguja na timu 4 zikitoka kisiwani Pemba, timu zinazotoka kisiwani Unguja ni  Bandari, Chuoni, KMKM, Mafunzo, Malindi, Mundu ambao wamenunua daraja kutoka kwa Miembeni United, Mtende iliyopanda daraja msimu huu na Zimamoto.
    Kwa upande wa kisiwani Pemba ni Chipukizi, Duma, Jamhuri na Mabinwa watetezi, Super Falcon.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAFUNZO YAANZA VEMA LIGI ZANZIBAR, FALCON YAENDELEA KUANGUSHA MOJA MOJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top