![]() |
Kutoka kulia Jerry Tegete, Athumani Iddi 'Chuji' na Haruna Niyonzima. Kwa nyuma ni Said Bahanuzi kushoto na Hamisi Kiiza kulia. |
Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA wa Yanga, Tom Saintfiet raia wa Ubelgiji amesema kwamba anataka mechi moja zaidi ya kujipima nguvu, kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Septemba 15, mwaka huu.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Mtakatifu Tom alisema kwamba amekwishawasilisha ombi lake hilo kwa uongozi wa klabu na sasa anasubiri jibu.
Aidha, Mtakatifu Tom alisema kwamba wachezaji wake wawili, kipa Said Mohamed na kiungo Idrisa Assenga jana hawakufanya mazoezi kwa sababu ya majeruhi, wakati Hamisi Kiiza bado yuko na timu yake ya taifa ya Uganda, The Cranes.
Viungo wake wengine waliokuwa wagonjwa, Athumani Iddi ‘Chuji’, Rashid Gumbo, Nizar Khalfan na Juma Seif ‘Kijiko’ walianza mazoezi jana.
Viungo hao walikosekana uwanjani Jumamosi, wakati Yanga inashinda 2-1, kwa mabao mawili ya dakika za lala salama, dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Saidi Bahanuzi ‘Spider Man’, kwa mara nyingine siku hiyo alikuwa shujaa wa Yanga baada ya kufunga bao la ushindi dakika ya 85 katika mchezo, ambao Coastal Union ilimpoteza kiungo wake Jerry Santo aliyepewa kadi nyekundu kwa kumtolea maneno machafu refa Hashim Abdallah dakika ya 59.
Hilo lilikua bao lake la nane Bahanuzi tangu aanze kuichezea Yanga miezi miwili iliyopita, akitokea Mtibwa Sugar. Awali ya hapo, beki Mganda, Philip Kaira alijifunga katika harakati za kuokoa krosi ya Shamte Ally dakika ya 84, bao la Coastal lilitiwa kimiani na kiungo Razack Khalfan.
Kocha Saintfiet anajivunia rekodi ya kushinda mechi 10 kati ya 11 alizoiongoza timu hiyo tangu ajiunge nayo miezi miwili iliyopita.
REKODI YA SAINTFIET YANGA
1. Yanga Vs JKT Ruvu 2-0
2. Yanga Vs Atletico (Burundi) 0-2
3. Yanga Vs Waw Salam (Sudan Kusini) 7-1
4. Yanga Vs APR (Rwanda) 2-0
5. Yanga Vs Mafunzo (Z’bar) 1-1 (5-3penalti)
6. Yanga Vs APR (Rwanda) 1-0
7. Yanga Vs Azam 2-0
8. Yanga Vs African Lyon 4-0
9. Yanga Vs Rayon (Rwanda) 2-0
10. Yanga Vs Polisi (Rwanda) 2-1
11. Yanga Vs Coastal Union 2-1
0 comments:
Post a Comment