![]() |
Mwaipopo |
Na Princess Asia
VIUNGO wawili tegemeo wa Azam FC na ambao hivi sasa wako juu ile mbaya kimchezo, Ibrahim Mwaipopo na Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr.’ sasa wanaendelea vizuri na kuna matumaini wakawa fiti kwa mechi ya Ngao ya Jamii, Septemba 11 dhidi ya Simba, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Viungo hao wamekwishaanza mazoezi mepesi, wakiongozwa na daktari wa timu hiyo, Dk Mwanandi Mwankemwa kuanzia gym hadi uwanjani. Dk. Mwanandi anasema wachezaji hao hali zao zinatia matumaini kwa sasa na wataendelea kuwaangalia hadi mwishoni mwa wiki ili kujua maendeleo yao.
Viungo hao tegemeo hakuwemo kwenye mechi ya kirafiki Jumapili dhidi ya Coastal Union ya Tanga, kwenye Uwanja wa Chamazi, kujiandaa na mechi hiyo dhidi ya Simba.
Katika mechi hiyo iliyokuwa tamu, mabao mawili ya John Raphael Bocco ‘Adebayor’ katika dakika za 15 na 44, yaliipa Azam FC ushindi wa mabao 2-0 Uwanja wa Chamazi.
Bocco alikuwa mwiba mchungu kweli siku hiyo kwa safu ya ulinzi ya Coastal, kwani pamoja kufunga mawili, lakini alikosa mabao matatu ya wazi mno katika mechi ambayo, kiungo Abdulhalim Humud alitolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 32 kwa rafu na lugha chafu.
Hiyo ni mechi ya tano Coastal inafungwa kati ya sita za kujipima nguvu ilizocheza kabla ya Jumamosi kufungwa 2-1 na Yanga, awali ilifungwa 3-2 na Bandari mjini Mombassa, baadaye 2-0 Tanga, ilifungwa 2-1 na Polisi mjini Morogoro na yenyewe iliifunga JKT Oljoro 1-0.
Kwa Azam hiyo ni mechi ya tatu mfululizo ya kujipima nguvu wanashinda, awali walizifunga 1-0 Prisons ya Mbeya na Transit Camp 8-0.
Azam inatarajiwa kuivaa Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Septemba 11, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ikiwa ni mchezo wake wa kwanza katika historia ya Ngao hiyo.
Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0.
Ikumbukwe mara ya mwisho Simba SC ilipokutana na Azam FC, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwezi uliopita Dar es Salaam, ilifungwa mabao 3-1, yote yakifungwa na Bocco na lile la kufutia machozi kwa wekundu hao Msimbazi liliwekwa kimiani na beki mahiri Shomari Kapombe, aliyemajeruhi kwa sasa.
0 comments:
Post a Comment