• HABARI MPYA

    Tuesday, September 04, 2012

    MNYAMA ANARUDI DAR TOWN LEO

    Wachezaji wa Simba SC

    Na Mahmoud Zubeiry
    BAADA ya mwezi na ushei wa kuwa kambini nje ya Dar es Salaam, mabingwa wa Tanzania Bara, Simba SC wanarejea leo Dar es Salaam tayari kwa mechi yao ya Alhamisi dhidi ya waliowahi kuwa mabingwa wa Kenya, Sofapaka FC, Uwanja wa Taifa.
    Mara ya mwisho Simba ilicheza Dar es Salaam Agosti 8, na kufungwa mabao 3-1 na City Stars ya Nairobi, Kenya Uwanja wa Taifa.  
    Msemaji wa klabu ya Simba, Ezekiel Kamwaga ‘Mr. Liverpool’ aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, mechi hiyo itakuwa ya mwisho kabla ya kucheza na Azam FC, Septemba 11, mwaka huu katika mechi ya Ngao ya Jamii.
    Kwa sasa kiwango cha Simba, inayofundishwa na Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick, akisaidiwa na Mganda, Richard Hamatre, kipo vizuri na timu inaonekana iko tayari kwa Ligi Kuu. Pamoja na Jumapili kulazimishwa sare ya 1-1 na Sony Sugar ya Kenya, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, lakini Simba ilicheza soka safi na washambuliaji wake walikosa mabao ya wazi zaidi ya matano.
    Lakini hata hali mbaya ya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid katika eneo la kuchezea inachangia kupunguza idadi ya mabao kwa Simba. Katika mechi tatu ambazo Simba imecheza kwenye Uwanja huo, imevuna mabao matano na kufungwa matatu, na kikwazo kimekuwa kikionekana ni hali ya eneo la kuchezea.
    Katika mchezo wa Jumapili, bao la Simba lilifungwa na Daniel Akuffo, wakati Komabil Keita alijifunga katika jitihada za kuokoa na kuwapa Wakenya bao la kuongoza. Awali, Simba ilicheza mechi mbili Arusha, dhidi ya Mathare United ya Kenya na JKT Oljoro ya Arusha, ambazo zote ilishinda 2-1, mshambuliaji mpya Daniel Akuffo kutoka Ghana akifunga bao moja kila mechi, Kiggi Makaasy na Mrisho Ngassa wakifunga mabao mengine.   
    Kitu moja tu ambacho Milovan anapaswa kuendelea kufanyia kazi ni makosa ya safu ya ulinzi na mawasiliano duni na makipa wao.
    Ilivyo sasa kipa yeyote anayesimama kwenye lango la Simba SC, kabla ya kuchunga wachezaji wa timu pinzani, anakuwa na jukumu la kwanza la kujihadhari na mabeki wake wasimfunge, kwani mabeki wote wa kati wa timu hiyo wamekwishaonyesha ‘kipaji  cha kujifunga’ katika mechi za karibuni, Juma Nyosso, Paschal Ochieng na Komabil Keita.
    Simba inajiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii Septemba 11, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambayo kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kukutanisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
    Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
    Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0. 

    MABINGWA WA MECHI ZA NGAO YA JAMII:
    Mwaka              Mshindi      Matokeo   
    2001                  Yanga         2-1 Simba
    2010                  Yanga         0-0 Simba (3-1penalti)
    2011                  Simba         2-0 Yanga
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MNYAMA ANARUDI DAR TOWN LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top