• HABARI MPYA

    Sunday, September 09, 2012

    OKWI ATUA DAR KUIVAA AZAM KESHOKUTWA

    Okwi

    Na Mahmoud Zubeiry
    YUKO tayari Dar es Salaam na keshokutwa atacheza- huyo si mwingine bali ni mshambuliaji hatari wa Simba SC, Emanuel Arnold Okwi ametua leo Jijini kutoka Zambia, ambako aliichezea timu yake ya taifa, Uganda, The Cranes mechi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani Afrika Kusini jana na kufungwa 1-0 kwa mbinde.  
    Okwi ametua Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere saa 1:00 usiku huu na moja kwa moja kuingia kambini, hoteli ya Sapphire, Kariakoo ambako klabu yake, Simba SC imejituliza ikijiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC keshokutwa, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Okwi hajaichezea Simba mechi yoyote tangu msimu huu uanze, kutokana na pilika zake za kujaribu kuhamia Ulaya, ambazo hazikufanikiwa.
    Okwi alikaribia kujiunga na FC Red Bull Salzburg ya Wals-Siezenheim, Austria baada ya kufuzu majaribio ya wiki tatu, lakini klabu huyo ikaghairi dakika za mwishoni akarejea nchini.
    Kukwama kwa Okwi kuliikosesha Simba Euro 600,000 ambazo klabu hiyo, ilikuwa tayari kutoa kumnunua.
    Awali, Simba ilipata ofa ya kumuuza Okwi kwa Sh. Bilioni 2 kwa klabu ya Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini, lakini mshambuliaji huyo akasema anataka kwenda Ulaya.
    Awali Olando Pirates ya Afrika Kusini ilimuomba Okwi akafanye majaribio huko kama angefuzu wangemsajili dau la dola 550,000 kabla ya kuibuka kwa taarifa za kutakiwa Italia na klabu ya Parma.
    Sasa Simba inamsubiri mshambuliaji wake mmoja tu, Mzambia Felix Sunzu ambaye kwa wiki nzima yuko kwao kwenye msiba wa dada yake, ambaye naye anatarajiwa kutua nchini wakati wowote.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: OKWI ATUA DAR KUIVAA AZAM KESHOKUTWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top