
KWA
mashabiki wa soka duniani kote, amezoeleka zaidi kwa jina la Patrick Mboma, ingawa
jina lake halisi ni Henri Patrick Mboma Dem.
Ni
kati ya wachezaji ambao Afrika ina kila sababu ya kujivunia vipaji vyake na
ingawa kwa sasa ametundika daluga, bado mambo yake ni mazuri, wakati huo
akicheza soka ya ushindani yameendelea kuvuta hisia za wengi.
Kwa
sasa Mboma ni balozi maalumu wa Japan ,
nchi ambayo inatarajia kumtumia mchezaji huyo kutoka nchini Cameroon katika
kuhakikisha inafanikisha juhudi za kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia 1922.
Wakati
akicheza soka ya ushindani, Mboma mbali na kutamba akiwa na timu ya Taifa ya Cameroon ,
lakini pia amezichezea klabu kadhaa barani Ulaya, zikiwamo klabu tatu maarufu
za Japan katika Ligi Kuu ya nchini humo, maarufu J.League.
Mboma,
aliyezaliwa Novemba 15, 1970 katika mji wa Douala
nchini Cameroon , kipaji
chake cha soka kilianza kuonekana mbele ya wengi mwaka 1993 na kama ilivyo ada kwa wanasoka wa Afrika, baada ya kufanya
vizuri nyumbani alianza harakati za kusaka ulaji barani Ulaya.
Harakati
hizo zilimwezesha kutua nchini Ufaransa, ambako akiwa huko aliweza kutamba na
timu ya Chateauroux ,
ambayo ilitosha kumfanya adhihirishe uwezo wake wa kuzifumania nyavu, kwani
katika mechi 48 alizocheza alifunga mabao 22.
Baada
ya hapo, Mboma alijiunga na Paris Saint-Germain mwaka 1994, lakini alishindwa
kuonyesha makali aliyoyadhihirisha wakati akiichezea Châteauroux, hali
iliyomfanya adumu na timu hiyo kwa msimu mmoja tu.
Mambo
yalipokwenda kombo, alijiunga na FC Metz ,
ambako alionekana kuzitumia vyema mechi chache alizocheza kwa kudhihirisha
umakini na umahiri wake wa kuzifumania nyavu, hali iliyowashawishi viongozi wa Paris
Saint-Germain kuamua kumchukua kwa mara ya pili mwaka 1996.
Katika
kilichoonekana kama kuwa na mikosi na timu
hiyo, mambo yalionekana kwenda kombo kwa Mboma, kwani alishindwa kabisa
kuonyesha umakini wa kuzifumania nyavu na katika mechi nane alizocheza,
alifunga bao moja tu.
Huo
ukawa mwisho wa Mboma na klabu za Ufaransa, kwani baada ya hapo, alitimkia bara
la Asia na kutua katika klabu ya Gamba Osaka
mwaka 1997, ambako walau alianza kuibua upya makali yake ya kuzifumania nyavu.
Aliifungia
timu hiyo mabao 29 katika mechi 34, rekodi ambayo ilionekana kutoa picha nzuri
kwa mshambuliaji huyo, lakini zaidi ya hilo
kiwango chake cha soka pia kilikuwa kivutio kwa wengi.
Haikushangaza
alipotimkia nchini Italia mwaka 1998 na kujiunga na klabu ya Cagliari ,
kabla ya kuihama timu hiyo mwaka 2000 na kujiunga na klabu nyingine nchini humo
ya Parma ,
ambayo aliichezea kwa msimu mmoja.
Aliihama
Parma mwaka 2001, baada ya kuifungia mabao matano katika mechi 24 na wakati
ikiaminika kuwa makali yake yameanza kupungua katika soka ya kulipwa, Mboma
alitimkia England na
kujiunga na klabu ya Sunderland mwaka 2002.
Hatua
hiyo ambayo ilipokelewa kwa mtazamo tofauti mbele ya mashabiki na wachambuzi wa
soka, baadhi wakiamini amefika mwisho na wengine wakiamini anatafuta makali,
mwishowe kila kitu kilidhihirika, baada ya kufunga bao moja tu katika mechi
tisa.
Katika
kilichotoa dalili kwamba Mboma alikuwa akielekea ukingoni, mwaka 2002 baada ya
kuchemsha Sunderland alitimkia Afrika Kaskazini na kutua nchini Libya , ambako
alijiunga na klabu ya Al-Ittihad ya huko.
Akiwa
na klabu hiyo bado hakuna lolote la maana alilolifanya katika kipindi cha mwaka
2002 na 2003, kwani hata kupata nafasi katika timu ilikuwa vigumu na hivyo
aliishia kucheza mechi mbili tu na hakufunga hata bao moja.
Wakati
ikiaminika mbele ya wengi kwamba angeachana na soka ya kulipwa, bado Mboma
hakuwa mchezaji wa kukata tamaa na badala yake, alirudi nchini Japan na
kujiunga na klabu ya Tokyo Verdy, katika kilichoaminika kuwa ni kufufua upya
kipaji chake.
Akiwa
na klabu hiyo, katika kipindi cha mwaka 2003 na 2004, kidogo Mboma alianza
kuonyesha uhai kwa kuifungia mabao 17 katika mechi 35 na kuhamia klabu nyingine
ya huko huko Japan ya Vissel Kobe, ambayo aliishia kuichezea mechi 10 na
kufunga mabao mawili tu.
Vissel
Kobe ilikuwa klabu ya mwisho kwa Mboma, kwani Mei, 2005, alitangaza rasmi
kustaafu soka ya kulipwa.
Ukiachana
na soka ya klabu, Mboma ni mmoja wa wachezaji waliotoa mchango mkubwa katika
timu ya Taifa ya Cameroon ,
ambayo aliichezea kwa mara ya kwanza mwaka 1995 na hadi anastaafu kuichezea
timu hiyo amecheza jumla ya mechi 57 na kufunga mabao 33.
Ameiwakilisha
Cameroon katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1998 nchini Ufaransa na 2002
huko Japan na Korea Kusini na zaidi ya hayo, mwaka 2000 aliiwezesha Cameroon
kutwaa medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki.
Katika
fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, Mboma ameiongoza vyema Cameroon kutwaa taji la michuano
hiyo katika fainali za mwaka 2000 na 2002.
Mboma
ambaye pia anasifika kwa kufunga mabao kwa mashuti ya mbali, mwaka 2000 alitwaa
tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika na mwaka 2002 akawa mfungaji bora wa michuano
ya Mataifa ya Afrika.
Wakati
hii leo akiwa ni mwanasoka mstaafu, mashabiki wanaendelea kumkumbuka Mboma kwa
mambo mengi enzi zake akiwa katika soka ya ushindani na mojawapo ni staili yake
ya kushangilia kama vile ameshika bastola
mbili kwa mikono yake.
WASIFU
WAKE:
JINA:
Henri Patrick Mboma Dem
KUZALIWA:
Novemba 15, 1970 (Miaka 40)
ALIPOZALIWA:
Douala , Cameroon
KLABU
ALIZOCHEZEA:
Mwaka Klabu
1990–1992
Paris Saint-Germain (aliishia benchi)
1992–1994
LB Châteauroux (Mechi 48, mabao 22)
1994–1995
Paris Saint-Germain (Mechi 8, bao 1)
1995–1996
FC Metz (Mechi 17, mabao 4)
1996–1997
Paris Saint-Germain (Mechi 8, bao 1)
1997–1998
Gamba Osaka (Mechi 34, mabao 29)
1998–2000
Cagliari (Mechi 40, mabao 15)
2000–2001
Parma (Mechi 24, mabao 5)
2002
Sunderland
(Mechi 9, bao 1)
2002–2003
Al-Ittihad (Mechi 2, hakufunga)
2003–2004
Tokyo Verdy 1969 (Mechi 35, mabao 17)
2004–2005
Vissel Kobe (Mechi 10, mabao 2)
(Tangu 1995
hadi 2004, aliichezea Cameroon mechi 56, ameifungia mabao 33)
0 comments:
Post a Comment