• HABARI MPYA

    Wednesday, January 09, 2013

    SASA TUWAACHE HAWA WAZUNGU WAFANYE KAZI

    Na Bin Zubeiry

    USHINDANI katika ya soka ya Tanzania upo katika timu tatu kwa sasa, Azam FC, Simba SC na Yanga, zote za Dar es Salaam.
    Hiyo inatokana na uwekezwaji ndani ya timu hizo kuwa tofauti sana na klabu nyingine zote nchini na pia kuonyesha dhamira ya dhati ya kutaka kutawala soka ya Tanzania.
    Kutoka klabu hizi tatu, hata kocha wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars Mdenmark Kim Poulsen anategemea kwa kiasi kikubwa kupata wachezaji wa kuunda kikosi chake.
    Mfano kwa sasa tu, wachezaji 17 wanaounda kikosi cha Stars ambacho leo kinakwenda Ethiopia kumenyana na wenyeji katika mchezo wa kujipima nguvu, wanatoka timu hizo.
    Hao ni kwa upande wa Azam wapo sita; makipa Aishi Manula na Mwadini Ally, mabeki Aggrey Morris, Erasto Nyoni, viungo Khamis Mcha na mshambuliaji John Bocco.
    Kwa upande wa Simba SC wapo sita pia; ni kipa Juma Kaseja ambaye pia ndiye Nahodha wa Stars, mabeki Amir Maftah na Shomari Kapombe, viungo Amri Kiemba na Mwinyi Kazimoto na mshambuliaji Mrisho Ngasa.
    Kwa upande wa Yanga wapo watano pia; ni mabeki Kevin Yondan na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, viungo Athuman Idd ‘Chuji’ na Frank Domayo na mshambuliaji Simon Msuva.
    Hapa inajiainisha yenyewe ni jinsi gani klabu hizo tatu ni mhimili mkuu wa Taifa Stars na idadi hiyo inaweza kuongezeka endapo klabu hizo zitapata mashindano zaidi ya kuwapa changamoto wachezaji wake na kupandisha viwango vyao.  
    Kwa sasa klabu zote zipo chini ya makocha wa kigeni, ambao wana rekodi nzuri huko walipotokea na uzoefu wa kutosha- maana yake ni makocha wazuri. Si wanafunzi, wote ni watu wazima na wenye uzoefu wa kutosha.  
    Yanga wanaye Mholanzi Ernie Brandts, aliyezaliwa Februari 3, mwaka 1956 mjini Nieuw-Dijk, Gelderland, ambaye mbali na kuichezea PSV Eindhoven ya Ligi Kuu ya Uholanzi, pia alichezea Roda JC Kerkrade, MVV Maastricht na De Graafschap.
    Brandts aliichezea mechi 28 timu ya taifa ya Uholanzi na kuifungia mabao matano na pia alicheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978.
    Katika fainali hizo, Raundi ya pili kwenye mechi na Italia, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyezifungia mabao timu zote katika mechi moja kwenye fainali za Kombe la Dunia.
    Alianza kujifunga dakika ya 18, kisha akaisawazishia Uholanzi dakika ya 50 katika mechi ambayo, mchezaji mwenzake Arie Haan baadaye aliifungia timu yake bao la ushindi na kutoka kifua mbele kwa mabao 2–1.
    Alipostaafu soka akawa kocha na katikati ya msimu wa 2007–2008, Brandts aliambiwa hataongezewa mkataba NAC-Breda, licha ya matokeo mazuri ya kushika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Uholanzi (Eredivisie), ingawa uamuzi huo haukuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo na nafasi yake akapewa Robert Maaskant kuanzia msimu wa 2008–2009.
    Akateuliwa kuwa Kocha wa Rah Ahan mwaka 2009, kabla ya kufukuzwa Desemba 2009 na kuibukia APR ya Rwanda mwaka 2010, kabla ya kutua Yanga mwaka huu.
    Simba wanaye Mfaransa Patrick Liewig, ni kocha wa zamani wa Akademi ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa, ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Club Africain ya Tunisia, Patrick Liewig ndiye atakayerithi mikoba ya Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick katika klabu ya Simba.
    Liewig ana Stashahada ya Juu ya ukocha na Shahada ya tatu ya ualimu wa soka ya vijana aliyotunukiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Ufaransa, Gerard Houiller na amehudhuria pia kozi za ufundishaji mazoezi ya viungo Juni mwaka 1999 katika Chuo Kikuu cha Dijon.
    Kwa upande wa uzoefu, Liewig alifanya kazi PSG kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 kama Kocha Mkuu wa akademi na kuna wakati alikuwa akishirikishwa pia katika programu za timu A, ingawa majukumu yake zaidi yalikuwa ni kwa Under 20, Under 18 aliowawezesha kutwaa Kombe la French Junior Gambardella na Under 16.
    Kuanzia mwaka 1989 hadi 1990:  alikuwa Meneja Mkuu wa Tomislav IVIC, 1990 hadi 1991 alikuwa Msaidizi wa Henri Michel, 1991 hadi 1994 alikuwa Msaidizi wa Artur Jorge, 1994 hadi 1996 alikuwa Msaidizi wa Luis Fernandez, 1996 hadi 1998: alikuwa Msaidizi wa Ricardo Gomez, 1998 hadi 1999 alikuwa Msaidizi wa Alain Giresse.
    Liewig pia alifundisha Al Wahda FC ya Abu Dhabi kuanzia 1999 hadi 2001, ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na Kombe la Ligi.
    Januari mwaka 2003 alikuwa Msimamizi wa Chama cha Soka UAE katika fainali za Afrika za U20 nchini Burkina Faso.
    Kuanzia mwaka 2004 hadi 2009 alikuwa Kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast aliyoipa mataji matatu ya Ligi Kuu ya nchini humo mfululizo, 2004, 2005 na 2006, Super Cup ya nchini humo 2005, 2007, 2008 na 2009 na akaiwezesha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, mara moja akiifikisha Nusu Fainali.
    Amekuwa Kocha bora wa Ivory Coast miaka mitatu mfululizo, 2004, 2005 na 2006 na tangu Septemba mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alikuwa kocha wa Club Africain ya Tunisia
    Azam wanaye Mfaransa, Stewart John Hall, ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa akademi ya Birmingham City F.C. ya England na amewahi kuzifundisha Saint Vincent na Grenadines na Pune FC ya India.
    Vema zaidi ni kwamba, hata mabenchi ya ufundi ya klabu hizi zote tatu sasa yameshiba kidogo, ukianzia pale Yanga Brandts ana wasaidizi wawili, mzalendo Freddy Felix Minziro na Mkenya Razack Ssiwa, ambao wote kwa wakato tofauti wamewahi kuwa makocha wakuu wa klabu hiyo.
    Simba pale, Mfaransa Liewig ana wasaidizi wawili pia, mzalendo Jamhuri Kihwelo na Mganda Moses Basena, ambao wote pia wakati tofauti wamewahi kuwa makocha wakuu wa klabu hizo.
    Azam nako, Hall ana wasaidizi watatu, Muingereza aliyezaliwa na kukulia Tanzania, Kali Ongala, Mkenya Ibrahim Shikanda na mzalendo Iddi Abubakar. Dhahiri hizi ni timu ambazo kama makocha wake watapewa fursa nzuri, basi watafanya kazi nzuri.
    Lakini kumekuwa na tatizo moja kubwa kwa klabu zetu, kutokuwa na subira au wakati mwingine viongozi kutaka kuwatoa kafara makocha kwa sababu zao binafsi.
    Sitaki nikumbushe nani alifanywa nini, lakini nakumbuka miaka ya karibuni katika klabu zote hizo tatu yametokea mazingira ya makocha kutolewa kafara. Kwa kweli haipendezi na huku ni kuleta mzaha katika mambo makini. Niwe wazi, nachukia sana watu wanaoleta mzaha katika mambo muhimu, kwa sababu watu hao ni kikwazo cha maendeleo katika sekta yoyote.
    Nachotaka kusema leo, viongozi wa Simba na Yanga na wamiliki wa Azam wabadilike kidogo, wajiwekee utaratibu wa kuwavumilia makocha na kuwapa muda, kuwawekea mazingira mazuri ya kufanya kazi, kutowaingilia katika shughuli zao, mfano kuwasajilia wachezaji na kuwapangia timu.
    Tuache sasa kila mtu afanye shughuli zake, mfua jezi afue jezi, mtu wa kutunza tovuti atunze tovuti, mgawa posho za wachezaji agawe posho, mmiliki amiliki timu au kiongozi awe kiongozi na makocha wawe makocha.
    Hawa makocha ambao wapo Simba, Azam na Yanga kwa sasa wote ni wazuri, tuvumilie falsafa na matakwa yao, wapewe fursa nzuri ya kufanyia kazi ili angalau baada ya miaka miwili kutoka sasa tuone watazifikisha wapi klabu hizi. Naendelea kuwatakia heri ya mwaka mpya wasomaji wangu, mwaka bado mbichi huu! 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SASA TUWAACHE HAWA WAZUNGU WAFANYE KAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top