• HABARI MPYA

    Sunday, February 10, 2013

    MESSI AFUNGA BAO LA 35 MSIMU HUU BARCA IKIUA 6-1

    Lionel Messi akichana msitu wa mabeki wa Getafe mchana wa leo.

    LIONEL Messi alifunga goli lake la 35 la ligi msimu huu wakati timu iliyopumzisha wakali ya Barcelona ilipotoa kipigo cha 6-1 nyumbani dhidi ya Getafe na kuwafanya wapae kwa tofauti ya pointi 12 kileleni mwa msimamo wa La Liga jana. Alexis Sanchez na David Villa walitumia vyema nafasi adimu ya kuanza katika kikosi cha kwanza kwa kufunga magoli huku Messi, Andres Iniesta, Cristian Tello na Gerard Pique nao kila moja akifunga wakati Barca ilipopata ushindi wa 20 katika mechi 23 za ligi msimu huu na kufikisha pointi 62. 
    Atletico Madrid walikuwa na pointi 50 katika nafasi ya pili kabla ya mechi yao ya jana saa 5:00 usiku dhidi ya Rayo Vallecano, pointi nne juu ya Real Madrid walio katika nafasi ya tatu, ambao waliwasambaratisha Sevilla 4-1 kwenye Uwanja wa Bernabeu Jumamosi. 
    Kocha wa muda wa Barca, Jordi Roura, ambaye anamshikia Tito Vilanova ambaye anauguza upasuaji wa koo, aliwapumzisha wachezaji kadhaa wa kikosi cha kwanza katika mechi hiyo dhidi ya Getafe kwenye Uwanja wa Nou Camp, wakiwamo wachezaji watatu wa timu ya taifa ya Hispania, Pedro, Cesc Fabregas na Sergio Busquets. 
    Alexis alifunga katika dakika ya sita, Messi akafanya matokeo yawe 2-0 dakika saba baadaye na Villa alifunga la tatu kabla ya dakika ya 60 na kuifanya mechi iwe ngumu kwa Getafe, ambao wanashika nafasi ya 12 wakiwa na pointi 29. 
    Messi alikimbia mbele na kumtengea pasi mtokea benchi Tello aliyefunga na nne dakika 11 kabla ya mechi kumalizika  kabla ya makosa ya beki wa kushoto Jordi Alba kumpa Alvaro Vazquez goli la kufutia machozi kwa wageni katika dakika ya 83. 
    Iniesta aliuwahi mpira uliozagaa na kufumua shuti la jirani na lango katika dakika ya 90 na kufunga la tano kabla ya Pique kukamilisha kipigo kizito katika dakika ya pili ya majeruhi akifunga katika goli tupu kufuatia pasi isiyo ya kichoyo ya Thiago Alcantara.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MESSI AFUNGA BAO LA 35 MSIMU HUU BARCA IKIUA 6-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top