• HABARI MPYA

    Monday, February 11, 2013

    SIMBA AMANI TUPU ARUSHA, NGASSA AZAWADIWA FEDHA, TALIB ATUA KAMBINI

    Simba SC

    Na Prince Akbar
    KLABU ya Simba imeendelea na mazoezi yake mjini Arusha na hali ya kikosi ni nzuri, morali ya wachezaji iko juu na hakuna mgogoro au matatizo yoyote.
    Taarifa ya Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga imesema majeruhi mpya ni beki Paul Ngalema ambaye aliumia goti katika mechi ya juzi dhidi ya Oljoro JKT. 
    Mchezaji huyo tayari amesafirishwa kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya kufanyiwa vipimo na uchunguzi zaidi.
    Kutokana na tatizo hilo, Ngalema hataweza kucheza katika ijayo dhidi ya Libolo ya Angola katika Ligi ya Mabingwa Afrika wikiendi ijayo.
    Kamwaga amesema uongozi wa Simba unapenda kuwaarifu wapenzi na washabiki wake kwamba hali ya timu ni shwari kabisa. Hakuna mchezaji yeyote aliyefungiwa wala kusimamishwa na hakuna mitafuruku baina ya wachezaji na makocha au wachezaji na viongozi wa klabu.
    "Simba SC pia inakanusha taarifa zozote za wachezaji wake au makocha wake kupigwa (au kutaka kupigwa) mara baada ya mechi ya Arusha. Kwa waliokuwapo katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta siku ya Jumamosi mara baada ya mechi dhidi ya Oljoro, watakuwa mashahidi kwamba baadhi ya wachezaji wa Simba walibebwa na washabiki na Mrisho Ngassa alipewa zawadi ya Sh 10,000 na shabiki mmoja kutokana na mchezo wake,"ilisema taarifa ya Kamwaga.
    Kamwaga amesema mashabiki walifahamu kuwa matokeo yale ya 1-1 yalikuwa ni sehemu ya mchezo na kwamba taarifa za kuwapo kwa vurugu zimetiwa chumvi kwa sababu ambazo klabu yetu haizifahamu.
    Amesema Simba SC inaomba mashabiki wake wawe watulivu na werevu katika wakati huu ambao timu inajiandaa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. "Umoja wa washabiki ndiyo utakaosaidia na si mtengamano,"amesema.
    Amesema timu itarejea Dar es Salaam Jumatano kutoka Arusha ambako imeweka kambi ya kujiandaa na mechi dhidi ya Libolo ya Angola.
    Mechi hiyo imepangwa kufanyika Jumapili ijayo (Februari 17) kuanzia saa 10:30 jioni na uongozi unafanya utaratibu wa kuiwezesha timu kufanya mazoezi katika Uwanja wa Taifa walau mara moja kabla ya mechi hiyo ili kutoa nafasi kwa benchi la ufundi kutoa maelekezo mahususi kwa wachezaji kuhusiana na mechi hiyo.
    Amesema Kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Talib Hilal anaelekea Arusha leo ili kuongeza nguvu ya benchi la ufundi la Wekundu wa Msimbazi. 
    Hii si mara ya kwanza kwa Talib kuongeza nguvu kwenye benchi la ufundi la Simba kwani alifanya hivyo pia miaka kumi iliyopita wakati klabu hiyo ilipocheza na Zamalek ya Misri na kufanikiwa kuitoa mwaka 2003.
    Kamwaga ametahadharisha Talib Hilal hajaja kuchukua nafasi ya mtu yeyote kwenye benchi la ufundi, bali amekuja kwa mapenzi yake kwa Simba na mara zote klabu inamkaribisha kwa vile uwezo wake kitaaluma, uzoefu wake na uwezo wake katika kuhamasisha unakubalika ndani ya klabu.
    Amesema Simba SC inaomba mashabiki na vyombo vya habari waisaidie klabu kwa kutotoa taarifa zenye kuashiria migogoro isiyokuwepo, kwani Simba wanawakilisha heshima na hadhi ya Tanzania katika mashindano haya.
    "Unachoomba uongozi wa klabu ni uzalendo kwa taifa letu walau katika kipindi hiki ambapo kinachoangaliwa ni utaifa wetu. Uongozi unaomba wadau wake wa vyombo vya habari kuandika habari za kujenga umoja, mshikamano na uzalendo kwa Watanzania wote ili hatimaye Simba ifanye vizuri,"amesema.
    Katika hatua nyingine, Kamwaga amesema Simba inakaribisha wafanyabiashara na makampuni kujitokeza kuidhamini mechi hii kwa njia ya matangazo.
    Amesema uongozi umeamua kuuza haki za kutangaza katika Uwanja wa Taifa itakapochezwa mechi hiyo kwa wote wanaotaka kuisaidia Simba.
    "Nafasi zinazouzwa ni za kutandaza mabao pembeni ya uwanja, kutangaza kwenye televisheni kubwa iliyopo uwanjani na nje ya uwanja. Wadhamini pia watapata fursa ya kutangazwa kupitia vyombo vya habari.Mechi hii inasubiriwa kwa hamu na watu zaidi ya milioni 15 ndani na nje ya Tanzania. Ni fursa ya kipekee kwa wafanyabiashara na makampuni kujitangaza,"amesema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA AMANI TUPU ARUSHA, NGASSA AZAWADIWA FEDHA, TALIB ATUA KAMBINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top