WAKATI fulani, Sir Robert ‘Bobby’ Charlton aliwahi kusema; “Watu fulani wananiambia kwamba, sisi wachezaji wa kulipwa ni watumwa wa soka. Vema, ikiwa huu ni utumwa, nipeni kifungo cha maisha,”.
Natambua, kwa vijana na wanasoka wengi wa kizazi cha sasa wanamsikia tu Bobby Charlton- huyu ni mwanasoka wa zamani wa kimataifa wa England, anayepewa heshima ya moja ya viungo bora kuwahi kutokea chini ya jua daima.
Alikuwamo katika kikosi cha England kilichotwaa Kombe la Dunia mwaka 1966 na pia akatwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Ulaya mwaka huo. Muda wake mrefu uwanjani, aliitumikia klabu ya Manchester United, ambako alijijengea umaarufu mkubwa kwa staili yake ya kushambulia na kutoa pasi nzuri katika eneo la kiungo sambamba na upigaji wake wa mashuti ya mbali.
Kwa waliobahatika kumuona huyu mtu, wanasema alikuwa fiti sana na mwenye stamina ya kutosha.
Bado nipo na wanasoka wa Tanzania na leo nataka nimzungumzie kijana mmoja anayevaa jezi namba mbili katika kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, akicheza nafasi ya kiungo.
Amefikia kwenye kiwango cha juu cha ubora kwa sasa katika soka ya Tanzania, akiwa ana namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Taifa Stars nani tegemeo la timu.
Kama kikosi cha Stars kitashuka dimbani kwa sasa bila ya huyu mvaa jezi namba mbili, dhahiri mashabiki watasikitika. Lakini pia, hata kocha Kim Poulsen iwapo itatokea siku hataweza kumtumia kijana huyo kwa dharula, atasikitika sana.
Kwa alipofikia sasa huyu kijana, mchezaji tegemeo wa klabu yake na Taifa Stars kwa Tanzania amemaliza. Ndiyo amemaliza na kinachofuata ni kusubiri kushuhudia kuporomoka kwake kisoka.
Kwa nini tusubiri hilo? Hapo ndipo ninapoyakumbuka maneno ya Bobby Charlton; “Watu fulani wananiambia kwamba, sisi wachezaji wa kulipwa ni watumwa wa soka. Vema, ikiwa huu ni utumwa, nipeni kifungo cha maisha,”.
Huyu kijana naye achague kifungo cha maisha kama anataka kufika mbali kisoka na kuvuna mafanikio zaidi, ikibidi hata kucheza Ulaya.
Na ukitazama soka kweli ni utumwa. Kila siku uamke asubuhi kufanya mazoezi na pengine urudie tena baadaye. Muda mrefu unakuwa kambini ukijiandaa na michezo. Huna muda wa kutosha wa kukaa na familia yako nyumbani.
Ni wewe na soka, soka na wewe. Unapata muda kidogo sana wa kuburudisha nafasi yako. Mke, au mpenzi wako anawasiliana na wewe zaidi kwa simu kulikoni kuwa pamoja nawe katika kalenda ya mwaka.
Ni mchezo ambao wakati mwingine unakera- yaani ni utumwa kabisa. Lakini uzuri wa utumwa wa soka ni kwamba, unakuwa na miaka takriban 10 ya kuishi katika hali fulani pengine usiyoipenda, ila baada ya kupumzika na kutungika daluga zako, akaunti yako ina fedha nyingi ulizokuwa unalipwa wakati unacheza, tayari umenunua ardhi ya kutosha, una nyumba kadhaa, miradi mingi iliyotokana na fedha ulizokuwa unalipwa wakati unacheza soka, unaishi kifahari.
Katika makala yangu iliyopita nilizungumzia juu ya wanasoka wetu kuwa na matarajio bila malengo na leo ni kama nawasilisha mwendelezo wa makala hiyo.
Kama huyo kijana alifika hapa alipofika kwa bahati, kwa sababu alikuwa hana kitu kingine cha kufanya akaamua aelekeze nguvu zake kwenye soka, sasa atambue amepata dira ya maisha yake na kinachofuata ni kujiwekea malengo.
Ahakikishe anakuwa katika kiwango kizuri kila wakati, kwa kutia bidii katika mazoezi, kufanyia kazi mapungufu yake ambayo walimu wake wamekuwa wakimuambia. Kudumisha nidhamu, usikivu na kuhakikisha kwa namna yoyote halewi sifa na kubweteka.
Ukishakuwa mchezaji mzuri na maarufu kama huyo kijana, unalipwa mshahara mzuri na klabu, kwa desturi ya wanasoka wa Kitanzania kinachofuata ni anasa, ambayo itakumaliza mapema sana na kupoteza yote, uzuri wa uchezaji na umaarufu, hatimaye ajira yenyewe.
Bado nina shaka kuhusu huyo kijana, nani rafiki zake, nani watu wake wa karibu na huwa wanamuambia nini. Huwa wanamshauri nini. Kama wanamuambia akiongeza bidii anaweza kucheza Ulaya na kuchuma mali kupitia soka, itakuwa vizuri.
Lakini kama wanamtongozea mademu tu na kumshawishi kutumbukia kwenye bwawa la anasa, ulevi, uvutaji bangi, hiyo mbaya sana na muda si mrefu taifa litapoteza.
Najua kwa sasa kijana huyo anawatamani akina Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanapokutana katika kambi ya Taifa Stars, wakitokea DRC wanakochezea TP Mazembe ambayo inawalipa vizuri. Lakini kama naye ataamua kuwa mtumwa kweli wa soka ana akajituma kwa malengo ya kufika mbali, iko siku akina Samatta watamtamani yeye wakati anarejea nyumbani akitokea Ulaya kuja kuichezea Taifa Stars.
Naam, umefika wakati nimfichue sasa huyo kijana, ni kijana aliyerithi viatu vya baba yake, Abubakar Salum ‘Sure Boy’, naye anaitwa Salum Abubakar akitumia jina lile lile la utani la baba yake, ‘Sure Boy Jr.’. Anayevaa jezi namba mbili (2) Taifa Stars. Hadi Jumapili tukijaaliwa.



.png)