Na Mahmoud Zubeiry
ALIYEKUWA kocha wa Yanga SC, Mbelgiji Tom Saintfiet ameomba kuwa kocha mpya wa timu ya soka ya taifa ya Uganda, The Cranes arithi mikoba ya Mscotland, Bobby Williamson aliyetimuliwa na Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA) mapema wiki hii.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY kwa simu jana usiku, Saintfiet ambaye pia alifanya kazi kwa miaka miwili na nusu kama kocha wa Namibia, baadaye Ethiopia na Yemen alisema atafurahi akipata mkataba wa kufundisha Uganda.
“Nimekuwa nikifuatilia soka ya Uganda kwa miaka kadhaa. Ni moja ya timu za kuvutia katika Bara hili na wachezaji wana uwezo mkubwa”, alisema. “Wakati nafundisha Ethiopia, Niliwaona walipokuja kucheza mashindano ya CECAFA, na nilipokuwa nafundisha Yanga SC nchini Tanzania, nilikuwa nina mmoja wa wachezaji wao kikosini (Hamisi Kiiza), ambaye alikuwa mzuri haswa. Pamoja naye, tulicheza naye na tukashinda Kombe la Kagame mwaka jana,”alisema.
“Mwakilishi wangu amezungumza na uongozi wa FUFA, chini ya Mulindwa, ambaye anaitakia mafanikio nchi yake, na wakikubaliana nitakutana naye mara moja kujadiliana namna ya kuiwezesha Uganda kwenda Brazil mwaka 2014, na Morocco kwenye AFCON mwaka unaofuata”, alisema.
Saintfiet, mwenye umri wa miaka 40 tu, amesema Uganda imeshindwa kufuzu kwenye mashindano makubwa katika miaka ya karibuni kutokana tu na kukosa bahati.
“Lakini sasa ni wakati wa kuwapeleka anga nyingine,” alisema. “Wanaweza kufanya hivyo, na ninataka kuwasaidia. Uganda inazidiwa pointi tatu tu na vinara wa kundi lao katika kuwania tiketi ya kucheza Kombe la Dunia, na kama watashinda mechi mbili za nyumbani dhidi ya Liberia na Angola Juni, itabadilisha msimamo wa Kundi”.
Saintfiet ni kocha wa kiwango cha juu, mwenye leseni ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) na uzoefu wa miaka 17 kazini licha ya umri wake mdogo. Mwaka jana aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Nigeria, kabla ya siasa kumuengua katika nafasi hiyo.
Alifanya kazi Yanga kwa miezi miwili tu na ushei, kabla ya kutofautiana na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Alhaj Yussuf Manji na kuamua kuondoka zake, akiiachia klabu taji la Kagame kabla ya siku chache kuibukia Yemen alikofanya kazi tangu Oktoba hadi wiki iliyopita alipoachia ngazi.



.png)