![]() |
Juma Kaseja akipewa mazoezi na kocha wa makipa wa Simba SC, James Kisaka |
Na Mahmoud Zubeiry
NAHODHA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Juma Kaseja anamaliza mkataba wake katika klabu yake, Simba SC Juni mwaka huu na hadi sasa hakuna mazungumzo yaliyofanyika kuhusu mkataba mpya. Kaseja mwenyewe ameithibitishia BIN ZUBEIRY katika mahojiano yaliyofanyika leo Dar es Salaam. Endelea.
![]() |
Kaseja wa kwanza kulia waliosimama katika kikosi cha Taifa Stars |
BIN ZUBEIRY: Habari za Ijumaa Nahodha
KASEJA: Nzuri, na wewe?
BIN ZUBEIRY: Njema, vipi mnaendeleaje Simba SC?
KASEJA: Hivyo hivyo, tunaendelea na mazoezi kujiandaa na mechi ijayo
BIN ZUBEIRY: Mnacheza na Azam ambayo inawania ubingwa dhidi ya Yanga, mtatoka?
KASEJA: Huu mpira, hata sisi tunawania nafasi. Tutakwenda kushindana kupigania matokeo mazuri.
BIN ZUBEIRY: Mna timu ya kuweza kusimama na Azam kweli kwa sasa?
KASEJA: Kwa nini hatuna? Simba ni nzuri, tena kuliko watu wanavyofikiria. Tukijipanga sisi wazuri sana, basi tu matatizo ya mgogoro na mgawanyiko wa uongozi tu.
BIN ZUBEIRY: Na hayo ndiyo yamesababisha kuyumba kwenu msimu huu?
KASEJA: Dhahiri kaka, huhitaji kwenda shule ili ujue hilo
BIN ZUBEIRY: Kwa hivyo mnacheza Ligi Kuu ili mmalize tu, lakini hamna matumaini yoyote…
KASEJA: Sisi bado tunapambana, hilo ndilo ninaloweza kukuambia
BIN ZUBEIRY: Huu ni mwaka wa 10 uko Simba SC pamoja na ule mmoja ambao uliondoka kwenda Yanga SC, nini siri ya mafanikio yako?
KASEJA: Nidhamu, kujituma, bidii ya mazoezi, ubunifu na uvumilivu pia.
BIN ZUBEIRY: Mchezaji unahitaji kuwa vipi ili ucheze muda mrefu katika soka ya Tanzania.
KASEJA: Jifanye mjinga, utacheza muda mrefu sana. We angalia tu, wale waliojifanya wajanja wako wapi sasa hivi.
BIN ZUBEIRY: Ni Nahodha wa Simba SC haifanyia vizuri kwa sasa, lakini wakati huo huo ni Nahodha wa Taifa Stars inayofanya vizuri kwa sasa, unajisikiaje?
KASEJA: Upande mmoja najisikia faraja kwa matokeo ya timu ya taifa, na kila siku nasema hakuna Mtanzania ambaye hapendi furaha, matokeo mazuri yakipatikana furaha inaanzia kwa wachezaji. Kwa Simba SC inaniumiza, lakini hii ni hali ya kupita tu.
BIN ZUBEIRY: Una muda gani zaidi katika mkataba wako na Simba SC?
KASEJA: Miezi miwili kitu kama hicho, Juni namaliza Mkataba
BIN ZUBEIRY: Umekwishafanya mazungumzo ya mkataba mpya na Simba SC?
KASEJA: Bado, na pia nadhani muda bado upo
BIN ZUBEIRY: Ikitokea timu inataka kukutoa Simba SC kwa wakati huu iwe ya nje au hapa nyumbani, utakubali?
KASEJA: Nitaangalia maslahi tu…kama Simba SC watakuwa na ofa nzuri katika mkataba wao mpya watakaonipa, sitakuwa na sababu ya kuhama timu.
BIN ZUBEIRY: Mwenyewe umepanga kutungika glavu zako lini
KASEJA: Hadi nitakapoona nimechoka, ila kwa sasa bado bado sana. Tena nasijikia vizuri ile mbaya
BIN ZUBEIRY: Changamoto gani inayokuumiza zaidi katika maisha yako ya soka
KASEJA: Soka ni mchezo mgumu sana, nyinyi Waandishi ndio pasua kichwa wa kwanza, natamani siku moja mcheze nyinyi halafu sisi wachezaji tuandike…
BIN ZUBEIRY: Kwa nini?
KASEJA: Mnawavuruga sana wachezaji, kwa mfano utasikia sasa watu wanaandika Kaseja mzee, mimi na Gianluigi Buffon nani mzee?
BIN ZUBEIRY: Tuachane na hayo Juma, unadhani Taifa Stars ina nafasi ya kwenda Brazil 2014?
KASEJA: Kwa hapa tulipo sasa, tuna pointi sita baada ya kucheza mechi tatu. Tunazidiwa pointi moja na Ivory Coast inayoongoza kundi letu, naweza kusema tuna nafasi.
BIN ZUBEIRY: Nini kinakufurahisha zaidi katika Taifa Stars kwa sasa?
KASEJA: Kocha (Kim Poulsen) anafanya kazi yake vizuri kwa pamoja na bechi lake zima la ufundi.
BIN ZUBEIRY: Zaidi ya hapo?
KASEJA: Wakubwa wanafanya kazi nzuri na kuna wachezaji vijana wanajituma sana kama Sure Boy, Domayo, Kapombe, Msuva, Aishi, Issa Rashid…hawa wanaibeba sana timu kwa sasa
BIN ZUBEIRY: Mtakwenda Morocco kurudiana nao, na baadaye mtaikaribisha Ivory Coast hapa…nini matarajio?
KASEJA: Mechi zote zitakuwa ngumu, lakini tutakwenda kupambana kwa nguvu zetu zote tupate matokeo mazuri
BIN ZUBEIRY: Hizo glavu za Nike unazotumia ni sawa kabisa na zile anazotumia Wojciech Szczesny wa Arsenal?
KASEJA: Kabisaa, hizi nilizinunua Dubai kabla ya mechi na Cameroon dola (za Kimarekani) 220. Kwa faida zaidi, hizi pia ni glavu ambazo anavaa Victor Valdes wa Barcelona na De Gea wa Man United…
BIN ZUBEIRY: Ulipanda ndege kwenda Dubai kununua glavu tu?
KASEJA: Hapana, niliziagiza…zikafikishwa hapa
![]() |
Kaseja na glavu na iatu vyake vya Nike |
BIN ZUBEIRY: Na hivi viatu ni Nike pia..
KASEJA: Ndiyo, ni viatu sawa na ambavyo wanavaa wachezaji wengine wakubwa duniani kama Cristiano Ronaldo…
BIN ZUBEIRY: Huna ulichosahau Yanga?
KASEJA: Haaa haaa…sina uhakika
BIN ZUBEIRY: Utastaafu ukiwa hapa hapa Msimbazi?
KASEJA: Hiyo tena mipango ya Mungu…
BIN ZUBEIRY: Na ukistaafu, utahamia kwenye shughuli gani?
KASEJA: Kwa kiasi kikubwa nitakuwa kocha
BIN ZUBEIRY: Utapenda na wanao wacheze mpira?
KASEJA: Kipaumbele kwa wanangu ni elimu zaidi, kama wakipenda kucheza siwezi kupambana nao…nitawaacha
BIN ZUBEIRY: Juma nashukuru sana kwa leo, naomba nikuage
KASEJA: Asante sana, nashukuru pia na ninakutakia kazi njema..
BIN ZUBEIRY: Asante, na wewe pia kila la heri
KASEJA: Amin.
![]() |
Kaseja akizungumza na Waandishi |