![]() |
Stewart Hall, kocha aliyeleta mafanikio Azam |
Na Mahmoud Zubeiry
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Brian Umony kesho anatarajiwa kurejea uwanjani wakati timu yake, Azam FC ikimenyana na Barack Young Controllers II katika mchezo wa marudiano wa Raundi ya Pili Kombe la Shirikisho Afrika.
Kocha wa Azam FC, Muingereza Stewart Hall ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, Umony amepona na amekwishaanza mazoezi na wenzake.
“Tungeweza kumtumia hata kwenye mechi na Ruvu Shooting wiki iliyopita, lakini tuliamua kumuacha apone sawasawa, na sasa yuko fiti kabisa na kesho anaweza kucheza,”alisema Hall.
![]() |
Umony; Amerudi |
Umony aliumia dakika ya tisa katika mechi ya kwanza ya Raundi ya Kwanza ya michuano hiyo dhidi ya Al Nasir ya Sudan Kusini na tangu wakati huo hajagusa mpira.
Kwa upande mwingine, Hall amesema maandalizi ya mchezo huo kwa ujumla ni mazuri na wana matumaini makubwa ya kushinda tena.
“Timu iko vizuri kabisa na tunaomba wapenzi wa soka wajitokeze kwa wingi kutushangilia kesho, tutawapa burudani nzuri na watafurahia,”alisema.
Azam inahitaji hata sare kesho, kwani katika mchezo wa kwanza ilishinda 2-1 ugenini na kuwa timu ya pili ya Tanzania kushinda Magharibi mwa Afrika, baada ya Simba SC mwaka 1974 kuifunga Hearts Of Oak mwaka 1974.