![]() |
| Babu Mfaransa; Patrick Liewig na kazi bila mshahara Simba SC |
Na Mahmoud Zubeiry
KUKOSEKANA kwa mtu mbadala wa kusaini hundi na stakabadhi mbalimbali za klabu ya Simba hivi sasa, badala ya Makamu Mwenyekiti Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ aliyejiuzulu ndiyo sababu ya kuchelewa kwa mishahara ya kocha Mfaransa, Patrick Liewig.
Liewig hajalipwa mishahara kwa miezi miwili sasa na anaishi na kufanya kazi katika mazingira magumu nchini, yeye na mkewe akiwa amepangiwa katika hoteli ya Spice, Kariakoo, Dar es Salaam.
Kocha huyo wa zamani wa akademi ya PSG ya Ufaransa na klabu ya ASEC Mimosa ya Ivory Coast, amekuwa akilalamikia hali hiyo na kusema anataka kikao na Mwenyekiti wa klabu, Alhaj Ismail Aden Rage azungumzie mustakabali wake.
“Tupo katika mchakato wa kubadilisha mtu wa kusaini atakayechukua nafasi ya Kaburu, taratibu zikikamilika, kocha atalipwa mshahara wake,”alisema kiongozi mmoja wa Simba, ambaye aliomba asitajwe jina.
Lakini wakati huo huo, Simba SC inaweza kuachana na kocha huyo wakati wowote na akidumu sana ni hadi baada ya Ligi Kuu.
Sababu kubwa ni klabu kutokuwa katika nafasi ya kulipwa kocha wa kigeni kwa sasa, haswa Wazungu ambao wanalipwa mamilioni mengi.
Simba SC pia inataka kupunguza idadi ya watu katika benchi lake la ufundi na mwishoni mwa msimu mmoja kati ya Mganda, Moses Basena au mzalendo Jamhuri Kihwelo anaweza kupewa mkono wa kwaheri ili kubana bajeti.
Katika hatua nyingine, Nahodha wa zamani wa Simba SC, Nico Nyagawa amepewa nafasi ya Umeneja Vifaa wa klabu, kufuatia kuachia ngazi kwa Kessy Rajab. Tayari Nyagawa amekwishaanza kazi.
Hadi sasa, Liewig amekwishaiongoza Simba SC katika mechi 20, akiiwezesha kushinda saba, sare sita na kufungwa saba tangu aanze kazi Januari mwaka huu, akirithi mikoba ya Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick.
REKODI YA LIEWIG SIMBA SC:
P W D L GF GA GD Pts
Simba 20 7 6 7 25 24 1 27
MECHI ZA SIMBA CHINI YA LIEWIG:
Simba SC 4-2 Jamhuri (Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 1-1 Tusker FC (Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 1-1 Bandari (Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 0-1 U23 Oman (Kirafiki)
Simba SC 1-3 Qaboos (Kirafiki)
Simba SC 2-1 Ahly Sidab (Kirafiki)
Simba SC 0-1 Black Leopard (Kirafiki)
Simba 3-1 African Lyon (Ligi Kuu)
Simba SC 1-1 JKT Ruvu (Ligi Kuu)
Simba SC 1-1 JKT Oljoro (Ligi Kuu)
Simba SC 0-1 Rec. de Libolo (Ligi ya Mabingwa)
Simba SC 1-0 Prisons (Ligi Kuu)
Simba SC 0-1 Mtibwa Sugar (Ligi Kuu)
Simba SC 0-4 Rec. de Libolo (Ligi ya Mabingwa)
Simba SC 2-1 Coastal Union (Ligi Kuu)
Simba SC 1-0 CDA (Kirafiki)
Simba SC 4-0 Singida United (Kirafiki)
Simba SC 1-1 Rhino FC (Kirafiki)
Simba SC 0-1 Kagera Sugar (Ligi Kuu)
Simba SC 2-2 Toto Africans (Ligi Kuu)



.png)