![]() |
Sure Boy kulia akipongezwa na Kocha Msaidizi wa Simba SC, Jamhuri Kihwelo 'Julio' jana Taifa |
Na Saada Akida
KIUNGO Salum Abubakar ‘Sure Boy’ jana ameendelea kudhihirisha yeye ni kiungo bora kabisa Tanzania, baada ya kufanikiwa kufikisha kwa ufasaha pasi 37 kati ya 40 alizopiga, wakati klabu yake, Azam FC ikimenyana na Simba SC, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, timu hizo ziligawana pointi kwa sare ya 2-2, mabao ya Simba SC yote yakifungwa na Ramadhani Singano ‘Messi’ na Azam yalifungwa na Kipre Tchetche kwa penalti na Humphrey Mieno.
Sure aling’ara jana uwanjani na kumfunika kiungo wa Simba SC, ‘dogo’ Abdallah Seseme, ambaye hata hivyo alijitahidi kwa kutoa kwa ufasaha pasi 19 kati ya 25.
Sure, mtoto wa winga wa zamani wa kimataifa Tanzania, Abubakar Salum pamoja na kufuzu katika katika mtihani wa pasi bora, lakini ameendelea kupoteza makali ya upigaji mashuti.
Msimu uliopita, Sure alikuwa mmoja wa wachezaji tishio kwa upigaji mashuti makali na kufunga pia, lakini jana alifumua shuti moja tu dakika ya 36 ambalo lilikwenda nje.
Mwinyi Kazimoto wa Simba SC aliyetokea benchi dakika ya 69 kwenda kuchukua nafasi ya William Lucian ‘Gallas’ aliweza kutoa pasi tano tu kwa ufasaha kati ya saba ndani ya dakika zake 21+5 za kuwapo kwake uwanjani.
Lakini Mwinyi pia alifanikiwa kupiga shuti zuri lililolenga lango, ingawa likaokolewa na kipa Mwadini Ally.
Mashabiki jana walitarajia burudani kubwa na nzuri tangu mwanzo wa mchezo sehemu ya katikati ya Uwanja kwa mchuano wa ufundi wa kuchezesha timu baina ya Sure na Mwinyi, lakini mambo yakawa tofauti baada ya kiungo wa Simba kuanzia benchi.
Wawili hao wote wapo timu ya soka ya taifa ya Tanzania na huchezeshwa kwa pamoja na kiungo wa Yanga, Frank Domayo na kufanya safu moja hatari sana ya kiungo Taifa Stars ambayo sasa imekuwa tishio barani Afrika.