![]() |
| Analo: Nsa Job abanwa |
Na Prince Akbar
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limemtaka mshambuliaji Nsa Job Mahenya wa Coastal Union kuwasilisha maelezo yake juu ya madai kuwa alipewa rushwa ya sh. milioni mbili ili asiifunge moja ya timu vigogo vya soka nchini.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura Mgoyo amesema leo kwamba, Job alikaririwa Aprili 3 mwaka huu na kituo cha redio cha Clouds FM katika kipindi cha Amplifier kuwa alipewa kiasi hicho cha fedha na kiongozi wa timu husika ili asiifunge katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom, lakini alipokea fedha hizo na kuifunga timu hiyo.
Wambura amesema lakini Nsa alilalamika baadaye kiongozi huyo alikuwa akimtaka arejeshe fedha hizo.
Amesema pia TFF imekiandikia kituo hicho cha redio kutaka nakala ya kipindi hicho ili pamoja na maelezo ya mshambuliaji huyo vipelekwe katika Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya hatua za kinidhamu.
“TFF itachukua hatua kali dhidi ya Job iwapo hatawasilisha maelezo yake kuhusiana na suala hilo, na imetaka wadau kutoa ushirikiano ili iweze kupambana kikamilifu na vitendo vya rushwa kwenye mpira wa miguu,”amesema.
TFF inaonekana kuanza kuvalia njuga madai kuhusu rushwa katika soka ya Tanzania, baada ya kufumbia macho kwa muda mrefu.
Kipa Shaaban Kado wa Coastal, wakati akiwa Mtibwa Sugar aliwahi kudai kupelekewa fedha na mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Ulimboka Mwakingwe, aliyetumwa na kiongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi, ili aachie mabao katika mechi baina ya timu hiyo.
Hata hivyo, pamoja na suala hilo kufikishwa kwenye vyombo vya sheria hakuna hatua zaidi zilizowahi kuchukuliwa.
Wachezaji wanne wa Azam FC, kipa Deo Munishi ‘Dida’ na mabeki Erasto Nyoni, Aggrey Morris na Said Mourad wa Azam FC, kwa sasa wamesimamishwa na klabu yao, kwa tuhuma za kuihujumu timu hiyo dhidi ya Simba katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ikafungwa 3-1.
Lakini suala la wanne hawa kwa sasa lipo kwenye meza ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).



.png)