• HABARI MPYA

    Wednesday, April 03, 2013

    TUSAHAU KUHUSU NGASSA, NA HAO AKINA DOMAYO, SURE BOY JE?


    KOCHA Luiz Felipe Scolari alitua Chelsea Julai 1, mwaka 2008 na kuwa kocha wa kwanza mshindi wa Kombe la Dunia kufanya kazi Ligi Kuu ya England. 
    Na alipoulizwa kama ni fedha ndizo zimemshawishi, akasema; “Ndiyo, hiyo ni moja ya sababu,”. Lakini akaongeza; “Nina umri wa miaka 59 na sitaki kufanya kazi hadi umri wa miaka 70. Nataka kustaafu ndani ya miaka minne au mitano, ijayo, hivyo ni sababu za kifedha, lakini kuna vitu vingine,”alisema.

    Unajua kuna nini hapa? Malengo. Luiz Felipe Scolari alijiwekea malengo ya kutofanya kazi hadi umri wa miaka 70 na katika siku za mwisho za maisha yake ya kazini, akaamua kuweka fedha mbele.
    Amekwishashinda Kombe la Dunia, anataka nini tena? Kustaafu akaunti yake haina akiba ya kutosha au kuendelea kufanya kazi hadi kifo, ili mradi apate fedha za kujikimu?
    Kujiwekea malengo katika maisha ni kipimo cha ufanisi wa mambo yako- hayo yalikuwa malengo ya mwishoni ya Scolari, lakini ya mwanzo yalitimia. Kuwa kocha bora na kushinda mataji makubwa. Ameshinda hadi Kombe la Dunia.
    Nimefanya mahojiano na wanasoka wengi nchini hadi sasa tangu nimeanza kazi hii ya Uandishi wa Habari na wengi waliniambia matarajio yao ya baadaye ni kucheza soka la kulipwa Ulaya.
    Hata Sekilojo Johnson Chambua aliniambia hivyo- lakini alipata ofa ya mshahara mzuri Uarabuni mwaka 1999 akaizembea na kubaki Yanga.  
    Jumapili wiki hii, mwanasoka nyota wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa ametimiza miaka 23 na akafanya sherehe ya Maulid nyumbani kwao Mwanza akifurahia mafanikio yake.
    Kwa hapa nyumbani, Ngassa amemaliza. Amecheza klabu tatu kubwa, Simba, Yanga na Azam ni mchezaji aliyefanya makubwa timu ya taifa. Amekuwa mfungaji bora wa mashindano mbalimbali, kuanzia Ligi Kuu hadi michuano ya CECAFA. Amebakiza nini?
    Amejenga  nyumba kadhaa mjini na kununua magari kadhaa ya kifahari. Kwa hapa nyumbani, Ngassa ni mchezaji wa kiwango cha juu.
    Huyu ni mchezaji ambaye amewahi kuvutia katika majaribio Ulaya na Amerika, lakini mwili wake mdogo ukamkosesha ulaji. Aprili mwaka 2009, Ngassa alifanya majaribio West Ham United ikiwa Ligi Kuu ya England.
    Baadaye mwaka juzi alikwenda Marekani kufanya majaribio Seattle Sounders FC na akapewa nafasi ya kucheza dhidi ya Manchester United katika mchezo wa kirafiki akitokea benchi.
    Kikubwa ambacho nimejifunza kutoka kwa wanasoka wa Tanzania, wengi wao wana matarajio bila malengo na kwa sababu hii hawawezi kufika mbali. Mafanikio kidogo tu mtu analewa sifa, bidii ya mazoezi inashuka, nidhamu inakuwa mbovu- na soka inamkimbia mara moja.
    Matarajio yanaambatana na malengo. Lazima kuwe na malengo pamoja na mikakati ya kutimiza hayo malengo. Ngassa nilifanya naye mahojiano mwaka 2005 wakati anaibuka Kagera Sugar na akaniambia matarajio yake ni kucheza soka ya kulipwa Ulaya.
    Lakini unaweza kuona, baada ya kupata mafanikio ya hapa nyumbani, kuvaa jezi za Simba, Yanga na Azam kushika fedha zilizobadilisha maisha yake ni kama ameridhika hivi.
    Ngassa amepata ofa nyingi hadi Ulaya, sahau kuhusu ile ya El Merreikh ya Sudan mwaka jana, lakini amekataa. Anakataa na juzi kasherehekea miaka 23 ambayo ni umri wa Andre Ayew ambaye tayari anawika Ulaya katika klabu ya Marseille ya Ufaransa.
    Ngassa anakuwa mfano tu hapa, lakini vipi wanasoka wengine wanaochipukia kwa sasa wenye umri chini ya miaka 20 kama akina Frank Domayo, Salum Abubakar, Haruna Chanongo na Simon Msuva, matarajio yao yanaambatana na malengo? Alamsiki.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: TUSAHAU KUHUSU NGASSA, NA HAO AKINA DOMAYO, SURE BOY JE? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top