![]() |
Azam; Watahukumiwa na Wacomoro |
Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limeteua waamuzi watakaochezesha mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho kati ya Azam na Barrack Young Controllers II ya Liberia itakayochezwa Jumamosi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwamuzi wa kati ni Adelaide Ali, mwamuzi msaidizi namba moja ni Amaldine Soulaimane wakati Ibrahim Mohame atakuwa mwamuzi msaidizi namba mbili. Mwamuzi wa mezani (fourth official) ni Ansudane Soulaimane.
Kamishna wa mechi hiyo itakayoanza saa 10.30 jioni atakuwa Abdelhamid Radwan kutoka Misri. Maofisa hao wa mechi hiyo watafikia kwenye hoteli ya Holiday Inn.
Barrack Young Controllers II imewasili nchini leo saa 3.35 asubuhi kwa ndege ya PrecisionAir ikitokea Nairobi, Kenya ilipounganisha safari hiyo iliyoanzia Monrovia kupitia Accra, Ghana.
Timu hiyo imefikia katika hoteli ya Sapphire Court na kesho itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume ikiwa ni sehemu ya maandalizi yake kwa ajili ya mechi hiyo huku wapinzani wao Azam wakiendelea kujinoa kwenye uwanja wao wa Azam Complex.