Na Princess Asia, DAR ES DALAAM
KOCHA wa Mkuu wa Azam FC, George ‘Best’ Nsimbe amesema kwamba haumizwi kichwa na Simba na Yanga na kwamba mechi zinazomuumiza kichwa kati zilizobaki za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ni dhidi ya Stand United na Mgambo JKT.
Tangu aanze kukaimu Ukocha Mkuu wa Azam FC miezi miwili iliyopita kufuatia kufukuzwa kwa aliyekuwa bosi wake, Mcameroon Joseph Marius Omog, Nsimbe ameshinda michezo minne na kutoka sare tatu.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, kocha huyo wa Uganda amesema kwamba lengo lake ni kuhakikisha timu yake inashinda michezo yote iliyobaki ili kutetea ubingwa.
Lakini Nsimbe amesema kwamba anaamini mchezo dhidi ya Stand United ni mgumu kuliko mechi dhidi ya Simba na Yanga.
“Simba na Yanga ni timu za kawaida, hivyo sina presha nazo, mechi ngumu kwangu ni za Stand na Mgambo, timu ambazo ziko chini zinahitaji kupata matokeo mazuri ili kujiweka nafasi nzuri”, alisema.
Azam FC jana walizinduka kutoka kwenye sare tatu mfululizo, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, mabingwa hao watetezi wametimiza pointi 42, baada ya kucheza mechi 22, nyuma ya vinara, Yanga SC wenye pointi 46 za mechi 21.
0 comments:
Post a Comment