• HABARI MPYA

    Sunday, April 19, 2015

    KWA MPIRA ULE, YANGA WAKIENDA TUNISIA AIBU!

    MASHABIKI wa Yanga SC jana walitoka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kama waliomwagiwa maji, kufuatia timu yao kulazimishwa sare nyumbani ya kufungana bao 1-1 na Etoile du Sahel ya Tunisia.
    Yanga SC sasa imejiwekea mazingira magumu ya kusonga mbele kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya sare hiyo katika mchezo wa kwanza hatua ya 16 Bora.
    Yanga SC inatakiwa kulazimisha sare ya kaunzia 2-2 au ushindi wa ugenini kabisa ndiyo itavuka katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo, ambako itacheza na moja ya timu zitakazotolewa katika Ligi ya Mabingwa.
    Yanga SC waliuanza vizuri mchezo wa jana kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la mapema dakika ya pili, mfungaji Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwa penalti, baada ya winga Simon Msuva kuangushwa kwenye boksi.

    Yanga ilishambulia kwa dakika mbili zaidi baada ya bao hilo, lakini kutoka hapo, Etoile wakauteka mchezo kutokana na kutawala sehemu ya kiungo.
    Yanga SC walikuwa wakipitishia mashambulizi yao pembeni kupitia kwa mawinga wake, Msuva na Mrisho Ngassa, lakini mshambuliaji Amissi Tambwe hakuwa katika ubora wake.
    Kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ alifanya kazi nzuri kipindi cha kwanza kuokoa michomo kadhaa ya hatari, lakini akafungwa bao rahisi kipindi cha pili.
    Mwishoni mwa kipindi cha kwanza, Yanga SC ilipata pigo baada ya Nahodha wake, Cannavaro kuumia mguu, jambo ambalo lilimlazimu kutorejea uwanjani kipindi cha pili, nafasi yake ikichukuliwa na Said Juma Makapu.
    Baada ya mabadiliko hayo, Mbuyu Twite alikwenda kucheza beki ya kati pamoja na Kevin Yondan, huku Makapu akienda kucheza kama kiungo mkabaji.
    Dakika mbili tu baada ya kuanza kipindi cha pili, Etoile waliata bao la kusawazisha kupitia kwa Ben Amor Med Amine aliyefumua shuti kali akiwa nje ya boksi baada ya kumsoma Barthez aliyekuwa amezubaa langoni.      
    Bao hilo la mapema kipindi cha pili liliwachanganya Yanga SC na kuvuruga kabisa mipango yao uwanjani, hivyo kuwapa fursa Etoile kutawala zaidi mchezo.
    Mrisho Khalfan Ngassa aliyekuwa mtengenezaji wa mashambulizi yote ya Yanga SC jana, alimpa pasi nzuri ndani ya boksi Msuva dakika ya 60, lakini akampasia kipa Mathlouthi Aynen mikononi.   
    Kocha Mholanzi, Hans van de Pluijm alifanya mabadiliko akimtoa kiungo Hassan Dilunga katikati ya kipindi cha pili na kumuingiza mshambuliaji Mliberia, Kpah Sherman.
    Dakika ya 87 Tambwe aliukwamisha mpira nyavuni akimalizia pasi ya Ngassa, lakini wakati anataka kuanza kushangilia akakutana na mkono wa refa Samuel Chirindiza wa Msumbiji akimuambia alikuwa ameotea.
    Baada ya tukio hilo, wachezaji wa Etoile wakaanza kujiangusha kupoteza muda.
    Awali ya hapo, dakika ya 85 Yanga ilipata pigo lingine baada ya beki wake wa kulia, Juma Abdul kuumia na kutoka nje akimpisha Rajab Zahir, aliyekwenda kucheza katikati, Mbuyu Twite akihamia pembeni kulia.
    Mchezo wa jana Etoile walicheza kama wao ndiyo waliokuwa wa nyumbani, na Yanga SC waliokuwa ugenini.
    Etoile walikuwa wenye kujiamini, wakicheza bila hofu hata chembe na kuwafanya Yanga SC wacheze kwa ‘woga woga’.
    Haikuwa Yanga SC ile ambayo tumeiona katika mechi za karibuni, Kombe la Shirikisho na Ligi Luu ikitoa vipigo, jana ilikuwa timu tofauti.
    Niwe wazi tu, Yanga SC hawakucheza vizuri jana. Walicheza kwa woga mno. Wachezaji hawakuwa wenye kujiamini kabisa. Yaani kama enzi zile za akina Mohammed Yahya ‘Tostao’ na Charles Boniface Mkwasa, ndiyo walikuwa wanacheza kwa woga namna hii dhidi ya timu za Kaskazini mwa Afrika.
    Tatizo lilikuwa nini? Sijui. Hii si ndiyo Yanga SC ambayo mwaka iliwafunga mabingwa wa kihistoria Afrika, Al Ahly hapa Uwanja wa Taifa?
    Tulikuwa tumeanza kusahau hadithi za Yanga kufungwa tano, sita inapokwenda kucheza Kaskazini mwa Afrika, ila iwapo watarudia kucheza kama walivyocheza jana, katika mchezo wa marudiano watarejea na kapu la magoli hapa nyumbani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KWA MPIRA ULE, YANGA WAKIENDA TUNISIA AIBU! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top