MEI 4, mwaka huu wapenzi wa soka Nigeria na Afrika kwa ujumla
walipokea habari za kusikitisha, kuhusu kifo cha mshambuliaji mahiri zamani
barani, Rashidi Yekini.
Rashidi Yekini alikuwa mshambuliaji hatari kabisa kuwahi
kutokea nchini Nigeria tangu kugunduliwa kwa mchezo wa soka. Alipewa jina la
utani la ‘Ye-King’ kutokana na ufumaniaji wake wa nyavu.
Alikulia mjini Kaduna ambaklo alikuwa ni gumzo kwa mashabiki
wa soka kabla ya kujulikana nchi nzima.
Mwaka 1994, Yekini aliiongoza Super Eagles kutwaa taji la
Mataifa ya Afrika huko Tunisia na kuwa mfungaji bora. Alikuwa tishio kwa mabeki
na makipa wa upinzani waliokuwa wakishindwa kumdhibiti, kutokana na umbo lake
kubwa na mashuti makali.
Baada ya mashindano ya Tunisia mwaka 1994, dunia nzima
ilikuwa na furaha ya kikaribisha timu bora ya Afrika kwenye fainali zake za
mara ya kwanza za Kombe la Dunia zilizofanyika Marekani. Mechi ya kwanza ya
Nigeria ilikuwa dhidi ya Bulgaria kwenye Uwanja wa Cotton Bowl huko Dallas.
Mbele ya mashabiki zaidi ya 40,000, Super Eagles ilifunga
bao la kwanza dakika ya 21 kutokana na shambulizi kali lililotengenezwa na
Yekini ambaye wakati huo alikuwa akichezea Victoria Setubal ya Ureno.
Lilikuwa bao zuri lililotokana na uchezaji wa uhakika kutoka
winga ya kulia alikokuwapo winga wa Ajax Amsterdam ya Uholanzi - Finidi George.
Nyota huyo, Finidi, aliichanganya beki ya Bulgaria na kupiga
krosi bomba iliyomkuta Yekini akiwa kwenye kasi ndani ya mita sita kutoka
langonmi mwa Bulgaria. Hakufanya makosa na kuandika bao la kwanza la Nigeria
kwenye historia ya Kombe la Dunia.
Uwanja mzima ulilipuka kwa shangwe na nusura Yekini azichane
nyavu za Bulgaria kwa furaha kubwa iliyoonekana wazi mwili mzima.
Aina yake ya ushangiliaji iliingia kwenye vitabu vya kumbukumbu.
Mechi hiyo ilimalizika kwa Nigeria kushinda 3-0 na kuizamisha kabisa timu
iliyokuwa ikiongozwa na Hristo Stoichkov. Ni mechi iliyoshuhudia ubora wa soka
la Afrika duniani.
Baada ya kustaafu soka la kimataifa, Yekini alishangaza watu
aliporejea kwenye Ligi Kuu ya Nigeria, na kung’ara akiwa na Julius Berger ya
Lagos msimju wa 2005-2006. Alifunga mabao kadhaa kabla hajatangazaa kustaafu
kikweli kweli na kumuachia umaarufu mkubwa.
Akiwa na Super Eagles alifunga mabao 37 na alijinyakulia
heshima duniani alipopewa tuzo ya uanasoka bora wa mwaka wa Afrika na CAF mwaka
1993.
Wakali wengine wa enzi zake kama Daniel Amokachi, Samson
Siasia, Augustine Eguavoen, Mike Emenalo, Sunday Oliseh na Ben Iroha ama
wameifundisha timu ya taifa au kuajiriwa na Nigeria Football Federation ( NFF)
au klabu za Ulaya, ni tofauti kabisa kwa Rashidi Yekini alikuwa ‘kimya’
alijiweka mbali na umaarufu baada ya soka, akibaki kuwa mchamungu tu
Hakuna aliyekuwa akifahamu nyendo zake, ingawa ni wazi walijua
alikuwa anaishi Ibadan. Aligoma kuzungumza na waandishi wa habari wanaomwinda
mara kwa mara kwa ajili ya mahojiano. Mwandishi aliyejaribu kupanga mahojiano
kwa msaada wa mchezaji mwenzake na Yekini nyumbani kwake, alishangaa pale
mpachika mabao huyo alipogoma kufungua mlango!
Pia Yekini alimuonya rafiki yake aache mara moja kuwapeleka
waandishi wa habari nyumbani kwake. Ni kwa nini Yekini, aliyefunga bao la
kwanza la Nigeria kwenye Kombe la Dunia aliamua kujitenga na jamii?
Aligomea ombi la NFF la kuipeleka pasi yake ya kusafiria ili
atengenezewe visa ya kwenda Afrika Kusini kwenye Fainali za Kombe la Dunia
mwaka juzi. Mabosi hao wa soka walikuwa wamemteua Yekini kuwa Balozi kwenye
Kombe la Dunia 2010 pamoja na kocha wa zamani wa timu ya taifa, Christian
Chukwu, wachezaji wa zamani wa Eagles, Garba Lawal, Amodu Shuaibu na Tijani
Yusuf.
Tangu atundike buti mwaka 2005 baada ya kuzichezea Julius
Berger FC na Gateway FC ya Abeokuta, alikuwa anajali shughuli zake tu. Sababu
kadhaa zilikuwa zikitolewa kuhusu chuki ya Yekini kwa jamii.
Kuna uvumi kuwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Eagles ana
matatizo na wachezaji wenzake wa timu ya taifa. Kulikuwapo na taarifa zisizo
rasmi kuwa kulikuwa na njama za kutompasia mipira nyota huyo wakati wa fainali
za Marekani mwaka 1994.
Inasemekana kuna kundi la wachezaji walichukizwa na jinsi
alivyoshangilia kwa nguvu baada ya kuifunga Bulgaria. Yekini hakufunga bao lingine
kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994. Na kikundi hicho kiliendelea
kumwangusha hata kwenye fainali za 1998 huko Ufaransa.
Huenda pia Yekini hakupenda kukutana na wabaya wake, ambao
baadhi yao walikwenda Afrika Kusini.
Halafu kuna suala la Jenerali Sani Abacha. Baada ya kombe la
mataifa kule Tunisia mwaka 1994, Yekini alikuwa ameweka kimiani mabao 13 na
alikuwa na lengo la kuvunja rekodi ya mabao 14 ya Laurent Pokou wa Ivory Coast.
Ndoto hizo za kutimiza azma hiyo kwenye fainali za Mataifa
ya Afrika nchini Afrika Kusini mwaka 1996 zilichanwa na uamuzi wa Abacha
kuizuia Eagles kushiriki mashindano hayo baada ya kuhitilafiana na Nelson
Mandela. Nigeria ilifungiwa kushiriki fainali za Burkina Faso mwaka 1998.
Mwaka 2000, wakati Nigeria na Ghana zilipoandaa mashindano
hayo, enzi za Yekini zilikuwa zimepita. Samuel Eto Fils wa Cameroun akaivunja
rekodi aliyokuwa akiitamani Yekini.
Insemekana kuwa hadi anafikwa na umauti, Yekini alikuwa akiumizwa
sana na jambo hilo na alikamua kuuguza majeraha hayo kwa kuwa peke yake.
Wachambuzi wengine wa soka wanasema uduni wa elimu aliokuwa nayo Yekini ulimzuia
kujichanganya na wenzake wenye elimu zaidi yake.
Kabla ya kifo chake, alikuwa anaendesha hoteli iitwayo
Liberty Motel, Barabara ya Ring, Ibadan, jimbo la Oyo, japo hakupenda kujichanganya
na watu. Inasemekana hata marafiki zake ni wachache sana kwenye jiji hilo la
zamani.
Naam, huyo ndiye Rashid Yekini, nguli wa soka aliyeiaga
dunia kipweke licha ya umaarufu mkubwa na heshima aliyojijengea- zaidi kutokana
na chuki aliyokuwa nayo dhidi ya wabaya wake, ambayo inadaiwa ilichangia kifo
chake. Mungu aiweke pema poponi roho ya marehemu. Amin.
WASIFU WAKE:
JINA: Rashidi Yekini
KUZALIWA: Oktoba 23, 1963 (Miaka 47)
KUFARIKI DUNIA: Mei 4, 2012
ALIPOFIA: Ibadan
KLABU ALIZOCHEZEA:
Mwaka
Klabu
1981–1982 UNTL
Kaduna
1982–1984
Shooting Stars
1984–1987
Abiola Babes
1987–1990
Africa Sports
1990–1994
Vitória Setúbal
1994–1995
Olympiacos
1995–1996
Sporting Gijón
1997 Vitória
Setúbal
1997–1998 FC
Zürich
1998–1999
Bizerte
1999 Al-Shabab
1999–2002 Africa
Sports
2002–2003 Julius
Berger
2005
Gateway
(Tangu 1986 hadi 1998, aliichezea Nigeria mechi 70,
akaifungia mabao 37)
0 comments:
Post a Comment