![]() |
Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange 'Kaburu' akionyesha alama ya vidole vitano, kuwakejeli wapinzani wao wa jadi, Yanga waliowafunga 5-0 katika Ligi Kuu msimu uliopita |
KIUNGO wa Yanga, Kiggi Makassy amesaini mkataba wa miaka
miwili kujiunga na wapinzani wa jadi, mabingwa wa Tanzania, Simba SC.
Habari za ndani kutoka kutoka Simba, ambazo BIN
ZUBEIRY imezipata kutoka ndani ya Simba, zimesema kwamba, Kiggi ambaye
amechoka mwenyewe na maisha ya Yanga, amekwenda Simba kwa hiari na mapenzi yake.
Kiggi ambaye mjomba wake, Itutu Kiggi ‘Road Master’ aling’ara
Simba mwaka 1991 akiiwezesha timu hiyo kutwaa Klabu Bingwa Afrika Mashariki, msimu
huu haukuwa mzuri kwake Yanga, kutokana na kuwekwa benchi mfululizo.
Kiggi ni mchezaji mzuri, ambaye siku za karibuni Yanga
walishindwa kumtumia vizuri na kuonekana kama ameshuka kisoka, lakini kuna
matumaini makubwa atang’ara Simba.
![]() |
Kiggi Makassy |
Historia inaonyesha wachezaji wengi wanaoondoka Yanga kwenda
Simba, hung’ara - kuanzia enzi za Ezekiel Greyson ‘Jujuman’, Said Mwamba ‘Kizota’
(wote marehemu), Mohamed Hussein ‘Mmachinga’, Mohamed Banka na Amiri Maftah.
Kiggi alijiunga na Yanga mwaka 2008, akitokea Mtibwa Sugar
ya Morogoro, ambayo nayo ilimtoa kituo cha kukuza vipaji cha Rollingston cha
Arusha, kinachomilikiwa na mwanasoka wa zamani wa kimataifa nchini, Ally
Mtumwa.
Tayari Yanga imesajili wachezaji wawili wa Simba, ambao ni kipa Ally Mustafa 'Barthez' na beki Kelvin Yonda, hivyo Simba sasa ni kama inaanza kulipa kisasi.
0 comments:
Post a Comment