• HABARI MPYA

    Thursday, June 07, 2012

    COPA COCA COLA TAIFA JUNI 24 DAR MPAKA PWANI


    MICHUANO ya Copa Coca-Cola ngazi ya Taifa inaanza kutimua vumbi Juni 24 mwaka huu kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani huku pambano la ufunguzi likiwa kati ya Kigoma na Lindi litakalofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
    Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace Wambura Mgoyo ameiambia leo BIN ZUBEIRY kwamba, upangaji ratiba (draw) umefanyika leo (Juni 7 mwaka huu) kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kushuhudiwa na waandishi wa habari, makocha wa timu za mikoa za Copa Coca-Cola na wadhamini kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-Cola.
    Amesema makocha 35 wa timu za Copa Coca-Cola kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani wako kwenye kozi ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) inayoendeshwa na wakufunzi Ulric Mathiot wa FIFA kutoka Seychelles na wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Sunday Kayuni wa Tanzania.
    Amesema mikoa 28 ya kimpira ya Tanzania itashiriki katika mashindano hayo na imegawanywa katika makundi manne ya timu saba saba. Baadaye timu zitapambana katika hatua ya robo fainali, nusu fainali na fainali itakayofanyika Julai 15 mwaka huu.
    Amesema Kundi A lina timu za Arusha, Ilala, Kigoma, Kusini Pemba, Lindi, Rukwa na Ruvuma. Kundi B ni Iringa, Kaskazini Pemba, Manyara, Mjini Magharibi, Morogoro, Mwanza na Tanga. Dodoma, Kaskazini Unguja, Kinondoni, Mara, Mbeya, Mtwara na Temeke ziko kundi C wakati kundi D ni Kagera, Kilimanjaro, Kusini Unguja, Pwani, Shinyanga, Singida na Tabora.
    “Viwanja vitakavyotumika katika mashindano hayo ambapo mechi zitakuwa zikichezwa asubuhi (saa 2.30) na jioni (saa 10.00) ni Uwanja wa Karume na Tanganyika Packers (Kawe) kwa Dar es Salaam. Viwanja vya Mkoa wa Pwani ni Tamco na Nyumbu. Timu zote katika mashindano hayo zitacheza katika viwanja hivyo,”amesema.
    Wambura pia amesema mbali ya Kigoma na Lindi, mechi nyingine za ufunguzi Juni 24 mwaka huu ni kundi B Morogoro na Manyara (saa 2.30 asubuhi Uwanja wa Kawe), kundi C ni Temeke na Kinondoni (saa 2.30 asubuhi Uwanja wa Nyumbu) na kundi D ni Kilimanjaro na Kusini Unguja (saa 2.30 asubuhi Uwanja wa Tamco).
    Amesema wachezaji wanaotakiwa kushiriki kwenye michuano hiyo ya umri chini ya miaka 17 ni wale waliozaliwa kuanzia Januari 1, 1996
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: COPA COCA COLA TAIFA JUNI 24 DAR MPAKA PWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top