• HABARI MPYA

    Tuesday, June 12, 2012

    TENGA ASEMA KIM POULSEN NI MTU WA KAZI, AKITOKA NYUMBANI NI SOKONI, HAJUI KUJIRUSHA


    Rais wa TFF, Leodegar Chillah Tenga kulia, akizungumza na Waandishi wa Habari leo ofisi za shirikisho hilo, Ilala, Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu wake, Angetile Osiah akiandika hadidu za rejea.

    RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chillah Tenga amemwagia sifa kocha wa sasa wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mdenmark Kim Polulsen kwamba ni mtu wa kazi na hajui anasa.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari katika ofisi za TFF, Ilala, Dar es Salaam mchana wa leo, Tenga alisema kwamba Kim akitoka nyumbani kwake amekwenda sokoni au kazini na hajui baa wala sehemu za starehe.
    Tenga amesema wana matumaini makubwa sana na Poulsen kwamba ataifikisha mbali soka ya Tanzania, kwa sababu hata timu yake ya sasa inaundwa na asilimia kubwa ya vijana walio na wastani wa umri wa miaka 23 na kwamba hata wakubwa wachache, rika la akina Juma Kaseja na Haruna Moshi ‘Boban’ wana miaka isiyozidi 27.
    Tenga amempongeza Kim na vijana wake kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Gambia, Jumapili katika mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil na ameomba timu hiyo iungwe mkono zaidi ili ifike mbali.
    “Tumefika hapa baada ya jitihada kubwa, ikiwemo kubadilisha kocha. Kupambana na nidhamu, tulimuambia mwalimu, tafadhali, hakikisha nidhamu, utendaji na jitihada za mazoezi, usiogope mchezaji, ita mchezaji, nampongeza sana na hakuna jambo la ajabu kwa sababu tunamjua Kim, ni mtu wa kazi, mwaka mzima”alisema Tenga.
    Tenga amesema kwamba tangu amewasili Kim Tanzania mwaka jana alianzisha programu nzuri ya vijana ambao amekuwa akiwakusanya kila mwezi na kuwanoa- jambo ambalo limesababisha hivi sasa awe na timu nzuri ya taifa, baada ya kupandishwa kutoka kocha wa timu za vijana, hadi ya wakubwa, akirithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Poulsen.
    “Wale vijana Sure Boy (Salum Abubakar) na Damayo (Frank) wamecheza pamoja karibu mwaka mzima timu ya vijana chini ya Kim na wanaelewana sana. Sasa tumekwishaanza kuandaa utaratibu wa kuwapatia vijana wataalamu wa saikolojia, ili wawafundishe mambo, namna ya kuzungumza na Waandishi wa Habari, kuweza kujiami na kadhalika.
    “Na tumeboresha maslahi yao, wakishinda mechi wanapata asilimia 15 ya mapato, wakitoa sare asilimia tano, ila wakifungwa hawapati kitu. Tutawakatia bima pia, mambo yatakuwa mazuri,”alisema Tenga.
    Taifa Stars hivi sasa inashika nafasi ya pili katika Kundi C, kwa pointi zake tatu, mabao mawili ya kufunga na matatu ya kufungwa, nyuma Ivory Coast inayoongoza kwa pointi zake nne, mabao manne ya kufunga na mawili ya kufungwa, wakati Morocco inashika nafasi ya tatu kwa pointi zake mbili, mabao matatu ya kufunga na matatu ya kufungwa na Gambia yenye pointi moja, mabao mawili ya kufunga na matatu ya kufungwa inashika mkia.
    Stars Jumapili itahamishia mawindo yake katika kinyang’anyiro cha tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani Afrika Kusini kwa kumenyana na Msumbiji mjini Maputo na inatarajiwa kuondoka nchini Ijumaa. Katika mchezo wa kwanza, timu hizo zilitoka sare ya 1-1 Dar es Salaam na Stars inatakiwa lazima kushinda ugenini ili kuitoa Mambas na kusonga mbele. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TENGA ASEMA KIM POULSEN NI MTU WA KAZI, AKITOKA NYUMBANI NI SOKONI, HAJUI KUJIRUSHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top