• HABARI MPYA

    Tuesday, June 12, 2012

    TRESURE KANU MBIYAVANGA, INJINI MPYA SIMBA SC BALAA


    Tresure Kanu Mbiyavanga
    DORIS MALIYAGA 
    SIMBA imekamilisha malengo waliyokusudia muda mrefu mara tu baada ya kumnasa kiungo wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Tresure Kanu Mbiyavanga kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.
    Mabingwa hao wa Ligi Kuu walikuwa na lengo hilo tangu msimu wa mwaka jana baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Moses Basena raia wa Uganda kuvutiwa naye katika mechi Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Motema Pembe.
    Simba ilicheza mchezo huo baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya 16 bora na Wydad Casablanca ya Morocco na Basena kumtamkia Mbiyavanga anataka kumsajili, ahadi ambayo sasa imekamilishwa, licha ya kutokuwepo kwa kocha huyo ambaye alitimuliwa mapema msimu uliopita.
    Katika mchezo huo, Mbiyavanga ambaye ana umbo la wastani, lakini limejengeka kwa mazoezi, alicheza kiungo safi na kuisumbua ngome ya Simba kwa kutoa pasi safi na mipira ya mashuti. Anakumbukwa kwa utambulisho wa nywele zake alizokuwa amepaka rangi nyeupe.
    Kutokana na hilo, Mwanaspoti ilifanya naye mahojiano ya kina kufahamu malengo yake na Simba pamoja na historia yake kwa ujumla.

    Sababu ya kujiunga na Simba Mbiyavanga anasema amejiunga na Simba baada ya kugundua mipango yao ya soka ni mizuri, lakini pia maslahi yamechangia.
    "Nimejiunga Simba kwa sababu ya mipango yao, mimi ni mchezaji naangalia panaponifaa katika mafanikio yangu,"anasema Mbiyavanga ambaye anaishabikia klabu ya Chelsea ya England.
    "Viongozi wa Simba na mimi tumekubaliana mambo mengi na ndiyo sababu ya kuondoka Motema Pembe na kuja Tanzania kucheza mpira,"anaeleza Mbiyavanga ambaye pia anawafagilia viungo; Mikel Obi na Michael Essien na anataka kufuata nyayo zao.
    "Mimi ni mchezaji na mpira ndiyo kazi yangu niliangalia maslahi, Simba tumekubalina pesa nyigi zaidi ya nilizokuwa napata Motema Pembe.
    "Lakini pia wana mpango mzuri katika maendeleo ya soka lao, nimeona katika michuano ya kimataifa na mimi ndiyo ninapenda."

    Malengo yake Mbiyavanga ambaye tayari ameshacheza soka la ushindani katika nchi tofauti kama Congo, Afrika Kusini, Rwanda, Gabon na Angola amesema, malengo yake ni kuipa mafanikio Simba kupitia uzoefu wake.
    "Malengo ni kuhakikisha naipa mafanikio Simba ili ifanye vizuri katika michuano ya kimataifa na Ligi Kuu Bara," anasema Mbiyavanga aliyeungana na Emmanuel Okwi raia wa Uganda, Felix Sunzu na Mussa Mudde.
    Anasema soka yake kwa mashabiki wa Tanzania si mgeni kwao kwa sababu walimshuhudia alipokuwa na Motema Pembe: "Naamini mimi si mgeni kwa mashabiki wa hapa, sina cha kuongea sana wao wasubiri kazi yangu uwanjani nami ninawaahidi sitawaangusha.
    Ameongeza kuwa, furaha yake itakamilika pale Simba itakapofanikiwa kutwaa Ubingwa wa Kombe la Kagame msimu huu na yeye akichangia mafanikio hayo.

    Alicheza na Mafisango kikosi kimoja Mbiyavanga aliumia alipokuwa akimhadithia, marehemu Patrick Mafisango ambaye ni Mcongo mwenzake aliyekuwa akiichezea Simba, lakini alifariki kwa ajali ya gari mwezi uliopita.
    "Sipendi kumzungumzia Patrick kwa sasa, lakini ndiyo imetokea mipango ya Mungu,"anaeleza kwa masikitiko. "Namfahamu Patrick tangu tukiwa wadogo nikicheza naye kikosi kimoja katika timu za vijana, tulikuwa wote viungo na tulisaidiana sana, ninapocheza mbele namba nane na yeye anacheza nyuma namba sita tunapishana.
    Sijui ingekuwaje kama tungekutana tena hapa Simba, lakini ni kama nilivyosema ni mipango ya Mungu, tuyaache kama yalivyo,"anaeleza.

    Majina yake Mbiyavanga amefafanua ukweli halisi wa majina yake kuwa ni Tresure Kanu Mbiyavanga, licha ya kuwa anatambulika kama Patrick Kanu Mbiyavanga katika wasifu wake kwenye mitandao na watu wanavyomjua hivyo.
    "Majina yangu ni Tresure Kanu Mbiyavanga ndiyo sahihi, hilo la Patrick ni kutokana na mashabiki, walinipa nikiwa mdogo wakifananisha na Patrick Viera (mchezaji wa zamani wa Arsenal ya Uingereza sasa yupo benchi la Manchester City),"anaeleza Mbiyavanga.

    Nje ya soka Mbiyavanga anasema akiwa nje ya soka anapomaliza majukumu ya mechi, anapenda kutulia nyumbani na familia yake.
    "Ninapomaliza mechi au kipindi cha mapumziko, napenda kutulia nyumbani na kucheza na familia yangu huku tukiangalia filamu na kusikiliza muziki,"anasema Mbiyavanga.
    Amesema yeye ni mtu wa sala, hutumia pia muda huo wa pamoja kufanya maombi.

    Historia yake Mbiyavanga ni wa kwanza katika familia yake yenye watoto nane, wadogo zake ni pamoja na Ilee, Erick, Milet, Shimen, Meryvey, Ritha na Atara.
    Yeye ni baba wa watoto wawili, wa kike ni Dayana (4) na wa kiume ni Tirsiana (1) aliowapata kwa mke wake mpendwa aliyemtaja kwa jina la Mam Kanu.
    Familia yake; mke na dada yake, Shimen pamoja na watoto wote wanaishi jijini Dar es Salaam.

    TRESURE KANU MBIYAVANGA Kuzaliwa: Machi 15, 1989,
    Mahali : Kinshasa, Congo.
    Klabu: Inter Luanda Club 2006-2008,
    APR 2008-2009,
    Mangasport 2009-2011
    Motema Pembe 2011-2012
    Simba 2012-
    Taifa: DR Congo



    SOURCE: GAZETI LA MWANASPOTI
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TRESURE KANU MBIYAVANGA, INJINI MPYA SIMBA SC BALAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top