• HABARI MPYA

    Tuesday, November 20, 2012

    FRIENDS OF SIMBA WAKUTANA KUJADILI MAMBO KLABUNI

    Hans Poppe

    Na Mahmoud Zubeiry
    KUNDI la Friends of Simba (F.O.S.) linatarajiwa kukutana kesho jioni kujadili mustakabali wa klabu kwa ujumla na kutoa msimamo wao mbele ya wanachama na wapenzi wa klabu hiyo.
    Hamkani si shwari Simba kwa sasa baada ya timu kumaliza nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ikitoka kuongoza kwa wastani wa pointi saba.
    Mwenyekiti wa F.O.S., Zacharia Hans Poppe ameiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, watakuwa na Mkutano kesho kujadili hali ya mambo klabuni kwao.
    “Sisi kazi yetu ni kusapoti uongozi uliopo madarakani, kuhakikisha timu yetu inafanya vizuri, sasa hali inayoendelea sasa inatutia shaka kuelekea mwakani, ambako tutakuwa na mtihani wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na pia Ligi ya Mabingwa.
    Kwa hivyo tutakutana, tutazungumza kwa mapana marefu sana, ili tujue undani na ukweli wa matatizo yaliyopo klabuni na baada ya hapo na sisi tutatoa mtazamo wetu,”alisema kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
    Baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Kamati ya Utendaji ya Simba, chini ya Mwenyekiti wake, Alhaj Ismail Aden Rage ilikutana na kufikia maamuzi ya kuvunja Kamati zote ndogondogo za klabu pamoja na kulifuta tawi la wanachama wakorofi, Mpira Pesa la Magomeni, waliomtukana kipa Juma Kaseja na kuendesha harakati za mapinduzi.  
    Lakini pia wasiwasi umeingia kutokana na kuvunjwa pia kwa Kamati ya Usajili, iliyokuwa chini ya Mwenyekiti Hans Poppe katika kipindi hiki kigumu ambacho klabu inatakiwa kurekebisha usajili kuelekea mzunguko wa pili na Ligi ya Mabingwa.
    Mbali na hivyo, kuna suala la mchezaji Emanuel Okwi ambaye amemaliza mkataba wake kwenye klabu hiyo na alikuwa kwenye majadiliano na Kamati ya Usajili, ambayo yalifikia pazuri, lakini kwa kuvunjwa kwa Kamati hizo, maana yake mazungumzo hayo hayawezi kuendelea.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: FRIENDS OF SIMBA WAKUTANA KUJADILI MAMBO KLABUNI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top