• HABARI MPYA

    Friday, November 09, 2012

    TOTO WAPO KAMA HAWAPO, WAMEJICHIMBIA TANDIKA TAYARI KUUA MNYAMA KESHO

    Toto African

    Na Mahmoud Zubeiry
    TIMU ya Toto African imejichimbia eneo la Tandika mjini Dar es Salaam kwa takriban wiki nzima, ikijifua vikali tayari kwa mchezo wao dhidi ya Simba kesho.
    Kocha wa Toto, John Tegete aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, yeye hatakuja Dar es Salaam kuungana na timu yake kwa ajili ya mechi hiyo kwa sababu ya majukumu ya kitaifa, lakini kikosi kipo vizuri.
    “Mimi nina majukumu ya maandalizi ya mchezo wa kirafiki wa Taifa Stars na Kenya huku Mwanza, ila kila kitu kipo sawa, timu iko huko, imeweka kambi Tandika na Jumamosi Mnyama anachinjwa Uwanja wa Taifa,”alisema Tegete.
    Tegete alisema Toto wafufuliwe kwa kaburini, kwa Simba watacheza mechi na kushinda kwa sababu wanaamini hao ni vibonde wao tu.
    “Na ndiyo maana sina wasiwasi nimebaki Mwanza najua tu vijana wangu watachinja Mnyama,”alisema.  
    Toto imekuwa na rekodi ya kuisumbua Simba katika Ligi Kuu hata ikiwa vibaya na hilo ndilo linatarajiwa kwenye mchezo wa kesho Uwanja wa Taifa.
    Awali, Simba ilitishia kugoma kucheza mechi hiyo kesho, siku tofauti na wapinzani wao wa jadi, Yanga SC.
    Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mapema wiki hii limetangaza kuzirudisha nyuma kwa siku moja mechi zote za mwisho za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, kutoka Jumapili wiki hii hadi Jumamosi, kasoro mechi ya Yanga na Coastal Union pekee, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
    Na sababu za kutorudishwa nyuma kwa mechi ya Yanga ni kwa kuwa Jumamosi kutakuwa na mchezo mwingine wa ligi hiyo, Uwanja wa Mkwakwani, kati ya Mgambo JKT na Azam FC.
    Lakini Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga aliiambia BIN ZUBEIRY juzi kwamba hawako tayari kucheza siku tofauti na Yanga kwa sababu ya upinzani uliopo baina yao katika mbio za ubingwa, kwani wanahofia mchezo mchafu.
    “Unajua bwana ligi hii ilipofikia ni pabaya, haiwezekani uzichezeshe Simba na Yanga siku tofauti, hivyo sisi tunawaandikia barua TFF kuwataarifu kwamba hatuko tayari kwa mabadiliko hayo,”alisema Kamwaga.
    Lakini inavyoonekana Wekundu hao wa Msimbazi wamefyata mkia na kesho wataingiza timu Taifa.
    Mechi nyingine za Jumamosi ni Mgambo JKT na Azam FC Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, African Lyon na Mtibwa Sugar Chamazi, Dar es Salaam, Prisons na JKT Ruvu Sokoine, Mbeya, Kagera Sugar na Polisi Morogoro, Kaitaba, Bukoba na JKT Oljoro na Ruvu Shooting Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: TOTO WAPO KAMA HAWAPO, WAMEJICHIMBIA TANDIKA TAYARI KUUA MNYAMA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top