• HABARI MPYA

    Tuesday, November 13, 2012

    WAGENI LIGI KUU, NANI WA UKWELI NANI FEKI?

    Didier Kavumbangu wa Yanga aliyeruka kama mkizi kushoto, mchezaji wa kigeni aliyeoongoza kwa mabao Ligi Kuu Bara baada ya mzunguko wa kwanza

    Na Mahmoud Zubeiry
    KAMA ilivyo nchi nyingi duniani, Tanzania pia katika Ligi Kuu yake kuna wachezaji wa kigeni na haijaanza leo, bali tangu miaka ya 1970, ingawa katika siku za karibuni, idadi ya wageni imekuwa ikiongezeka katika ligi hiyo. Awali, mgeni alipatikana katika klabu mbili kongwe pekee, Simba na Yanga lakini sasa hata klabu nyingine za mikoani pia nazo zina wachezaji wa kigeni. Lakini vipi kuhusu michango yao katika klabu zao na mustakabali wao mzima baada ya mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo? BIN ZUBEIRY inakupa jibu. Endelea.

    Yaw Berko
    YAW BERKO (Yanga SC, Ghana):
    Kuna dalili za kutosha huu ukawa msimu wake wa mwisho Yanga, kutokana na uhusuiano wake na viongozi wa klabu hiyo kuzidi kuharibika. Yaw Berko pamoja na umahiri wake langoni, kipa huyu kutoka Ghana anadaiwa anaringa na pia anatuhumiwa wakati mwingine eti anahujumu timu. Msimu uliopita aliletewa Shaaban Kado lakini akashindwa kumuondoa langoni, ila msimu huu Ally Mustafa ‘Barthez’ anaonekana kufanya vizuri, hivyo kumtengenezea Berko mazingira ya kupewa mkono wa kwaheri Yanga. Amecheza mechi kadhaa za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwemo dhidi ya watani wa jadi, Simba, lakini Barthez amecheza zaidi.

    Felix Sunzu
    FELIX SUNZU (Simba SC, Zambia):
    Ameendelea kuwa mshambuliaji tegemeo katika klabu ya Simba, licha ya kusajiliwa kwa washambuliaji wapya akina Daniel Akuffo kutoka Ghana na Abdallah Juma. Mchezaji huyu mrefu kutoka Zambia ambaye ndiye analipwa mshahara mkubwa zaidi Tanzania, Sh. Milioni 5, amekuwa akiisaidia mno timu yake kutokana na kucheza kwa kujituma hata kwenye mechi ngumu. Kwa kiwango chake katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Sunzu bado anastahili kuendelea kupiga kazi Simba na hata mshahara wake anaolipwa anautumikia vizuri.

    Kipre Balou
    KIPRE BALOU (Azam FC, Ivory Coast):
    Msimu huu anafanya kazi, tofauti sana na msimu uliopita ambao ulikuwa wa kwanza kwake nchini. Hadi mzunguko wa kwanza unamalizika, Kipre Michael Balou amekuwa ana wastani mzuri wa kucheza kuanzia chini ya kocha Mserbia, Boris Bunjak na hata kwa Muingereza, Stewart Hall. Baada ya Azam kuwasimamisha wachezaji wake wanne wa safu ya ulinzi, kipa Deo Munishi ‘Dida’, mabeki Erasto Nyoni, Said Mourad na Aggrey Morris, katika mechi ya mwisho ya mzunguko wa kwanza, Balou alicheza beki ya kulia na akafanya kazi yake vizuri tu pamoja na kufungwa mabao 2-1 na Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

    Mbuyu Twite
    MBUYU TWITE (Yanga SC, Rwanda):
    Yanga imelamba dume hapa, hakuna shaka kabisa kusema hivyo. Beki huyo wa kimataifa wa Rwanda, aliyesajiliwa kutoka APR ya Rwanda, amecheza vema mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kiasi cha kujikusanyia mashabiki wengi. Amekuwa akitumika kama beki wa pembeni, lakini alionyesha ubora wake zaidi, wakati ambao Kevin Yondan alikuwa anaumwa naye akaanza kutumika kama beki wa kati. Na katika mechi hizo, ambazo Yanga ilicheza bila Yondan, Twite akicheza katikati na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, uimara wa ukuta wa timu hiyo ulioneikana kuongezeka. Twite mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ni kifaa na si katika ulinzi tu, bali ameweza pia kufunga mabao matatu hadi mwisho wa mzunguko wa kwanza.











    EMANUEL OKWI (Simba SC, Uganda):
    Emanuel Okwi
    Hii mashine, acha masikhara. Mganda huyu ambaye amemaliza mkataba na Simba SC na hivi sasa yupo katika majadiliano ya kuongeza mkataba, ameendelea kufanya kazi yake vizuri. Akitumiwa kama mshambuliaji wa pembeni, Okwi ameendelea kutengeneza nafasi na kufunga yeye mwenyewe pia. Amefunga mabao ya kusisimua katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, mfano lile lililokuwa la tatu katika mechi dhidi ya Azam. Ni mchezaji ambaye Simba ikishindwa kumshawishi kuongeza mkataba na akaenda kwa hasimu yeyote, Simba watakuwa wamefanya kosa kama ambalo Arsene Wenger alifanya Arsenal, kwa kumruhusu Robin Van Persie aende Manchester United. Watajilaumu.

    Joseph Owino
    JOSEPH OWINO (Azam FC, Uganda):
    Mustakabali wake sasa haujulikani katika klabu ya Azam, baada ya kujikuta anaendelea kukaa benchi kwa makocha wote waliofundisha timu hiyo hadi mwisho wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu. Hakuwa mwenye umuhimu mbele ya Boris Bunjak na watu wakadhani Msrebia huyo alikuwa anakosea, lakini mbele ya Muingereza, Stewart Hall mambo ndiyo yamezidi kuwa magumu kwa beki huyu wa zamani wa Simba SC. Fikiria, baada ya Azam kuwasimamisha wachezaji wake wanne wa safu ya ulinzi, kipa Deo Munishi ‘Dida’, mabeki Erasto Nyoni, Said Mourad na Aggrey Morris, katika mechi ya mwisho ya mzunguko wa kwanza, mshambuliaji Kipre Balou alichezeshwa beki ya kulia wakati Owino yupo na angeweza kucheza katikati, Samir Hajji  Nuhu akacheza pembeni. Nini kinafuata kwa Owino Azam?





    HARUNA NIYONZIMA (Yanga SC, Rwanda):
    Haruna Niyonzima
    Mwanasoka bora zamani Afrika, Abedi Ayew Pele kutoka Ghana amemvulia kofia kiungo huyu wa Rwanda na kushangaa anafanya nini Afrika. Pele alimuona Haruna katika dakika 90 tu za mechi moja dhidi ya Azam FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Nomvemba 4, mwaka huu Yanga ikishinda 2-0.  Hicho ni kielelezo tosha kwamba Haruna ni mchezaji bora na Yanga ina kila sababu ya kujivunia kikungo huyu, ambaye anaingia msimu wa pili katika klabu hiyo tangu asajiliwe kutoka APR ya Rwanda. Yanga wana bahati sana kuwa na mchezaji huyu, ambaye amewahi kufanya majaribio na kufuzu Ujerumani, lakini mizengwe ya klabu yake ya zamani, APR ikamkwamisha kucheza huko.

    Paschal Ochieng
    PASCHAL OCHIENG (Simba SC, Kenya):
    Beki huyu wa zamani wa Yanga, hadi sasa mambo hayamuendei vizuri Simba SC na lolote linaweza kutokea juu yake kuelekea mzunguko wa pili. Anaweza akarudi, au asirudi. Aseme na Mungu wake, maana kwa hali iliyopo Simba, hawana muda wa kumvumilia mchezaji na hilo ndilo linalomnyima usingizi beki huyu Mkenya kwa sasa. Amekuja Simba wakati mbaya, unaweza kusema hivyo, lakini Ochieng si beki mbaya akama angeikuta timu hiyo imetulia. Ushahidi wa hilo, Juma Said Nyosso naye msimu huu ameonekana anafaa kuchezea Simba B, sasa utasemaje kwa Ochieng?


























    Kipre Tcheche
    KIPRE TCHECHE (Azam FC, Ivory Coast):
    Kijana safari hii ameonyesha yeye ni nani, hadi mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu unafikia tamati yeye ndiye mfungaji bora wa mabao wa Azam, akipokea nafasi ya John Bocco ‘Adebayor’, ambaye maumivu yamempunguza kasi msimu huu. Kama kuna kitu Kipre Herman Tcheche alikuwa anajifunza msimu uliopita, basi ameweza na msimu huu anatenda inavyotakiwa. Kama Azam walikuwa wana wasiwasi na uwezo wake, bila shaka mechi 13 za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu zimewapa jibu, kwamba hawakukosea kumsajili mchezaji huyu kutoka Ivory Coast. 

    Hamisi Kiiza
    HAMISI KIIZA (Yanga SC, Uganda):
    Aliuanza vibaya msimu huu na hiyo ilitokana na ubinafsi uliotaka kuanza kuitafuna Yanga, kabla ya viongozi kuushitukia na kupambana nao. Kiiza alikuwa kama anatengwa na wenzake, hapewi pasi hata akiwa anatazama na nyavu. Uongozi ukaligundua hilo na ukawakaripia wachezaji mno, hatimaye baada ya hapo, ufedhuli huo ukatoweka na Yanga ikawa kitu kimoja, dhamira moja na hapo ndipo Hamisi Kiiza alipowaonyesha wana Yanga ni kwa sababu gani Uganda walimuita Diego Milito. Alifunga mabao katika mechi mbili muhimu za ukingoni mwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, dhidi ya Azam na dhidi ya Coastal na baada ya hapo amerejesha heshima.   

    Komabil Keita
    KOMANBIL KEITA (Simba SC, Mali):
    Amecheza mechi moja tu ya mwisho, dhidi ya Toto African katika Ligi Kuu tangu alipocheza siku Simba ikitandikwa 3-0 na Sofapaka ya Kenya katika mchezo wa kirafiki. Ukitazama uchezaji wake katika mechi hiyo, akicheza pamoja na Shomari Kapombe haukuwa mbaya, ila tu wachezaji wa uwezo kama wa kwake ni wengi tu hapa nchini. Obadia Mungusa anaweza kuwa bora kuliko Keita. Huwezi kuiona tofauti ya Victor Costa na Keita. Kwa kweli mustabali wa mchezaji huyu kutoka Mali ndani ya Simba  ni mgumu, ana asilimia kubwa ya kutorudi mzunguko wa pili. 

    Ibrahim Shikanda
    IBRAHIM SHIKANDA (Azam FC, Kenya):
    Ameendelea kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza cha Azam mbele ya makocha wote, Boris Bunjak aliyeondolewa na hata Muingereza Stewart Hall aliyerejeshwa kurithi mikoba ya Mserbia huyo. Ingawa Tanzania hivi sasa hatuna tatizo sana na mabeki wa pembeni, lakini kwa sababu Mkenya huyu amekuwa mchezaji wa Azam kwa takriban misimu mitatu sasa, si vibaya akiendelea na maisha katika klabu hiyo. Ni mzuri, lakini wapo wazalendo wazuri kama au kuliko yeye, na hata Azam wakiamua kuachana naye iwapo watapata mbadala wake wa uhakika, haitashangaza.

    Didier Kavumbangu
    DIDIER KAVUMBANGU (Yanga SC, Burundi):
    Yanga msimu huu wanastahili pongezi katika uundaji wa timu yao kwa ujumla, nadhani wamejifunza kutokana na madudu ambayo wamekuwa wakiyafanya miaka ya karibuni. Hapana shaka huyu ni mchezaji mwingine wa maana sana ndani ya kikosi cha Yanga katika wachezaji wa kigeni, baada ya Kiiza, Niyonzima na Mbuyu Twite. Jamaa ameonyesha uwezo mkubwa mno katika kuwapa ‘karaha’ mabeki na makipa. Ni mpambanaji. Shujaa. Jasiri. Ana uwezo wa kumiliki mpira, kuuficha, kasi na kwa ujumla unaweza kusema Kavu anajua. Amemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, akiwa anaongoza kwa mabao na wengi wamemkubali.  

    DANIEL AKUFFO (Simba SC, Ghana):
    Ana asilimia chache mno za kurejea kwenye kikosi cha Simba Januari, kwani mtu wa kwanza ambaye hamkubali kabisa mshambuliaji huyo kutoka Ghana ni kocha, Profesa Milovan Cirkovick kutoka Serbia. Cirkovick amesema amekwishampa nafasi ya Dani, lakini ameshindwa kudhihirisha uwezo wake na sasa hamtaki tena kwenye kikosi chake. Lakini ingekuwa vema kama Simba wangempa nafasi zaidi mshambuliaji huyo kwa kumrudisha Januari ili acheze kwa miezi mingine mitano ili kuona zaidi juu yake. Labda amechelewa kuendana na mazingira na soka ya Tanzania kwa ujumla. Labda. Labda kweli uwezo wake mdogo, labda!

    Suleiman Jingo
    MOHAMED SULEIMAN JINGO (Toto Africans, Uganda):
    Kwa sababu wengi macho yetu yapo Simba, Yanga na Azam tunashindwa kujua kwamba kuna klabu nyingine zina wachezaji wazuri tu wa kigeni zimesajili, mojawapo ni Toto Africans ya Mwanza, ambayo ina winga mmoja matata kutoka Uganda, anaitwa Mohamed Suleiman Jingo. Jamaa mmoja mfupi, ambaye amesajiliwa kutoka Express ‘Red Eagles’ ya Uganda msimu huu. Kwa Toto, wakiendelea kuishi vizuri na mchezaji huyo, kuna uwezekano mkubwa baadaye wakamuuza Azam, Simba au Yanga kwa bei nzuri tu.

    WILLFRED OJODALE AMMEH (Kagera Sugar, Nigeria):
    Jina lake kamili ni Wilfred Ojodale Ammeh, mshambuliaji aliyesajiliwa kutoka Abuja Stars ya Nigeria katika klabu ya Kagera Sugar ya Bukoba mkoani Kagera. Mara nyingi huwa anacheza kama mshambuliaji wa pembeni kushoto na amekuwa mchezaji wa kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Kagera. Miongoni mwa makocha ambao wana uwezo wa kuwajua wachezaji wazuri nchini, ni Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ wa Kagera, hivyo kitendo cha kumpa namba ya kudumu kwenye kikosi chake Mnigeria huyu, maana yake kweli anajua.

    Benjamin Effe
    BENJAMIN EFFE OFUYAH (Kagera Sugar, Nigeria):
    Bonge la beki, akili, maarifa, mbinu, ufundi, nguvu na kujituma unavipata kwake. Kama Simba wangemuona Effe kabla ya kuwasajili Keita na Ochieng, bila shaka wangepambana na Kagera Sugar kugombea saini ya mchezaji huyu. Lakini bahati mbaya hawakumuona. Wachezaji wa Yanga walimsifia sana beki huyu baada ya mechi yao na Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba na baadaye mashabiki wa Dar es Salaam wakajionea uwezo wake, siku timu hiyo ilipomenyana na Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Jamaa alicheza soka nzuri sana na alivutia. Haikushangaza baada ya mechi hiyo, ikaibuka minongo’no kwamba Simba, Yanga na Azam zote zimevutiwa na kijana huyo.









    Hannington Kalyesebula
    HANNINGTON KALYSEBULA BOSA (Kagera Sugar, Uganda):
    Amekuwa kipa wa kwanza wa Kagera Sugar hadi msimu uliopita, lakini mambo yamembadilikia msimu huu amejikuta akisubiri mbele ya Andrew Ntala. Kipa huyu kutoka Uganda, ni mzuri na hata msimu uliopita alipambana na upinzani wa Amani Simba, ingawa baadaye akaushinda, sasa haijulikani kama safari hii Ntala amekuja kumuondoa moja kwa moja, au naye atachemsha kama Amani. Ana nafasi ya kurejea kwenye kikosi cha Kagera Sugar Januari mwakani na hapo ndipo atakapopata fursa ya kujinusuru kutupiwa virago kwa Wakata Miwa hao wa Misenyi.

    ENYINNA DARLINGTON ARIWODO (Kagera Sugar, Nigeria):
    Ni mchezaji wa kikosi cha kwanza cha Kagera Sugar ambaye anafunga na kutengeneza nafasi za wenzake kufunga. Mnigeria huyu aliyesajiliwa kutoka Toto Africans msimu huu, ni mzuri na kwa timu anayochezea si vibaya akaendelea kuwapa changamoto wachezaji wazalendo. Ila tu, Obinna anahitaji kuongeza juhudi na si kubweteka, kwani akiwa mchezaji ambaye anaiingiza gharama za ziada kwa klabu, kwamba mbali na mshahara analipiwa kibali cha kufanya kazi pia, anatakiwa afanye kazi kweli.

    Da Silva na mkewe na mwanawe
    DEANGELIS GABRIEL DA SILVA (Coastal Union, Brazil):
    Coastal Union walimsajili kiungo huyu kutoka Nepal, nchi ambayo Mtanzania Castory Mumbara amewahi kucheza. Mchezaji huyo aliomba nafasi ya kusajiliwa Coastal kupitia ukurasa wa Facebook wa timu hiyo. Alituma DVD zake ambazo viongozi walipoziona wakaridhika naye na kumsajili. Hata hivyo alichelewa kuja na alipotua kocha Hemed Morocco akagundua kiungo huyo Mbrazil anahitaji muda zaidi wa mazoezi kabla ya kuanza kucheza, hivyo akampa programu ya kufanya mazoezi na kikosi cha pili cha Wana Mangushi. Tusubiri mzunguko wa pili itakuwaje juu yake.  

    Philip Kaira
    PHILIP METUSELA MUGENZI (Coastal Union, Uganda):
    Amewahi kucheza URA ya Uganda pamoja na Joseph Owino, ni beki mzuri tu na wakati fulani hata Simba na Yanga walimtaka. Lakini ameshindwa kumshawishi kocha hata mmoja wa Coastal Union kumpa nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Wagosi wa Kaya. Juma Mgunda akiwa anasaidiwa na Habib Kondo, walikuwa wanampiga mkeka beki huyo Mganda na hata sasa Hemed Morocco akiwa anasaidiwa na Ally Kiddy wanamuweka benchi mchezaji huyo. Nini mustakbali wake ikiwa makocha wote wanaoletwa katika timu hiyo wanamchunia? Tutajua Januari.

    OBINNA ONYIEKECHI SALAMASUSA (African Lyon, Nigeria):
    Mmiliki wa African Lyon, Rahim Kangezi ‘Zamunda’ anasema Mnigeria huyu ni mchezaji mzuri, lakini hajitambui hivyo anaweza kuachana naye mzunguko wa pili. Inawezakana, kwa sababu kulingana na mikakati mipya ya Lyon, wanataka kufanya usajili wa kufa mtu, ikiwemo wa wachezaji wa kigeni. Katika orodha ya wachezaji wanaowataka, wapo Mbuyu Twite wa Yanga, Emmnauel Okwi na Mrisho Ngassa wa Simba, ambao Zamunda amesema usajili wao kwa pamoja watatu hao wote utagharimu dola 200,000 za Kimarekani. Kwa hivyo unaweza kusema Obinna anachungulia mlango wa kutokea Lon.

    Hood Mayanja
    HOOD ABDUL SEEWA MAYANJA (African Lyon, Uganda):
    Huyu jamaa anatekeleza wajibu wake vizuri African Lyon na mabao yake kwa sasa ndiyo ambayo yanaibeba timu hiyo. Kwa kukumbushia tu, mchezaji huyu kutoka Uganda amewahi kufanya majaribio Yanga, chini ya kocha Mserbia, Kostadin Papic, lakini pamoja na kuvutia, idadi ndogo ya kikanuni ya wachezaji wa kigeni katika Ligi Kuu ikamsukumia  nje ya kikosi cha Wana Jangwani. Akaenda Mtibwa Sugar ya Morogoro na tangu msimu uliopita yupo African Lyon ambako anaendelea vizuri.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: WAGENI LIGI KUU, NANI WA UKWELI NANI FEKI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top