• HABARI MPYA

    Monday, January 07, 2013

    SIMBA A YAJITOA KOMBE LA MAPINDUZI LICHA YA KUTINGA NUSU FAINALI

    Kikosi cha Simba kilichotinga Nusu Fainali jana

    Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
    PAMOJA na kufuzu hatua ya Nusu Fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi jana, Simba SC italazimika kuiachia timu yao ya pili, maarufu kama Simba B iendelee na michuano hiyo hata kama ikiingia fainali, ili kikosi cha kwanza kiende Oman keshokutwa.
    Kocha Mkuu wa Simba SC, Mfaransa Patrick Liewig aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, anataka kwenda Oman na kikosi kamili ili aweze kuwajua wachezaji wote na kuweza kuipanga vyema timu yake.
    Kuhusu wachezaji wa timu ya taifa, ambayo Januari 11 itacheza mchezo wa kirafiki na Ethiopia, Liewig alisema suala hilo linashughulikiwa na viongozi wa klabu hiyo. “Najua viongozi walikuwa wana kikao na viongozi wa shirikisho (TFF).
    Sijui wamekubaliana vipi, lakini naweza kuwavumilia wachezaji hao wajiunge na timu Oman baada ya mechi na Ethiopia,”alisema.
    Simba jana ilifuzu Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi, licha ya kutoka sare ya 1-1 na Bandari ya hapa katika mchezo wa mwisho wa Kundi A, kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
    Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Bandari wakitangulia kupata bao kwa penalti, mfungaji Haitham Juma dakika ya sita kabla ya Kiggi Makassy kuisawazishia Simba SC dakika ya 16.
    Refa aliwapa penalti Bandari baada ya Haruna Shamte kumchezea rafu Fauzi Ally katika eneo la hatari na Haitham akaenda kupiga penalti, ambayo ilipanguliwa na kipa Dhaira na mpira kumkuta tena mpigaji, aliyeukwamisha nyavuni.
    Kiggi alifunga kwa mpira wa adhabu kutoka upande wa kulia wa Uwanja, umbali wa mita 20, baada ya Abdallah Seseme kuangushwa.    
    Kipindi cha pili, Simba walianza kwa kuimarisha kwa kikosi chao wakiwaingiza kwa mpigo, Mwinyi Kazimoto, Haruna Chanongo na Jonas Mkude kuchukua nafasi za Mussa Mude, Salim Kinje na Ramadhani Singano ‘Messi’, wakati Bandari walimtoa kipa wao Hassan Hajji na kumuingiza Ahmad Suleiman.
    Kwa matokeo hayo, Simba SC imeungana na Tusker ya Kenya kufuzu Nusu Fainali ya michuano hiyo. Tusker ni kinara wa kundi kwa pointi zake saba na Simba imeingia kama mshindi wa pili kwa pointi zake tano.
    Wachezaji wa Simba SC walioitwa Stars ni kipa Juma Kaseja, mabeki Amir Maftah na Shomari Kapombe, viungo Amri Kiemba na Mwinyi Kazimoto na mshambuliaji Mrisho Ngasa.
    Katika wachezaji wote hao walioitwa Stars, walio kwenye kikosi cha Simba kinachocheza Kombe la Mapinduzi ni Kapombe na Mwinyi Kazimoto pekee. Kaseja, Ngassa, Kiemba ni majeruhi, wakati Amir Maftah imeelezwa ana madai yake anayosubiri alipwe ndipo ajiunge na timu.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA A YAJITOA KOMBE LA MAPINDUZI LICHA YA KUTINGA NUSU FAINALI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top