• HABARI MPYA

    Monday, May 07, 2012

    MAN CITY WATAKUWA 'MAFALA' WAKIUKOSA UBINGWA


    Tevez na Silba kushoto

    SAWA soka inaundwa na maajabu, lakini sijui kama hilo linaweza kutokea hapa. Ni katika vita ya ubingwa wa Ligi Kuu England kwa msimu huu.
    Haitashangaza kama Ligi Kuu itaanza kulipamba kwa vitambaa vya rangi ya bluu taji hilo, wakisubiri kufikisha Etihad Stadium Jumapili hii ili kukabidhiwa wenyewe ‘mwali’ wao.
    Labda tetemeko la ardhi au masahibu mengine ya mwenyezi Mungu ndiyo yatakayoizuia Manchester City kutawazwa mabingwa kwa mara ya kwanza baada ya kusubiri kwa miaka 44.
    Wapinzani wao? Kikosi cha QPR – ambacho kitaamua hilo inanolewa na Mark Hughes, kocha aliyetimuliwa kiutata na Man City kumpisha Roberto Mancini.
    Na rekodi yao ya ugenini kwa msimu huu kwa kikosi hicho cha QPR, hakuna atakayetoa sarafu yake kwa upande wa Man City kunyakua ubingwa huo.
    Baada ya mabao maridadi kabisa katika kipindi cha pili yaliyofungwa na Yaya Toure dhidi ya Newcastle juzi, kwa sasa njia safi kabisa Etihad kumpokea ‘mwali’ huyo.
    Hakika, ilikuwa ni siku njema kabisa kwa nyota huyo wa Ivory Coast – aliyesherehekea ‘birthday’ yake kwa kutimiza miaka 29.
    Ilikuwa ni siku ya kukumbukwa kwa mchezaji huyo ambaye aliwapa shangwe mashabiki wa klabu hiyo kwa mara ya kwanza tangu 1968.
    Mancini nyuma ya Balotelli
    Usiku wa juzi, bado Mancini aliendelea kupuuza kwamba ubingwa ni wao msimu huu, licha ya mpinzani wake kocha wa Manchester United, Alex Ferguson kudai kwamba Man City imeweka “mikono miwili” kwenye taji hilo.
    “Hakuna kilichoamriwa hadi sasa,” alisema Muitaliano huyo. “Tuna mechi nyingine ngumu Jumapili ijayo — kama ilivyokuwa leo (juzi).”
    QPR wagumu? Si timu ya kubeza, Roberto Mancini — napaswa kulitambua hilo na kufahamu kwamba heshima ya mashabiki wa City isije ikachafuka mwisho wa mchezo wa Jumapili hii.
    Kama kuna timu ambayo unaweza kucheza dhidi yao na kuwa na uhakika wa kunyakua taji ni QPR — licha ya kwamba kikosi hicho kinahitaji pointi moja kujinusuru kutoka kwenye hatari ya kushuka daraja.
    Klabu hiyo ya London Magharibi imekuwa na rekodi ya kupoteza mechi nyingi za ugenini — mechi 13 — ikiwa ni zaidi ya timu yoyoye kwenye ligi hiyo.
    Tangu walipopata ushindi wao wa mwisho dhidi ya Stoke, Novemba 19, wamepoteza mechi 10 na kutoka sare mbili katika mechi zao za 12 za hivi karibuni walizocheza nje ya Loftus Road.
    Kwa mtazamo huo na Man City ikiwa ilipata sare kwenye mchezo wao wa pili wa ligi msimu na kushinda zote walizocheza nyumbani — kwa hilo ile subira ya muda mrefu imefika ukingoni.
    Tevez na Balotelli
    Baada ya kufunga bao la pili, Yaya Toure alikuwa na uhakika mkubwa kwamba kikosi hicho kimeonyesha bayana kuhusu uwezo wao wa kunyakua ubingwa kwa msimu huu.
    Mashabiki wa Man City wakawa na uhakika na kuimba: “Na sasa mmetuamini....tunakwenda kunyakua ubingwa wa ligi.”
    Bao hilo la pili lilibainisha kila kitu kwamba huu ni msimu mzuri kabisa kwa Man City na hakuna kitachoweza kuwazuia katika kutimiza ndoto yao ya kunyakua ubingwa.
    Wakati walipoweza kuifunga Newcastle kwa ‘counter-attack’, City ilionyesha kuwa na uchu wa kufunga baada ya kwenda mbele wachezaji wanne dhidi ya wawili wa Newcastle.
    Sergio Aguero, alikimbia na mpira upande wa kushoto, akamtafuta Nigel de Jong, aliyepiga ndefu kwa Gael Clichy – beki huyo wa pembeni alimpenyezea Yaya Toure, ambaye alitulia na kumchambua kipa Mdachi Tim Krul.
    Kwenye benchi lao, David Platt alionekana kuchanganyikiwa, Mancini alipiga ngumi upepo na Brian Kidd alichofanya ni kuangusha tabasamu tu.
    Kilikuwa kipindi chao cha kufurahi na kusahau kilio cha 1993 – wakati walipobanwa Old Trafford na kikosi cha Alex Ferguson kikifanikiwa kunyakua ubingwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 26.
    Baada ya kuona timu yao inapata ushindi safi katika mechi hiyo ngumu kabisa, waliamini hakuna kitachoweza kuwazuia katika kunyakua ubingwa huo msimu huu.
    Ilikuwa siku mbaya kwa Newcastle – kwasababu walitambulisha sanamu ya gwiji wao, Bobby Robson na kisha wanakumbana na kichapo.
    Kwa Man City iliongoza ligi hiyo kwa karibu miezi mitano kabla ya United kupoka usukani na kutishia kulinyakua taji hilo.
    Baada ya kichapo kutoka kwa Arsenal – ilikuwa ni siku ambayo Mancini aliamini kwamba ubingwa tena kwao basi, lakini baada ya United kuteleza na kisha kufanikiwa kuwafunga kwa sasa kila kitu kipo mikononi mwao.
    Kun Aguero
    City kwa sasa itaamua yenyewe, kunyakua taji au kulitoa sadaka kwa mahasimu wao United kwa maana ya kushindwa kupata ushindi katika mchezo wao wa mwisho dhidi ya QPR.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAN CITY WATAKUWA 'MAFALA' WAKIUKOSA UBINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top