• HABARI MPYA

    Friday, May 04, 2012

    OKWI, KIIZA, NIYONZIMA, ASAMOAH KUTOCHEZA JUMAPILI


    Okwi
    Na Khatimu Naheka
    IDARA ya Uhamiaji Tanzania imesema itawaondoa nchini muda wowote wachezaji Haruna Niyonzima, Hamis Kiiza, Kenneth Asamoah wa Yanga na Emmanuel Okwi (Simba).
    Niyonzima

    Tamko hilo limetolewa jana na Naibu Kamishna wa Idara ya Uhamiaji, Abbas Mussa Orovya, alipozungumza na Championi Ijumaa juu ya uhalali wa wachezaji hao kuendelea kufanya kazi nchini.
    Orovya alisema wachezaji hao wa Yanga taratibu zao za kuishi nchini zilifanyika na kufikia hatua nzuri lakini hazijakamilika, hivyo muda wowote wanaweza kuwaondoa kwa kuwa taratibu ni lazima zikamilike, wakati Okwi kibali chake cha muda kimeisha.
    “Kibali cha Okwi kinatakiwa kifanyiwe mchakato mpya kwa kuwa muda wake umeisha na alitakiwa kufikia Mei (mwaka huu) awe na kibali kipya. Hawajaja mpaka sasa kufanya mchakato wa kibali kipya.
    “Kabla hatujawatimua, Yanga waje kukamilisha vibali vya Asamoah, Niyonzima na Kiiza kwa kuwa mchakato upo kwenye hatua nzuri,” alisema Orovya.
    Kuhusu wachezaji wa kimataifa wa Azam, alisema wote walikamilisha michakato ya kuishi na kufanya kazi nchini kihalali.
    “Wiki iliyopita tuliwasiliana na TFF kupitia kwa Mkurugenzi wa Ufundi, Sunday Kayuni, juu ya hali halisi na tutalifanyia kazi suala hilo kwa umakini mkubwa. Pia tunawakumbusha viongozi wa klabu nyingine,” alisema.
    Mara kadhaa, uongozi wa klabu za Yanga na Simba umekuwa ukifanya uzembe kuhusiana na vibali vya waajiriwa wao wa kigeni, hali ambayo husababisha tafrani na Idara ya Uhamiaji.
    Kiiza

    GAZETI LA CHAMPIONI
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: OKWI, KIIZA, NIYONZIMA, ASAMOAH KUTOCHEZA JUMAPILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top