![]() |
| Wachezaji wa Simba SC |
SUDAN iko hatarini kufungiwa kucheza michuano ya klabu Afrika, kutokana na malalamiko ya timu mbili, Simba SC ya Tanzania na TP Mazembe ya DRC kutumwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) dhidi ya vitendo vya kihuni na visivyo vya kiunamichezo ambavyo klabu hizo zimefanyiwa nchini humo.
Simba SC imetuma malalamiko Afrika (CAF) leo kutokana na vitendo visivyo vya kiuanamichezo inavyofanyiwa nchini Sudan inakosubiri pambano lake dhidi ya Al Ahly Shendy kesho.
Taarifa ya Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamgwa kutoka Sudan, imesema kwamba tangu wawasili nchini Sudan juzi, wamekuwa ikifanyiwa vitendo
visivyo vya kiungwana na wenyeji wake, Shirikisho la Soka Sudan (SAF) na Al
Ahly Shendi.
Jana, Simba ilifanyiwa vitendo hivyo kabla ya kwenda katika mji wa
Shendi itakakochezwa mechi hiyo na baada ya kufika katika mji huo uliopo
takribani kilomita 170 kutoka mji mkuu Khartoum.
Simba iliwasili Shendi majira
ya saa mbili usiku kwa saa za Sudan (sawa na saa za huko) baada ya safari ya
takribani masaa manne kutoka Khartoum.
Safari ya kutoka Khartoum hadi Shendi
ilianza majira ya saa kumi jioni na timu ikafika saa mbili usiku, kwa maana ya
masaa manne ya safari ya barabara jambo ambalo ni kinyume cha kanuni za CAF
zinazozungumzia umbali usiozidi masaa mawili.
Ingawa kanuni ya CAF kifungu cha
5 (3) kinazungumzia umbali wa kusafiri kwa basi usizidi kilomita 200, Simba
inaweza kutuma malalamiko kwamba kutoka Khartoum hadi Shendi ni zaidi ya
kilomita 150 kwa vile si haiwezekani kutumia masaa manne kwa umbali huo.
Zaidi
ya usumbufu huo wa kusafiri muda mrefu, Simba pia inajiandaa kutuma malalamiko
CAF kwa vile hoteli waliyopangiwa haina kiwango kinachokubalika na shirikisho
hilo.
Kwa mujibu wa kanuni ya CAF kifungu cha 7 (c), timu mwenyeji inatakiwa
kuhakikisha kuwa timu mgeni inaishi katika hoteli ya daraja la kwanza na pia
msafara mzima unakaa katika hoteli moja.
Hata hivyo, Simba imewekwa katika
hosteli inayofanana na mabweni ya wanafunzi na imepewa vitanda 24 tu huku
msafara ukiwa na watu takribani 30.
Wakati ilipokuja Tanzania, Simba ililipia
gharama za watu 30 wa timu hiyo na kulikuwa na makubaliano kwamba na wao
watafanya hivyo wakati Wekundu watakapokwenda Sudan.
Kutokana na ukosefu huo wa
vyumba, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alilala kwenye makochi ya chumba
cha mapokezi pamoja na kocha msaidizi wa makipa wa Simba, James Stephan Kisaka.
Viongozi wengine wa Simba, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Swedy Mkwabi na
kiongozi wa msafara, Hussein Mwamba ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
TFF, pia walikosa pa kulala na hivyo wakalazimika kwenda kulala nje ya hosteli
hiyo ya Shendi.
Wakizungumzia hali hiyo, wawakilishi wa timu ya Shendi walidai
kwamba inatokana na ukweli kuwa mji wao ni mdogo na hakuna hoteli nyingine
kubwa kuliko hiyo mji mzima. “Kusema kweli mlitupokea vizuri sana tulipokuja
Dar es Salaam na hatuna malalamiko yoyote yale. Hata hivyo, huu ndiyo uwezo
wetu na hatuna la kufanya.
Hata Ferroviaro ya Msumbiji walikaa hapahapa
walipokuja hapa, alisema Hamdy Ibn Hossein,” mwakilishi wa Shendi. Rage alisema
Simba itacheza mechi yake dhidi ya Shendi wakati tayari ikiwa imewasilisha
malalamiko yake CAF kupitia kwa kamisaa wa pambano hilo ambaye alitarajiwa
kuwasili hapa jana jioni (Ijumaa).
“Hawawezi kusema kwamba kwa sababu
Ferroviarro walikaa hapa basi na sasa tukae. Hii si hoteli inayosemwa na CAF,
hii ni hosteli ya kuweka wanafunzi. Huu ni uvunjaji wa wazi wa kanuni na
tunaukataa,” alisema.
Ingawa Simba iliwasili Shendi saa mbili usiku, chakula
kilicheleweshwa hadi saa sita usiku ambako wachezaji waliamshwa kula jambo
linaloonyesha kuwa hujuma zimepangwa.
Jana, magazeti ya Tanzania yaliripoti
kuhusu Simba ilivyotelekezwa katika hoteli ya Safiga jijini Khartoum kuanzia
saa nne asubuhi hadi saa kumi jioni bila ya taarifa yoyote huku wenyeji wakidai
wamekwama kwenye foleni.
Kutokana na Simba kuingia Shendi usiku, Kocha Mkuu,
Milovan Cirkovic, aliamua kuwapa wachezaji mapumziko hadi jana lakini wachezaji
waliamua kujifanyia mazoezi wenyewe.
Mmoja wa wachezaji waliokuwa wakijifanyia
mazoezi binafsi ambayo yanajulikana kwa jina la individual, alikuwa ni Haruna
Moshi Boban ambaye alikutwa akifanya mazoezi ya peke yake kuzunguka eneo la
hosteli ilikofikia timu.
“Tangu juzi hatujafanya mazoezi kwa sababu ya safari
na vituko vya hawa wenyeji wetu. Nimeamua kujifua mwenyewe kwa sababu ukikaa
muda mrefu bila mazoezi hata mwili nao unazoea ulegevu. Ndiyo maana najifua,”
alisema.
Zaidi ya Boban, wachezaji wengine waliokutwa wakifanya mazoezi majira
hayo ya saa tano usiku ni Mwinyi Kazimoto, Juma Kaseja, Patrick Mafisango,
Shomari Kapombe, Uhuru Selemani na Emmanuel Okwi.
Katika mechi ya kwanza
iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 na
inahitaji sare ya aina yoyote au kufungwa chini ya mabao 3-0 ili kusonga mbele.
Wakati Simba wakifanyiwa hivyo, mashabiki wa klabu ya Al Merreikh ya Sudan
wameufanyia fujo msafara wa klabu ya Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mjini Khartoum, wakidai na wao walipokewa vibaya na
klabu hiyo mjini Lubumbashi wiki mbili zilikzopita.
Mazembe yenye washambuliaji wawili
Watanzania, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu ipo Khartoum kwa
ajili ya mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Merreikh,
hatua ya 16 Bora.
Katika vurugu hizo, basi walilokuwa
wamepanda wachezaji wa Mazembe limevunjwa vioo na athari zaidi ikiwemo hali
hali za wachezaji bado hazijajulikana.
Sasa mechi hiyo iliyopangwa kufanyika
kwenye Uwanja wa Omdurman, hatima yake ipo mikononi mwa Shirikisho la Soka
Afrika (CAF)- ambayo inatarajiwa kuchukua hatua muda mfupi ujao, kubwa zaidi
ikitarajiwa kuifuta mashindanoni Merreikh na kuifungia hivyo Mazembe kusonga
mbele.
Katika mchezo wa kwanza, Samatta, maarufu
kama Sama Goal, aliibuka shujaa kwenye Uwanja wa Kibassa Maliba, baada ya
kufunga bao moja katika ushindi wa 2-0.



.png)
0 comments:
Post a Comment