• HABARI MPYA

    Friday, May 04, 2012

    WACHEZAJI YANGA WAWATUMIA SALAMU WAZEE YANGA


    Waandishi wetu
    WAKATI uongozi wa Yanga ukiendelea kuwatengeneza kisaikolojia wachezaji wake kwa kuwalipa mapema mishahara na posho kuelekea pambano la kufunga msimu wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba Jumamosi wiki hii, baadhi ya wachezaji wameeleza kukerwa na mgogoro unaoendelea ndani ya klabu hiyo ya Jangwani.

    Kwa wiki nzima sasa, uongozi wa Yanga umeelemewa na shinikizo toka kwa wazee wa klabu hiyo waliodhamiria kuchukua usimamizi wa timu kwa kile walichokibainisha kuwa ni uongozi mbovu uliosababisha timu kufanya vibaya.

    Wakiongea na Mwananchi jana kwa nyakati tofauti huku baadhi yao wakitaka majina yao yasiandikwe kwenye gazeti, walisema pamoja na kutosimama upande wowote kuunga mkono pande zinazolumbana, bado wanaamini madhara ya mgogoro huo yanawagusa hata wao.

    Walisema pamoja na wazee wa klabu hiyo kususa uamuzi wao wa awali kutaka kuichukua timu, bado haimaanishi kwamba mgogoro umefika tamati na kuzitaka pande zote mbili kuafikiana haraka hasa kipindi hiki kuelekea mechi dhidi ya Simba.

    Akielezea hali hiyo ya Yanga, kipa Shaban Kado alisema, "Mgogoro siyo mzuri ukizingatia tupo kwenye kipindi kigumu na mechi ya watani zetu, tungeomba wazee wetu, viongozi wote kwa pamoja tushirikiane, tushikamane,  tuhakikishe tunashinda mechi yetu ya Jumamosi.

    "Itakuwa mbaya zaidi kama tutapoteza tena mechi yetu dhidi ya Simba, siku zote naamini kidole kimoja hakivunji chawa. Sitegemei kwenye mgogoro timu inaweza kufanya vizuri, ningependa hizi kelele za mgogoro zifike tamati," alisema Kado.

    Kado alisema, yeye na wachezaji wenzake wasingependa kuwa sehemu ya migogoro kwa sababu wameajiriwa kucheza soka na mambo ya utawala yana watu wake wa kusimamia.

    "Kelele hizo na sisi tuanazisikia na kuzipuuza kwa sababu hazituhusu na hatupaswi kuziingilia kwa sababu siyo zilizotuleta Yanga.

    "Kazi iliyotuleta Yanga ni moja tu .... kucheza soka, wanaolumbana wana mambo yao wanataka, sisi hayatuhusu," alisema mchezaji wa kiungo wa Yanga ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini.

    Alisema jambo la msingi, yeye na wachezaji wenzake hawaungi mkono upande wowote, ila wanaangalia kinachowafanya kulipwa mishahara Yanga.

    Aidha, Shamte Ally akieleza kukerwa na kinachoendelea Yanga alisema: "Sio muda muafaka kulumbana na kuwekeana bifu. Viongozi na wazee wetu wanatakiwa kujenga mshikamano tunaelekea mechi ya lawama dhidi ya Simba."

    Ally alisema baada ya kupoteza ubingwa msimu huu, wamebaki na fursa moja ya kulinda heshima yao, nayo ni kuifunga Simba kwenye mchezo wa Jumamosi wiki hii.

    Alisema kinachotakiwa sasa ni kuweka pembeni tofauti zilizopo na kujiandaa vizuri na mchezo dhidi ya Simba. "Tunapaswa kulinda heshima yetu kwa kuifunga Simba baada ya kupoteza ubingwa," alisema.

    Kwa upande wake, Hamis Kiiza alisema kuwa pamoja na kuzingatia zaidi kilichompeleka Yanga, lakini hafurahishwi na hali ilivyo. "Huu ni mgogoro wa kiutawala, mimi sina cha kusema zaidi ya kufanya kilichoniweka Yanga," alisema Kiiza.

    "Mimi nasikia kwenye vyombo vya habari taarifa za mgogoro, nimetumia muda mwingi kuwatuliza wenzangu kutojihusisha na hali iliyopo ila tuweke mkazo kwenye mchezo wa mwisho," alisema Kiiza.

    Kwa upande wake, Rashid Gumbo alisema, "mimi sipendi kabisa kusikia mambo hayo, kwanza hayanihusu tuwaachie wenyewe, sisi tunataka kucheza soka malumbano siyo kazi yetu."

    Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Yanga, Llyod Nchunga amesema wachezaji wote wamelipwa mishahara na posho zao walizostahili baada ya kushinda mechi za Ligi Kuu.

    "Hakuna malimbikizo ya mishahara, tumeshawalipa posho ya michezo yote walioshinda kasoro ile mitatu tu ambayo walipoteza, sasa hivi tunawajenga wachezaji wetu kisaikolojia wajue wao ni mabingwa wa Kombe la Kagame, wasisikitike kupoteza nafasi ya kutetea ubingwa," alisema Nchunga.

    Akiongelea maandalizi ya pambano hilo, Kocha Fred Minziro alisema, "Wachezaji wote wako fiti, nachokifanya hivi sasa ni kuwajenga kisaikolojia na nimeshawambia kuwa mgogoro wa viongozi hautuhusu, sisi ni waajiriwa tu Yanga, viongozi watajua wenyewe watamalizaje mgogoro wao.

    Akieleza mchezo huo, Minziro alisema,"Simba wanaingia uwanjani kusaka ubingwa, sisi tutacheza kulinda heshima yetu."

    Imeandikwa na Sweetbert Lukonge, Jessca Nangawe, Vicky Kimaro na Sosthenes Nyoni
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WACHEZAJI YANGA WAWATUMIA SALAMU WAZEE YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top