![]() |
Katibu wa Baraza la Wazee wa Yanga, Mzee Ibrahim Ally Akilimali katikati |
WAZEE wa klabu ya Yanga na wanachama
maarufu kwa migogoro, wakiongozwa na Mzee Ibrahim Ally Akilimali na Bakili
Makele, leo wameibuka wakimpiga mkwara Mwenyekiti wa klabu hiyo, Wakili Lloyd Baharagu
Nchunga, asithubutu kufukuza mchezaji yeyote, bali aondoke yeye.
Nchunga alikaririwa jana akisema kipigo cha
mabao 5-0 kutoka kwa wapinzani wao wa jadi, Simba Jumapili kilitokana na hujuma
iliyofanywa na wana Yanga wenzao- kiasi kwamba akaustaajabu u-Yanga wana wana
Yanga hao.
Nilifurahishwa na kauli ya jemedari wa
migogoro, Bakili, akisema kwamba Nchunga asifukuze mchezaji yeyote kwa sababu,
hii si mara ya kwanza Yanga kufungwa tano.
Ukifuatilia historia ya mechi hii, kabla
haijachezwa, kauli za wazee hao kabla ya mechi na sasa baada ya mechi unaweza
kupata picha fulani, kwamba Nchunga yuko sahihi kusema kuna hujuma.
Wazee hawa walisema kabla ya mechi, hata Yanga
ikiifunga Simba, lazima Nchunga aondoke. Walisema hivyo kwa sababu wanajua Nchunga
amekuwa na rekodi nzuri ya kuifunga Simba na kutwaa mataji makubwa, likiwemo
Kombe la Kagame, ambalo mara ya mwisho klabu ililitwaa mwaka 1999.
Lakini kusema; Hata akiifunga SImba, lazima
aondoke- maana yake nini?
Walitengeneza mazingira ya timu kufungwa
ili kuhalalisha safari ya Nchunga? Kama hivyo ndivyo wamefanikiwa- lakini
nataka kuwaambia wazee hao na wote walioko nyuma yao kwamba, wameshika udhu kwa
najisi.
Najisi ni nini? Ni uchafu unaomfanya muumini wa dini ya
kiislamu apoteze udhu- kiasi kwamba hata ibada yake haiwezi kuswihi.
Kwa mfano, maji masafi, lakini kumbe mtu
aliyakojolea, japo tone dogo tu la mkojo, likazidiwa na maji- ila hayo maji
mfuate Mufti kamuulize yanaswihi kushikia udhu? Atakuambia hapana usithubutu.
Sasa wazee wa Yanga wameshika udhu kwa
najisi. Je, ni safi hao?
Lengo ni kumng’oa Nchunga. Sadakta. Lakini kitendo
cha kufanya jitihada zozote, bila kujali maslahi ya klabu yao, ili mradi tu
wamuondoe Nchunga klabuni ni kosa kubwa.
Naamini dhambi hii, itawatafuna wahusika-
kama historia haitafutika, Yanga ilifungwa 5-0, Mei 6, 2012.
Kitendo cha uongozi wa Yanga, chini ya
Mwenyekiti wake Nchunga kuthubutu kumtumia beki Nadir Haroub Cannavaro katika
mechi na Coastal Union ya Tanga, kilikuwa kinatosha kabisa kama sababu ya
kuwawajibisha viongozi katika Mkutano Mkuu.
Lakini kwa sababu hawakuwa wenye kujiamini
kama wanweza kuwa na hoja za kupambana naye kwenye mkutano Mkuu, wakaona
waongeze sababu. 5-0.
5-0 hajafungwa Nchunga, imefungwa Yanga. Wajukuu
wa Bakili wakikua wataikuta historia hiyo.
Siku hizi kuna Yanga maslahi, na Yanga damu
na huu ndio wakati mwafaka kuanza kuwachanganua yupi ni yupi.
Bakili anasema Nchunga asifukuze mchezaji
kwa sababu hii si mara ya kwanza Yanga kufungwa 5-0.
Popote alipo Bakili ajiulize hatua gani
ilichukuliwa na Yanga, chini ya Mwenyekiti wake Jabir Idrisa Katundu Julai 2, mwaka
1994, baada ya Yanga kufungwa 4-1 na Simba?
Kama hajui nitamkumbusha, walifukuzwa
wachezaji karibu wote, wakabaki wachache tu kama Kenneth Mkapa, Constantine
Kimanda, Sekilojo Chambua, Sanifu Lazaro ‘Tingisha’ na Mohammed Hussein
‘Mmachinga’, wengine wote walitimuliwa kwa tuhuma za hujuma.
Baada ya hapo, Yanga iliundwa na wachezaji
waliokuwa wakiandaliwa na Tambwe Leya (sasa marehemu) katika kikosi cha pili,
ambao ni pamoja na Godwin Mashoto (sasa marehemu), Mzee Abdallah, Anwar Awadh,
Maalim Saleh ‘Romario’, Nonda Shaaban na wengineo, waliosajiliwa kutoka timu
mbalimbali kuimarisha kikosi kama Bakari Malima, Reuben Mgaza waliotoka Pan
African.
Sasa iweje leo Bakili anazungumza tena
nyumbani kwa Mzee Katundu aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga wakati wa 4-1 akimzuia
Nchunga kufukuza wachezaji wasio waaminifu?
Na kwa nini sasa akina Bakili awatetee
wachezaji? Inatia shaka. Lakini mimi nawashangaa wana Yanga wa leo, wanaokubali
kuibeba fedheha hii kwa urahisi tu.
Inasikitisha, Yanga imefikia hapa- na kwa
mtaji huu daima wataendelea kukodolea macho mafanikio ya Simba. Na baada ya
muda mrefu wa kuizungumzia 6-0 kama kipigo cha kihistoria, inapoelekea Yanga
vipigo kama hivyo, vitakuwa vya kawaida.
Kumkubali au kumkataa kiongozi ni demokrasia,
lakini tena inafikia hadi watu wanahujumu timu zao wenyewe? Hapa ilipofikia
sasa tukae mkao wa kula, maana huwezi jua baada ya hili lingine lipi litafuata.
Zamani wazee wetu walikuwa wanasema mtoto akikunyea
mkononoi, hauukati, unausafisha, lakini wazee wa leo wa Yanga wanachoma moto
nyumba yao, kisa adui kaingia. Nani anapoteza? Nachoweza kusema tu, wazee wa
Yanga wameshikia udhu najisi. Alamsiki!
0 comments:
Post a Comment