• HABARI MPYA

    Friday, August 24, 2012

    YANGA NA RAYON LEO, KAGAME ASHEREHEKEA TAJI NA YANGA

    Kikosi cha Yanga
    Na Mahmoud Zubeiry
    MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Yanga SC ya Dar es Salaam, watacheza mechi ya kwanza katika ziara yao nchini Rwanda kesho Uwanja wa Amahoro mjini Kigali, dhidi ya mabingwa wa zamani wa Afrika Mashariki na Kati pia, Rayon Sport.
    Leo Yanga watatembelea Ikulu ya Rwanda, walipoalikwa na rais Paul Kagame kupeleka Kombe la Afrika Mashariki na Kati, ambalo tangu mwaka 2002 mfadhili wake mkuu na mlezi wake ni Rais Kagame.
    Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb ameiambia BIN ZUBEIRY kwa simu kutoka Kigali kwamba, timu hiyo baada ya kufika nchini humo jana, ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Nyamirambo na leo asubuhi itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Amahoro.
    Bin Kleb alisema kwamba Yanga itashuka dimbani kumenyana na Polisi Jumapili na kwa mujibu wa ratiba ya awali, wanatakiwa kurejea Dar es Salaam Jumatatu.
    Hata hivyo, Bin Kleb alisema wanafanya mipango ya kurefusha ziara yao nchini humo na kama watafanikiwa watacheza mechi zaidi.  
    Awali, Yanga ilikuwa icheze pia na mabingwa wengine wa zamani wa Kombe la Kagame, APR, lakini kutokana na timu hiyo kukabiliwa na mgogoro hivi sasa uliosababisha kufukuzwa kwa kocha Mholanzi, Ernest Brandy na nafasi yake kupewa kocha mzalendo kwa muda, imeshindwa kucheza.
    Katika ziara hiyo, Yanga haijaambatana na mfungaji bora wa Kombe la Kagame, Said Bahanuzi ambaye amebaki Dar es Salaam kwa matatizo ya kifamilia. Yanga imekwenda Rwanda na msafara wa watu 42, wakiwemo wachezaji 28, Maofisa watano wa benchi la Ufundi na viongozi wanane.
    Viongozi walio na timu Kigali ni Mwenyekiti, Yussuf Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini Mama Fatma Karume, Francis Kifukwe na Seif Ahmed ‘Magari’ sambamba na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Abdallah Bin-Kleb na Salum Rupia.
    Benchi la ufundi ni kocha mkuu; Tom Saintfiet, Kocha Msaidizi Fred Felix Minziro, Meneja Hafidh Saleh, Daktari, Sufiani Juma na Mtunza vifaa Mahmoud Omary ‘Mpogolo’, wakati wachezaji ni makipa: Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Said Mohamed. Mabeki Shadrack Nsajigwa, Godfrey Taita, Juma Abdul, Oscar Joshua, Stefano Mwasyika, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan, Ibrahim Job, Ladisalus Mbogo; viungo Athumani Iddi ‘Chuji’, Juma Seif ‘Kijiko’, Salum Telela, Simon Msuva, Shamte Ally, Omega Seme, Idrisa Rashid, Nizar Khalfan, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Rashid Gumbo, Nurdin Bakari na washambuliaji; Hamis Kiiza ‘Diego’, Jerry Tegete na Didier Kavumbangu.
    Yanga ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo wiki mbili zilizopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
    Hiyo kwa ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo, Yanga inatwaa Kombe hilo, baada ya awali kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba katika fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth Asamoah ambaye ametemwa, ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo refa alilikataa.
    Yanga ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka 1975 ikiifunga tena Simba katika fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara ‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
    Ikachukua tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo, Kampala, Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Said Nassor Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) na Edibily Jonas Lunyamila.
    Ilichukua tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa, Uwanja wa Nakivubo, kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, Yanga ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru kutangulia kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter akicheza penalti mbili za Waganda.   
    Aidha, kwa kutwaa Kombe hilo chini ya Mbelgiji huyo, Yanga imeendeleza rekodi yake ya kutwaa mataji ya michuano hiyo, chini ya makocha wa kigeni baada ya mwaka 1975 kuchukua chini ya Tambwe Leya aliyekuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, (sasa marehemu), 1993 chini ya Nzoyisaba Tauzany aliyekuwa raia wa Burundi kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, mwaka 1999 chini ya Raoul Shungu wa DRC na mwaka jana chini ya Mganda, Sam Timbe. 
    Rais Kagame akisalimiana na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Yanga, Mama Fatma Karume

    MEZA YA MAPROO; Hapa kuna Mbuyu Twite, Hamisi Kiiza aliyeipa mgongo kamera, Didier Kavumbangu kushoto na Yaw Berko anayetazajma kamera

    Wachezaji

    Rais Kagame akisalimiana na kocha wa Yanga, Tom Saintfiet


    Wachezaji wa Yanga wakims

    Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' akiwa na kocha Saintfiet, wakimkabidhi Kombe Rais Kagame 
    Mwenyekiti wa Yanga, Yussufr Manji akizungumza kitu mbele ya rais Kagame

    Sief Ahmad Magari akimkabidhi jezi ya Yanga Rais Kagame mbele ya Mama Fatma Karume

    Rais Kagame akizungumza na Yanga

    Rais Kagame akizungumza na Mwenyekiti wa Yanga, Manji

    Rais Kagame katika picha ya pamoja na Yanga. PICHA ZOTE NA SALEH ALLY, MHARIRI KIONGOZI GAZETI LA CHAMPIONI

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA NA RAYON LEO, KAGAME ASHEREHEKEA TAJI NA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top