Na Ally Mohamed, Zanzibar
LIGI Kuu ya
Zanzibar, maarufu Zanzibar Grand Malt Premier League imeendelea tena leo kwa
michezo miwili.
Uwanja wa
Amaan mjini Unguja, Malindi ambao wameinunua timu ya Miembeni SC, waliteremka
uwanjani kuivaa Bandari ambayo imepanda daraja msimu huu, katika mechi hiyo
Bandari wameianza vyema ligi hiyo baada ya kuchomoza na ushindi wa mabao 3-2. Mabao
ya Bandari yalifungwa na Mussa Omar katika dakika ya 31, Haisam Khamis dakika
ya 57 na Shariff Kitwana katika dakika ya 78, wakati mabao ya Malindi yalifungwa
na Amour Suleiman dakika ya 44 na 68.
Huko
kisiwani Pemba, wawakilishi wa Zanzibar katika michuano ya Kombe la Shirikisho
Afrika mwakani, Jamhuri wakicheza na Duma ambayo inamilikiwa na Jeshi la
Kujenga Uchumi (JKU) wameanza vizuri baada ya kuchomoza na ushindi wa mabao
2-0, yaliyotiwa kimiani na Mfaume Shaaban katika dakika ya saba na 72.
Ligi hiyo
inatarajia kuendelea tena kesho, kwa mchezo mmoja ambao utapigwa Uwanja wa
Amaan ukiwakutanisha Mtende Rangers na Zimamoto mechi itakayoanza saa 10:30
jioni.
Mapema jana,
pazia la ligi hiyo lilifunguliwa mechi mbili kuchezwa katika viwanja viwili
tofauti, kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja, Mabaharia wa KMKM walikutana
na Mafunzo, ambapo mechi hiyo imemalizika kwa Mafunzo kuchomoza na ushindi wa
bao 1-0, bao hilo pekee likipatikana katika dakika ya tano, mfungaji Mohammed
Abdulrahman.
Huko
kisiwani Pemba nako ilipigwa mechi moja ikiwakutanisha mabingwa watetezi wa
ligi hiyo, Super Falcon na Chipukizi ambapo kwa mara nyengine tena Super Falcon
ambao ni wawakilishi wa Zanzibar katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani,
wamefungwa 2-0.
Hiyo ni
mechi ya sita mfululizo Super Falcon wanapokea kipigo, wakianzia katika
michuano ya BancABC Super 8, ambapo walipoteza mechi zao zote 3 za hatua ya
makundi, kabla ya kukubali kipigo cha 3-1 kutoka kwa Jamhuri katika mechi ya
Ngao ya Jamii iliyochezwa Septemba 1, mwaka huu Uwanja wa Amaan na juzi
wakicheza na Coastal Union ya jijini Tanga katika mechi ya kirafiki, mchezo
uliochezwa Uwanja wa Ngome, Fuoni, Wilaya ya Magharibi, Unguja walifungwa 2-0.
Ligi kuu ya
Zanzibar, ambayo msimu huu inafahamika kwa jina la Zanzibar Grand Malt Premier
League kutokana na mdhamini kinywaji cha Grand Malt, inashirikisha timu 12,
huku timu 8 zikitoka kisiwani Unguja na timu 4 zikitoka kisiwani Pemba, timu
zinazotoka kisiwani Unguja ni Bandari,
Chuoni, KMKM, Mafunzo, Malindi, Mundu ambao wamenunua daraja kutoka kwa
Miembeni United, Mtende iliyopanda daraja msimu huu na Zimamoto.
Kwa upande
wa kisiwani Pemba ni Chipukizi, Duma, Jamhuri na Mabinwa watetezi, Super
Falcon.
0 comments:
Post a Comment