KLABU ya Liverpool FC ya England imemsajili beki Mholanzi mwenye asili ya Ghana, Jeremie Frimpong kutoka Bayer Leverkusen ya Ujerumani.
Beki huyo wa Kimataifa wa Uholanzi amesaini mkataba wa muda mrefu leo Uwanja wa mazoezi wa Wekundu hao, AXA Training Centre baada ya kufaulu vipimo vya afya.
Frimpong anayeweza kucheza pia kama winga — anatua Anfield baada ya miaka minne na nusu ya kucheza Ujerumani akiwa na Leverkusen, ambayo aliichezea jumla ya mechi 190 akifunga 30 na pasi 44 za mabao.
Frimpong alikuwa sehemu ya kikosi cha Leverkusen kilichoweka historia kwa kushinda mataji ya Bundesliga na DFB-Pokal msimu wa 2023-24 kikiweka rekodi ya kucheza mechi 51 bila kupoteza ambayo ilivunjwa kwenye Fainali ya lEuropa League.
Mafanikio binafsi kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 ni pamoja na kuteuliwa kwenye kikosi Timu ya Msimu ya Bundesliga misimu ya 2022-23 na 2023-24.
Mzaliwa huyo wa Amsterdam, Frimpong kisoka aliibukia kwenye timu za vijana za Manchester City ya England pia, kabla ya kwenda Celtic ya Scotland mwaka 2019 ambako alicheza mwaka mmoja na nusu akishinda mataji matatu ndipo akatimkia Leverkusen.
Frimpong aliichezea kwa mara ya kwanza timu ya taifa ya Uholanzi Oktoba 2023 na sasa amefikisha mechi 12 huku pia akiwa amefunga bao moja.
Namba ya jezi atakayovaa Frimpong Liverpool itatajwa baadaye kabla ya msimu mpya.
0 comments:
Post a Comment