• HABARI MPYA

    Friday, May 16, 2025

    GWIJI WA CAMEROON EMMANUEL KUNDE AFARIKI DUNIA


    BEKI wa zamani wa Kimataifa wa Cameroon, Emmanuel Jérôme Kundé amefariki dunia leo nchini kwao akiwa na Umri wa miaka 68 — Rais wa Shirikisho la Soka Cameroon (FECAFOOT) amethibitisha.
    Kundé alizaliwa Julai 15 mwaka 1956  mjini Ndom na kisoka aliibukia klabu ya Mbankomo mwaka 1973, kabla ya kuhamia Tempête de Nanga-Eboko mwaka 1975 alikocheza hadi mwaka 1977 akahamia Canon Yaoundé alikodumu kwa miaka 10. 
    Mwaka 1987 alihamishia maisha yake ya soka barani Ulaya, nchini Ufaransa ambako alichezea Stade Lavallois Mayenne kwa msimu mmoja akahamia Reims aliyoichezea pia msimu mmoja.
    Mwaka 1989 alirejea nyumbani, Cameroon na kuchezea klabu za Prévoyance Yaoundé hadi mwaka 1991 akahamia Olympic Mvolyé aliyoichezea hadi mwaka 1992.
    Ameichezea timu ya taifa ya Cameroon kuanzia mwaka 1979 hadi 1992 akihusika katika jumla ya mechi 
    102 na kufunga mabao 17.




    Kumbukumbu zake nzuri katika utumishi wake Indomitable Lions ni katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1982 nchini Hispania na 1990 nchini Italia.
    Alikuwemo pia kwenye kikosi cha Simba Wasiofungika kilichotwaa Kombe la Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 1984 nchini Ivory Coast na 1988 nchini Morocco.
    Kundé alifunga bao la ushindi katika Fainali mwaka 1988 dhidi ya Nigeria kwa mkwaju wa penalti, kabla ya miaka miwili baadaye, 1990 kufunga bao la kusawazisha kwenye mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya England kwa penalti pia timu hizo zikitoka sare ya 2–2 na mchezo ulipohamia kwenye dakika 30 za nyongeza, Gary Winston Lineker akawafungia Three Lions kwa penalti pia bao la ushindi dakika ya 105.
    Alicheza pia Fainali za AFCON mwaka 1992 nchini Senegal akiwa anamalizia soka yake Olympic Mvolyé.
    Mungu ailaze roho ya marehemu Emmanuel Jérôme Kundé mahali pema peponi. Amin. 

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: GWIJI WA CAMEROON EMMANUEL KUNDE AFARIKI DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top