![]() |
Tazama shughuli ya Sure Boy Jr. |
Na Princess Asia
SASA wako fiti kabisa na watacheza shoka ile haswa kesho, tarajia hilo. Viungo tegemeo wa Azam FC, Ibrahim Mwaipopo, Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr.’, Jabir Aziz na Hamisi Mcha ‘Vialli’ na beki wa kushoto, Salum Waziri waliokuwa majeruhi wanaendelea vizuri mazoezini.
Azam inajifua kwenye Uwanja wake wa Chamazi, Dar es Salaam na wachezaji wake wote wapo kambini hapo hapo kwenye hosteli za Uwanja huo, tayari kwa mechi ya Ngao ya Jamii kesho dhidi ya Simba, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Azam inatarajiwa kuivaa Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ikiwa ni mchezo wake wa kwanza katika historia ya Ngao hiyo.
Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0.
Ikumbukwe mara ya mwisho Simba SC ilipokutana na Azam FC, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwezi uliopita Dar es Salaam, ilifungwa mabao 3-1, yote yakifungwa na Bocco na lile la kufutia machozi kwa wekundu hao Msimbazi liliwekwa kimiani na beki mahiri Shomari Kapombe, aliyemajeruhi kwa sasa.
Katika kujiandaa na mechi hiyo, Azam imecheza mechi nne za kujipima nguvu na kushinda zote, dhidi ya Prisons 1-0, Transir Camp 8-0, Coastal Union 2-0 na Azam Akademi 4-0.
0 comments:
Post a Comment